
LAGOS, NIGERIA: Bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, Anthony Joshua, amelazwa hospitalini baada ya kupata ajali ya barabarani eneo la Makun kwenye Barabara Kuu ya Lagos–Ibadan, Jimbo la Ogun, leo.
Ofisa Uhusiano wa Umma wa Polisi wa Jimbo la Ogun, Babaseyi Oluseyi, amethibitisha tukio hilo katika taarifa iliyotolewa kwa gazeti la PUNCH la nchi hiyo.
“Kamanda ya polisi wa Jimbo la Ogun anathibitisha kutokea kwa ajali ya barabarani leo mbele ya Sinoma kabla ya Danco, kando ya Barabara Kuu ya Lagos–Ibadan. Anthony Joshua na watu wengine waliojeruhiwa wamewahishwa hospitalini,” imesema taarifa hiyo na kuongeza:
“Taarifa zaidi zitatolewa baadaye.”
Awali, iliripotiwa kuwa tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya saa 5:00 asubuhi na kwamba ajali imetokea karibu na Kituo cha Mafuta cha Danco.
Inaelezwa kwamba gari aina ya Lexus Jeep lililombeba Joshua lenye namba ya usajili KRD 850 HN liligongana na lori lililokuwa limesimama.
Mmoja wa mashahidi wa tukio ameeleza kuwa AJ alipata majeraha madogo, huku watu wawili wakifariki dunia papo hapo.
“Msafara ulikuwa na magari mawili; Lexus SUV na Pajero SUV. Joshua alikuwa amekaa nyuma ya dereva akiwa na mtu mwingine pembeni yake. Kulikuwa na abiria mmoja aliyekaa pembeni ya dereva, hivyo jumla ya watu wanne walikuwa ndani ya Lexus iliyopata ajali,” kimesema chanzo hicho huku gari la walinzi wake lilikuwa linafuata kwa nyuma.
“Mimi na mashuhuda wengine tulianza kutoa msaada na kusimamisha magari yaliyokuwa yanapita kuomba msaada. Dakika chache baadaye maofisa wa Jeshi la Usalama Barabarani (FRSC) waliwasili. Abiria aliyekaa pembeni ya dereva na yule aliyekaa pembeni ya Joshua walikuwa wamefariki dunia papo hapo.”
Katika taarifa aliyotuma kwa PUNCH Jumatatu, Oluseyi alithibitisha kuwa Joshua na watu wengine waliojeruhiwa walihusika katika ajali ya gari na waliwahishwa katika hospitali isiyotajwa.
Hivi karibuni Anthony Joshua alimchapa Jake Paul kwa Knockout ya raundi ya sita katika pambano la raundi nane lisilo la ubingwa ambalo liliuteka ulimwengu wa masumbwi kutokana na mpinzani wake kutokuwa na uzoefu mkubwa wa ngumi.