Mwaka 2008 Azam FC ilipanda daraja kushiriki ligi kuu msimu wa 2008/09.

Mwaka huo huo ikaanzisha akademi kwa lengo la kulea vijana ili kuwaandaa kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Hadi wakati huo hakukuwa na klabu nyingine yeyote yenye timu za vijana, hivyo watoto wa Azam hawakuwa na wenzao wa kushindana nao.

Ndipo viongozi wa klabu hiyo wakaenda kuiomba TFF kuanzisha mashindano ya vijana ili washindane na vijana wao.

TFF ikaupenda huo mpango lakini haikuwa na uwezo wa kifedha kuutekeleza…na ikaweka wazi hilo.

Kwa kuwa Azam FC waliyahitaji sana mashindano haya, wakatengeneza ushawishi kwa kampuni mama ya SSB inayomiliki klabu hiyo ili iyadhamini.

Ndipo ukaja udhamini wa maji ya uhai na mashindano hayo yakaitwa Kombe la Uhai…na ndivyo ligi ya vijana chini ya miaka 20 ilivyoanza.

Kwa kifupi ni kwamba ligi hiyo ilianzishwa kama wazo la Azam FC, na kwa jitihada za Azam FC.

Hiyo ni faida ya kwanza ya akademi ya Azam FC.

Matunda ya jitihada za Azam FC kwa taifa yalianza kuonesha dalili mwaka 2013 pale kikosi cha Taifa Stars kilichokuwa na wachezaji 13 kutoka Azam FC kilipoifunga Morocco 3-1 kuwania kufuzu Kombe la Dunia la 2014.

Matunda yakaiva mwaka 2019 pale Tanzania ilipofuzu kwa fainali za AFCON kule Misri.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa takribani miaka 40.

Katika kikosi kilichofuzu hadi kwenda kushiriki, Azam FC ilikuwa na mchango wa asilimia 42.

Mchango huu ni kwa wachezaji ambao aidha walilelewa Azam FC na wakaondoka, au walikuwa bado wapo Azam FC.

Kwenye harakati za kufuzu, Stars ilitumia jumla ya wachezaji 48, huku 20 wakiwa ni mazao ya Azam FC.

Na kwenye fainali zenyewe Stars ilikwenda na wachezaji 23 huku wachezaji 10 wakiwa mazao ya akademi ya Azam FC

Magolikipa

1. Aishi Manula – Simba SC.

2. Metacha Mnata – Mbao FC.

3. Gadiel Michael – Yanga SC.

4. Mohamed Hussein – Simba SC.

5. Himid Mao – Petrojet.

6. Mudathir Yahya – Azam FC.

7. Yahya Zayd – Ismailia.

8. Farid Mussa – Tenerife.

Washambuliaji

9. Rashid Mandawa – BDF.

10. Saimon Msuva – Difaa El Jadidi.

Hawa ni nje ya wale ambao hawakupita akadeki lakini wameendelezwa zaidi na Azam FC,  kama John Bocco ambaye alicheza Azam FC miaka 10 na Erasto Nyoni aliyecheza Azam FC miaka 9 kabla hawajatimkia Simba, na Aggrey Morris ambaye hadi wakati huo alikuwa Azam kwa miaka 10.

Pia Frank Domayo ambaye hadi wakati alikuwa Azam FC kwa miaka 6.

Mechi ya kwanza ya Tanzania ilikuwa dhidi ya Senegal, na Tanzania kupoteza kwa mabao 3-0.

Lakini hata hivyo, golikipa wa Stars, Aishi Manula, alifanya kazi ya ziada kwa kuokoa michomo 8 ya wazi.

Kiwango hiki kikamfanya aingie kwenye kikosi bora cha raundi ya kwanza ya mashinda hayo.

Baada ya hapo ikafuata CHAN 2020 iliyofanyika 2021.

Aishi Manula kwa mara nyingine aligonga vichwa vya habari kwa kufanya okozi nane za wazi na kuongoza.

Na sasa kwenye AFCON 2025 huko Morocco jina jipya kutoka akademi ya Azam FC linatawala.

Nalo ni la Zubery Masoud Foba, zao jingine la akademi, kutokea mji wa Musoma mkoa wa Mara.

Foba ambaye alipandishwa msimu wa 2022/23 na kuendelea kuwa chini ya makipa waandamizi akijifunza, alicheza kwenye mechi ya kwanza ya Taifa Stars kwenye kampeni za mwaka huu.

Ilikuwa dhidi ya Nigeria ambapo alifanya okozi za wazi 8 na kulistua taifa.

Japo Stars ilipoteza 2-1 lakini kipa huyo aliicheza vyema nafasi yake.

Huu ni uthibitisho kwamba akademi ya Azam haibahatishi.

Zuberi Foba anatupa uhakika kama taifa kuwa na kipa wa kumtegemea kwa miaka mingi ijayo, kutokana na umri wale.

Kwa sababu Foba ana miaka 23…kama ataendelea kuimarika na kupata uzoefu zaidi, anaweza kutawala nafasi yake kwenye kikosi cha timu ya taifa kwa miaka 10 ijayo.

Zuberi Foba na Azam FC ni kama walizaliwa kuishi pamoja.

Mwaka 2015 timu ya vijana ya Azam FC ilipata mwaliko huko Musoma kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki.

Dhidi ya Polisi Mara, mechi ambayo iliisha kwa sare ya 1-1, na dhidi ya Musoma Combine,  mechi iliyoisha kwa sare ya 3-3.

Baada ya mechi hizi, bwana mdogo mmoja…mdogo kweli, alimfuata kipa wa Azam FC na kumuomba vilinda mikono (gloves).

Akamwambia kipa yule, “Natamani sana kuwa kipa nichezee Azam kama wewe”.

Kipa aliyekuwa anaambiwa maneno haya ni Mwalo Ilunga, ambaye na yeye ni zao la akademi ya Azam FC.

Alijiunga nayo mwaka 2011 sambamba na Aishi Manula, baada ya kung’aa kwenye mashindano ya Copa Coca-Cola akiwa na timu ya mkoa wa Kigoma.

Haya ndio mashindano ambayo pia Azam FC iliyatumia kuwapata nyota wengine wengi kama Mudathir Yahya, Gadiel Michael, Sospeter Bajana, Farid Mussa na wengine wengi.

Bahati mbaya Mwalo hakufanikiwa sana kama mchezaji kwani alipata majeraha na kuacha mpira.

Baadaye akarudi nyumbani Chamazi na klabu ikamsomesha na sasa kocha wa makipa.

Wakati anarudi, Zuberi naye akawa ameshajiunga na akademi ya Azam FC.

Mwalo alikuwa tayari ameshasahau lakini sio Foba…akamkumbusha ile siku.

Mwalo akashangaa kuona ndoto ya dogo kuwa sehemu ya Azam FC ianenda kuwa kweli.

Kuanzia hapo wakawa wanaishi na kocha na mchezaji wake.

Mwaka huu Aishi Manula ambaye aliingia mwaka mmoja na Mwalo, naye akarudi nyumbani na kuifanya familia kuwa kubwa.

Foba mwenyewe amekuwa akimfuatilia sana Aishi Manula na kumuona kama shujaa wake.

Foba alikuwa anavaa jezi namba 28 ambayo pia Aishi amekuwa akiitumia tangu akiwa Azam, hadi Simba.

Lakini baada ya Aishi Manula kujiunga na Azam FC,  Foba akaivua jezi hiyo na kumpa Aishi, kwa namna anavyomheshimu.

Foba kwa sasa yuko chini ya mikono sana ya watu wawili muhimu sana kwake.

Na yeye analiweka lango la Taifa Stars katika mikono salama.

Ahsante akademi ya Azam FC…ama kwa hakika ina kitu!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *