Alipoanza kampeni zake mapema mwaka huu, mgombea urais wa chama kikuu cha upinzani, NUP, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, aliwahimiza Waganda—ikiwa ni pamoja na wasiokuwa wafuasi wake—kutumia bendera ya Uganda kama nembo ya umoja na mabadiliko ya kisiasa. Hii ni katika nchi ambayo imekuwa chini ya uongozi wa Rais Yoweri Museveni kwa takribani miongo minne.

“Kule kote utakakowasilisha ujumbe wa mageuzi, nakuomba ushike bendera ya Uganda”, Bobi Wine, mgombea wa urais kwenye tiketi ya upinzani.

Mwitikio wa wananchi umeonekana kila mahali—kuanzia magari na pikipiki, milingoti ya umeme, hadi kwenye mapaa ya majengo. Hali hii ni tofauti kabisa na ilivyokuwa awali, ambapo bendera zilionekana zaidi kwenye majengo ya serikali na taasisi za elimu pekee.

Kwa muda mrefu, wengi waliamini kuwa haikuwa sahihi kwa raia wa kawaida kumiliki aukuonyesha benderaya taifa nyumbani au katika biashara zao.

Sasa, kama wanavyosema baadhi ya wananchi, huu ni mwamko mpya wa kuthamini bendera ya taifa kama ishara ya utaifa, uzalendo na msimamo wa kisiasa.

“Tunataka moyo huo wa kutaka nchi bora ukumbatiwe na kila raia kwa kushika bendera. Huvunji sheria yoyote kwa kuwa nayo”, alisema raia mmoja wa Kampala.

“Bendera ni nembo yetu sote Uganda. Nilishtuka sana kuona mtu aliyekuwa akipeperusha bendera kwenye pikipiki yake akipigwa na kupokonywa bendera na mwanajeshi”, alisikitishwa piahuyu mkaazi wa jiji kuu ya Uganda.

“Hakuna sababu ya kumpiga anapeperusha bendera ya taifa”

Yoweri Museveni Rais wa Uganda
Rais wa Uganda, Yoweri MuseveniPicha: Algerian Presidency/AA/picture alliance

Hata hivyo, onyo lililotolewa na mkuu wa majeshi, Muhoozi Kainerugaba, kuhusu kile alichokitaja kuwa matumizi mabaya ya bendera ya taifa, pamoja na visa vilivyosambaa mitandaoni vikionyesha wanajeshi na polisi wakiwakamata raia na kuwapokonya bendera, vimezidisha mjadala kuhusu haki za kiraia. Baadhi ya wananchi sasa wana mashaka kuhusu uhalali wa kushika au kupeperusha bendera ya taifa hadharani.

Kwa upande wake, mwanahistoria John Sempebwa anafafanua umuhimu wa bendera ya taifa kama alama ya hadhi, uhuru na uzalendo wa wananchi.

“Chama cha NUP chaweza kutumia bendera hiyo kuhamasisha watu kushiriki uchaguzi. Hakuna sababu ya kumpiga ambaye anapeperusha bendera ya taifa”, alisema Sempebwa.

Kutokana na umaarufu mkubwa wa bendera katika kipindi hiki cha kampeni, biashara ya bendera imekua kwa kasi. Bei za bendera za aina mbalimbali zimepanda kwa zaidi ya asilimia mia tatu, lakini bado mahitaji yanaendelea kuongezeka, hasa miongoni mwa wananchi wanaohudhuria mikutano ya kampeni.

Kwa ujumla, kote duniani, bendera ya taifa ni kitambulisho muhimu cha utaifa, siasa na uzalendo, na huheshimiwa kwa kiwango cha juu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *