China ilisema inafanya mazoezi hayo ya kijeshi ikilenga maeneo ya Bandari, Kaskazini na Kusini Magharibi mwa Taiwan, katika zoezi linalojumuisha meli za kivita, wapiganaji, makombora na madroni. Msemaji wa jeshi la China amearifu kwamba Beijing itatumia pia jeshi la wanamaji, Jeshi la angani na maroketi kwa luteka hiyo kubwa kabisa ya kijeshi inayoitwa “Justice Mission 2025”
Mazoezi hayo yanalenga kuonesha utayari wa kukabiliana kupitia majini, kukizingira kisiwa hicho hasa katika bandari na maeneo yake muhimu.
China pia ilitoa ramani ya maeneo matano makubwa karibu na Taiwan ambako inapanga kufanya mazoezi hayo ya kijeshi kuanzia saa mbili asubuhi, hadi saa kumi na mbili jioni kesho Jumanne. Jeshi limeonya pia kwamba kwa sababu ya usalama, hakuna meli yoyote inayotakiwa kupita katika mlango wa bahari wa Taiwan.
Beijing inadai Taiwan kuwa sehemu ya eneo lake na imekataa kuondoa uwezekano kwamba itatumia hatua za kijeshi kukidhibiti kikamilifu kisiwa hicho. Hatua ya hivi karibuni iliyokosolewa na China nichina Taiwan Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Taiwan, kuiuzia kiwango kikubwa cha silaha.
China: Hatua za kuizuwia China kuungana na Taiwan hazitofanikiwa
Kitendo hicho kiliifanya China kufoka vikali, ikitoa onyo kwamba nchi za nje zinazoipa Taipei Silaha zitachochea eneo hilo kuingia katika vita vikubwa. China haikutaja nchi yoyote katika taarifa yake hiyo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian amesema hatua zozote za kuizuwia China kuungana na Taiwan hazitofanikiwa.
“Vitendo vyovyote vya kichokozi vinavyovuka mstari mwekundu na vinavyochochea suala la Taiwan vitajibiwa vikali kutoka China na mipango yoyote mibaya ya kuzuia kuungana tena kwa China na Taiwan itashindwa.”
Taiwan yakosoa luteka ya China
Taiwan imekosoa hatua hiyo ya China iliyoiita ya kichokozi. Wizara ya ulinzi ya kisiwa hicho imesema maeneo ambayo China imeamua kufanyia mazoezi yake ya kijeshi yanajumuisha pia njia za kimataifa ikisema hilo linaweza kuathiri safari za ndege zinazoingia na kuondoka kutoka maeneo ya karibu ya Taiwan.
Taiwan imeongeza kuwa tayari imeshuhudia ndege 89 za kijeshi za China, meli za kivita 28 pamoja na vyombo vya ulinzi vya pwani karibu na kisiwa hicho hii leo asubuhi. Wizara ya ulinzi imesema hii ni idadi kubwa ya ndege za China kuonekana kwa siku moja karibu na kisiwa hicho tangu Oktoba 15 mwaka 2024.