
Msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-FARDC, Meja Jenerali Sylvain Ekenge amesimamishwa kazi, kufuatia matamshi tata aliyotoa, yanayoashiria ubaguzi dhidi ya wanawake wa Kitutsi nchini humo, wakati wa mahojiano kwenye Televisheni ya taifa.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kusimamishwa kazi kwa Sylvain Ekenge kunakuja saa chache tu baada ya matamshi yake ambapo alitoa wito wa kuwa macho dhidi ya wanawake wa Watutsi.
Msemaji wa jeshi la DRC Meja Jenerali Sylvain Ekenge, amesimamishwa kazi na Mkuu wa Majeshi ya DRC kwa kutoa matamshi yanayoonekana kuwa ya kibaguzi dhidi ya jamii ya Watutsi wa nchi hiyo wikendi iliyopita kwenye televisheni ya taifa.
Video ya matamshi yake ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuchochea hisia mseto kwenye jamii na pia katika nyanja ya kisiasa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, ambaye alionyesha kukerwa na matamshi yaliyotolewa na msemaji wa jeshi la Kongo, Jenerali Ekenge, akilenga jamii ya Watutsi, amesema kuwa: “Matamshi yote ya chuki lazima yakataliwe kwa hali yote” akiongeza kuwa “Maelewano ya kitaifa yanaweza kujengwa tu juu ya roho ya ujumuishaji kwa jamii zote.”
Hata hivyo, tangu aingie madarakani Raïs wa DRC, Félix Tshisekedi, amekuwa akipambana dhidi ya aina zote za ubaguzi dhidi ya watu wa jamii hii la Wakongo nchini DRC na dhidi ya jamii zote 450 zinazounda DRC.
Mkuu wa jeshi ametoa wito kwa watu wote kuungana, kusimama pamoja na kukataa matamshi yote ya chuki, ili kuiunga mkono FARDC katika kutekeleza dhamira yao.
Freddy Tendilonge/Kinshasa/RFI Kiswahili.