
Utafiti uliofanywa na kampuni ya Infotrak unaonyesha kuwa, endapo uchaguzi wa urais wa Kenya ungefanyika hivi leo, Rais William Ruto angeibuka mshindi; hata hivyo uchaguzi huo ungelazimu kuingia katika duru ya pili kwa sababu ushindi wake usingevuka kiwango cha asilimia 50+1 ya kura kinachohitajika.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliopewa anuani ya ‘End-Year Poll Politics’, Rais Ruto anaongoza kwa umaarufu kwa asilimia 28 akifuatiwa na aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i (asilimia 13) naye Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ataibuka wa tatu kwa asilimia 12.
Hata hivyo, kwa vile kutawazwa mshindi anayetokana na kura za urais nchini Kenya kunashurutisha mgombea kupata angalau asilimia 50+1 ya kura halali zilizopigwa, kulingana na utabiri wa uchunguzi huo wa maoni, uchaguzi huo ungelazimu kuingia katika duru ya pili.
Ruto ameonekana kupanda chati ya umaarufu hususan baada ya kuridhia kufanya kazi na aliyekuwa Waziri Mkuu na Kiongozi wa ODM hayati Raila Odinga, hali iliyosaidia kudhibiti serikali yake iliyokuwa inakumbwa na msukosuko uliochangiwa na maandamano ya Gen Z yaliyofanyika 2024.
Umaarufu wa kiongozi huyo ambaye imekuwa ikidaiwa kwamba huenda akawa rais wa muhula mmoja, vile vile unaonekana kuongezeka zaidi katika siku za karibuni kufuatia ushindi mkubwa wa chama chake kwenye uchaguzi mdogo wa Novemba ambapo wagombea wa Serikali Jumuishi kwenye ngazi za useneta na ubunge wote walishinda viti walivyowania; jambo lililotoa pigo kali kwa mrengo wa upinzani unaojumuisha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka na Fred Matiang’i…/