
KOCHA Msaidizi wa Fufuni, Sueliman Abbas na Sheha Khamis Rashid wa Muembe Makumbi City, kila mmoja kwa waakati wake ameitaja presha ndiyo iliyoamua matokeo ya mechi baina yao.
Timu hizo zimekutana leo Desemba 29, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja katika mwendelezo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, Fufuni ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 56, kupitia Mboni Steven Kibamba aliyeachia shuti kali nje ya boksi ambapo kipa wa Muembe Makumbi City, Hamza Mohamed alishindwa la kufanya, akishtukia nyavu zinatikisika.
Bao hilo halikudumu sana kwani krosi ya chinichini iliyopigwa na Ali Khamis Faki dakika ya 63, ilimkuta Abdallah Idd Pina akiwa ndani ya boksi, kwa utulivu mkubwa akachagua upande wa kushoto mwa kipa wa Fufuni, Idrissa Mohamed Mgunya na kuisawazishia Muembe Makumbi.
Baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, Sheha amesema: “Timu mbili zimekutana zote zikiwa ngeni katika mashindano haya, kumbuka Fufuni walitufunga kwenye ligi, kwahiyo wachezaji walikuwa na wasiwasi wasije kupoteza tena na wapinzani wakawa wana wasiwasi wasije kuruhusu kulipizwa kisasi ndio ikapelekea hali kuwa hivyo.
“Lakini pointi moja tuliyoipata tunaenda nayo mazoezini kujiandaa na mechi ijayo dhidi ya Simba. Kuna makosa ya kiuchezaji nimeyaona, tutayarekebisha kwenye uwanja wa mazoezi ingawa tuna siku chache za kufanya hivyo kabla ya kucheza na Simba.”
Naye Kocha Suleiman, amesema: “Presha ya kutopata bao kipindi cha kwanza licha ya kutawala mchezo ilifanya wachezaji wangu kuwa na hamu sana ya kufunga kipindi cha pili. Viungo na washambuliaji walitengeneza nafasi lakini wakashindwa kuweka mpira golini japo baadae tukafanikiwa kuongoza, wapinzani wakasawazisha.
“Tumeliona hilo na tutarirekebisha kwani mechi ijayo dhidi ya Simba tunahitaji kufanya vizuri ili kusonga hatua inayofuata.”
Baada ya leo, Januari 3, 2026 Muembe Makumbi City itacheza dhidi ya Simba, kisha Januari 5, 2026 ni Fufuni dhidi ya Simba ambapo yenye pointi nyingi kati ya timu hizo tatu za kundi B, itafuzu nusu fainali.