Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran ametangaza kwamba mawimbi ya kwanza ya satelaiti zote tatu zilizobuniwa na kutengenezwa ndani ya Iran zinazoitwa “Zafar 2”, “Paya” na “Kowsar” zilizotumwa angani Jumapili jioni Disemba 28, 2025 yamepokewa kwa mafanikio ardhini akisisitiza kuwa, hii inathibitisha uzima wa kiufundi na utendajikazi mzuri wa satelaiti hizo za Iran baada ya kuingia kwenye obiti.

Profesa Sayyid Sattar Hashemi amegusia pia mchakato wa kupatikana mawasiliano ya awali kutoka kwenye satelaiti hizo tatu za Iran na amesema: Mawimbi ya kwanza ya satelaiti tatu za “Zafar 2”, “Paya” na “Kowsar” yamepokewa katika Kituo cha Kudhibiti Mwendo wa Satelaiti cha Mahdasht, Kituo cha Qeshm na pia Kituo cha Sairan. Kupokewa mawimbi hayo kwa wakati mmoja kwenye vituo kadhaa ni ushahidi wa uthabiti na utendajikazi sahihi wa mifumo ya mawasiliano wa satelaiti hizo.

Ameongeza kuwa, kupokewa mawimbi ni hatua ya kwanza muhimu baada ya kurushwa satelaiti anga za mbali na kusema: “Mafanikio katika hatua hiyo hutoa msingi muhimu wa ufuatiliaji wa kuendelea wa kiufundi, utulivu katika obiti na ni mwanzo wa hatua zinazofuatia za kazi zilizopangiwa kufanya satelaiti husika.”

Jana Jumapili, Disemba 28, 2025, Iran ilirusha hadi kwenye obiti, satelaiti tatu zilizobuniwa na kutengenezwa ndani ya Iran. Hii ni mara ya kwanza kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kurusha satelaiti nyingi angani kwa wakati mmoja. Iran hivi sasa ni sehemu ya klabu ya takriban nchi 10 duniani ambazo zina uwezo wa kubuni, kutengeneza na kurusha satelaiti anga za mbali.

Hata hivyo, mara hii Iran imetumia kituo cha kurushia satelaiti cha Vostoch-ny Cosmod-rome cha Russia kurusha satelaiti zake hizo ambazo ni za teknolojia ya kisasa zaidi. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *