Msipandishe bei vifaa vya shuleMsipandishe bei vifaa vya shule

WAKATI Watanzania wakiendelea kuungana na watu wengine duniani kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka, maandalizi ya wanafunzi kurejea shuleni nayo yamepamba moto.

Hapa nchini shule zinafunguliwa Januari 13 mwakani kuruhusu muhula mwingine wa masomo kuendelea huku wanafunzi waliosajiliwa kuanza elimu ya awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza wakiwa na shauku kubwa ya kuanza masomo yao.

Katika mchakato huo, wazazi na walezi ndio wenye kazi kubwa ya kuhakikisha vifaa vya shule kwa watoto wao zikiwemo sare, madaftari, kalamu, mabegi, soksi, viatu na mahitaji mengine kwa wale wa bweni vinapatikana kuwawezesha wanafunzi kuanza masomo yao kwa amani na furaha.

Kutokana na haya, wafanyabiashara wasio na utu hutumia fursa hii kupandisha bei vifaa vya shule kwa kuwa wanajua ni lazima wazazi wanunue ili watoto wao wasishindwe kwenda shule.

Hivi karibuni kuelekea kuanza kwa muhula huo mpya wa masomo wa mwaka 2026, viongozi wa wafanyabiashara wadogo ‘machinga’ walitoa onyo kwa wafanyabiashara kutopandisha bei za vifaa vya shule ili kuondoa visingizio kwa wazazi kushindwa kuwapeleka watoto shule.

Rai hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamachinga Tanzania, Stephen Lusinde alipozungumza na HabariLEO na kusisitiza ni haki kwa kila mtoto kupata elimu bila kuangalia kipato cha mzazi wake, hivyo shule zikifunguliwa wanatakiwa kupewa mahitaji yote ya shule ili waweze kuanza masomo.

Kwanza tunaupongeza uongozi wa wamachinga kwa kutoa kauli hii kuonesha inajali elimu ya watoto wa Kitanzania. Kwa sababu hiyo, tunawakumbusha wafanyabiashara wa vifaa vya shule wadogo, wa kati na wakubwa kuzingatia utu na uzalendo katika biashara zao. Kupandisha bei vifaa vya shule ni kurudisha nyuma juhudi za serikali kujenga miundombinu bora ya shule ili watoto wengi wapate elimu wanayostahili.

Tunaungana na uongozi wa wamachinga kuwasisitiza wafanyabiashara wa vifaa vya shule kuviuza kwa bei za kawaida hata kama mahitaji ni mengi ili kumwezesha kila mtoto anayepaswa kwenda shule aende bila kikwazo cha kukosa mahitaji muhimu.

Tunaamini wakifanya hivyo nchi nzima na kuweka pembeni tamaa ya kupata fedha nyingi isivyo halali, watakuwa wamechangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa elimu kwa kizazi cha sasa na kijacho. SOMA: SMZ kuongeza bajeti ya elimu tril 1/-

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *