Takriban watu 13 wamefariki na karibu 100 wamejeruhiwa baada ya treni kuacha njia katika eneo la kusini-magharibi mwa Mexico la Oaxaca, limesema jeshi la wanamaji la Mexico.
Treni hiyo, iliyokuwa ikisafiri kati ya Ghuba ya Mexico na Bahari ya Pasifiki, imebeba abiria 241 na wafanyakazi tisa.
Jumla ya watu 98 wamejeruhiwa, ambapo 36 wanatibiwa hospitalini, imesema taarifa ya jeshi.
Treni iliacha njia yake ya reli ilipozunguka kona karibu na mji wa Nizanda.
Mwanasheria Mkuu wa Mexico amethibitisha kuwa uchunguzi unaendelea.
Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum amesema watano kati ya waliojeruhiwa walikuwa katika hali mbaya.
Picha kutoka eneo la ajali zinaonyesha wafanyakazi wa uokoaji wakiwasaidia abiria kushuka kwenye treni.
Jeshi la wanamaji la Mexico ndilo linaloendesha safari za treni iliyokumbwa na ajali.