Viongozi hao wawili walizungumza kwenye kikao cha pamoja cha waandishi habari baada ya kukutana kwenye makazi ya Trump ya Mar-a-Lago jimboni Florida Jumapili mchana.

Viongozi wote wawili waliripoti kuwepo kwa maendeleo katika masuala mawili yenye utata zaidi kwenye mazungumzo ya amani – uhakikisho wa usalama wa Ukraine na kugawanywa kwa eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine ambalo Urusi inataka kulifanya kuwa sehemu ya himaya yake.

Trump na Zelenskiy walitoa maelezo machache na hawakutangaza tarehe ya mwisho ya kukamilisha makubaliano ya amani, ingawa Trump alisema itakuwa wazi “katika wiki chache zijazo” kama mazungumzo ya kukomesha vita yatafanikiwa. Alisema “masuala machache yenye utata” kuhusu ardhi lazima yatatuliwe. “Naam, nadhani, ardhi unayoizungumzia, baadhi ya ardhi hiyo imechukuliwa. Baadhi ya ardhi hiyo labda inakaribia kunyakuliwa, lakini inaweza kuchukuliwa katika kipindi kijacho cha miezi kadhaa. Je, ni bora kufikia makubaliano sasa? Wamekuwa jasiri sana. Walipigana vikali sana na wanaendelea kupigana vikali sana na kusababisha uharibifu mkubwa.” Alisema Putin.

Rais Donald Trump akizungumza na Zelensky kwenye makazi yake ya Mar-a-Lago
Trump amekiri mazungumzo hayo ni magumu na bado yanaweza kuvunjika, na kuacha vita hivyo vikiendelea kwa miaka mingiPicha: Joe Raedle/AFP/Getty Images

Zelenskiy alisema makubaliano kuhusu uhakikisho wa usalama wa Ukraine yamefikiwa. “Na tulijadili vipengele vyote vya mpango wa amani, ambavyo vinajumuisha – na tuna mafanikio makubwa – mpango wa amani wa ajenda 20: tumekubaliana kwa asilimia 90, na dhamana za usalama kati ya Marekani na Ukraine: tumekubaliana kwa asilimia 100, dhamana za usalama kati ya Marekani na Ulaya na Ukraine: tunakaribia kukubaliana, mwelekeo wa kijeshi: tumekubaliana kwa asilimia 100, mpango wa ustawi unakamilika.” Alisema Zelensky.

Trump alichukua tahadhari zaidi, akisema kwamba wamefikia asilimia 95 ya suala hilo, na kwamba anatarajia nchi za Ulaya “kuchukua sehemu kubwa” ya juhudi hizo kwa msaada wa Marekani.

Trump na Zelensky walisema mustakabali wa eneo la Donbas haujatatuliwa, ijapokuwa rais huyo wa Marekani alisema mazungumzo yako kwenye mkondo sahihi. Marekani inapendekeza liwe eneo huru la kiuchumi ikiwa Ukraine itajiondoa huko, ingawa bado haijulikani jinsi eneo hilo litakavyofanya kazi kivitendo.

Wala viongozi hao hawakutoa maelezo zaidi kuhusu aina ya makubaliano waliyofikia kuhusu kuihakikishia Ukraine usalama baada ya vita kumalizika, kitu ambacho Zelensky alieleza jana kuwa ni hatua muhimu katika kufikia amani ya kudumu.

Trump na Putin wazungumza kabla ya mkutano na Zelensky

Rais wa Urusi Vladmiri Putin (kushoto) na mshauri wake wa sera za kigeni Yuri Ushakov
Kabla ya kukutana na Rais Zelensky wa Ukraine, Trump alifanya mazungumzo ya simu na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Kristina Kormilitsyna/Sputnik/REUTERS

Muda mfupi kabla ya Zelensky na ujumbe wake kuwasili kwenye makazi ya Trump ya Florida, Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin walizungumza kwenye simu. Trump alisema yalikuwa mazungumzo yenye tija huku mshauri wa sera ya kigeni wa Kremlin Yuri Ushakov akiiyaita ya kirafiki.

Ushakov alisema Putin alimwambia Trump usitishaji mapigano kwa siku 60 uliopendekezwa na Umoja wa Ulaya na Ukraine utarefusha vita. Mshauri huyo wa Kremlin aidha alisema Ukraine inahitaji kufanya uamuzi kuhusu Donbas bila kuchelewa.

Siku moja kabla ya Zelensky kuwasili Florida kukutana na Trump, vikosi vya Urusi viliishambulia Kyiv na maeneo mengine ya Ukraine kwa mamia ya makombora na droni. Mashambulizi hayo yalikata umeme na mifumo ya kupasha joto majumbani katika maeneo ya mji mkuu wa Ukraine. Putin alisema Moscow itaendeleza vita vyake ikiwa Kyiv haitatafuta amani ya haraka.

Wakuu wa nchi za Ulaya walishiriki kwa sehemu kwenye mkutano wa Trump na Zelensky kwa njia ya simu. Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen alisema “Ulaya iko tayari kuendelea” kufanya kazi na Ukraine na washirika wake Marekani,” na akaongeza kuwa kuwa na dhamana za usalama zenye nguvu zitakuwa na umuhimu mkubwa.

Vyanzo: Mashirika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *