Hujambo mpenzi mskilizaji na hususan mfuatiliaji wa matukio ya spoti na karibu katika kipindi chetu cha mwisho mwaka huu 2025, tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyoshuhudiwa ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia ikiwemo michuano ya AFCON inayoendelea kurindima nchini Morocco.
Ligi ya Mabingwa wa Asia
Klabu ya soka ya Esteghlal ya Iran imefanikiwa kutinga hatua ya 16 Bora baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Al Muharraq ya Bahrain katika mchezo wao wa mwisho wa Kundi A, wa Ligi ya Mabingwa ya Asia ya AFC 2025/26 Jumatano. Mabao kutoka kwa Esmaeil Gholizadeh, Duckens Nazon na Jasir Asani yaliifanya timu hiyo ya Iran kufikisha pointi nane katika Uwanja wa Sheikh Ali Bin Mohammed Aal Khalifa, alama sita nyuma ya Al Wasl ya Umoja wa Falme za Kiarabu walioko kileleni mwa kundi hilo.

Ushindi huo umeipelekea klabu hiyo iingie kibabe kwenye hatua ya mtoano ya ligi hiyo ya kikanda. Kabla ya hapo, klabu nyingine ya mpira wa miguu ya Iran ya Teractor ilisonga mbele pia kwenye Ligi ya Mabingwa ya AFC baada ya kupambana kijeshi na kuishinda Al Duhail ya Qatar kwa mabao 2-1 Jumatatu iliyopita. Ushindi huo unamaanisha kwamba ikiwa na pointi 14, kikosi cha Dragan Skocic kimehakikishiwa kumaliza katika nafasi nane bora huku Al Duhail ya Djamel Belmadi ikiwa ingali inakabiliwa na kibarua kizito ikiwa wanataka kusonga mbele.
Mieleka: Muirani Bingwa wa Dunia
Muungano wa Mieleka Duniani (UWW) umemtaja Rahman Amouzad kutoka Iran kuwa mwanamieleka wa mtindo wa freestyle (kujiachia) “Aliyeng’ara Zaidi” kwa mwaka huu 2025. “Amouzad aling’ara msimu huu, baada ya kushinda taji kwenye Mashindano ya Dunia, Michezo ya Mshikamano wa Kiislamu na Mashindano ya Muhamet Malo Ranking Series, na kumaliza msimu kama mwanamieleka aliyeorodheshwa nambari 1 duniani. UWW imetangaza kwenye taarifa yake kuwa, Muirani huyo alijinyakulia pointi 58,000 kwenye uorodheshaji wa kimataifa wa Ranking Series, huku akichota “rekodi isiyo na dosari ya alama 14-0” kwa mwaka huu 2025. Shirikisho hilo la mieleka duniani limeeleza kuwa, ushindi mara tano kati ya mapambano yake yote mwaka huu ulikuwa dhidi ya “wapinzani wa ngazi ya juu” wanaoshikilia medali za dunia au Olimpiki, wakiwemo Real Woods kutoka Marekani, Umidjon Jalalov kutoka Uzbekistan, Taiyrbek Zhumashbek Uulu, raia wa Kyrgyzstan, na Mjapani Kotaro Kiyooka.

UWW imesema, “kivutio hicho kikuu cha msimu kwa Amouzad” kilikuja katika Mashindano ya Dunia ya Mieleka ya 2025 huko Zagreb. Amouzad, “ana umri wa miaka 23 pekee na bado anaendelea kuwa bora zaidi.” Kabla ya hapo, Saeed Esmaeili wa Iran alitawazwa kuwa mwanamieleka “Aliyetamalaki Zaidi” wa mwaka huu 2025, katika mieleka mtindo wa Greco-Roman. Timu ya taifa ya mieleka ya kujiachia (freestyle) ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara kadhaa imetwaa ubingwa wa mashindano ya dunia ya mchezo huo. Aidha timu dada ya mieleka ya Greco-Roman ya Iran imekuwa ikifanya vizuri pia na kuipaisha Jamhuri ya Kiislamu katika mapambano ya kibara na kimataifa.
AFCON yaendelea kurindima Morocco
Duru ya 35 ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON imeendelea kurindima nchini Morocco, ambapo wawakilishi wawili wa Afrika Mashariki kwenye mashindano hayo ya kibara walishuka dimbani wikendi hii katika mchuano wa kufa kupona. Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Uganda katika ngoma hiyo ya majirani wa Afrika Mashariki. Tanzania ilipata bao lake dakika ya 59 kupitia mkwaju wa penalti uliopachikwa wavuni na Simon Msuva, huku Uganda ikisawazisha kunako dakika ya 80 kupitia Denis Omedi. Timu ya Taifa ya Nigeria imefanikiwa tayari imetinga hatua ya 16 Bora ya michuano ya AFCON baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Tunisia katika mchezo wa wikendi nchini Morocco. Nigeria, iliyoko Kundi C, ilipata mabao yake kupitia kwa Ademola Lookman aliyefunga dakika ya 44 na 50, kabla ya Victor Osimhen kuongeza bao la tatu dakika ya 67.

Kwa upande wa Tunisia, mabao yao yalifungwa na Hannibal Mejbri dakika ya 64, huku bao la pili likifungwa na Ali Abdi dakika ya 87 kupitia mkwaju wa penalti. Hapo awali, Ademola Lookman alicheka na nyavu mara 2 wakati Nigeria ilipopata ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo dhidi ya Tanzania huko Fez, Morocco, katika mechi yao ya ufunguzi ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Baada ya matokeo hayo, Nigeria inaongoza Kundi C kwa pointi 6, ikifuatiwa na Tunisia yenye pointi 3, wakati Tanzania na Uganda kila moja ikiwa na pointi 1.
Michezo ya mwisho ya kundi hilo itachezwa Januari 6, 2026 ambapo Tanzania itavaana na Tunisia, huku Uganda ikipimana nguvu na Nigeria. Mbali na hayo, mshambuliaji nyota wa Misri, Mohamed Salah alifunga bao la pekee kwenye mechi iliyopeleka Mafarao kuvunja rekodi ya kuwashinda Afrika Kusini katika Kundi B la Kombe la Mataifa ya Afrika na kuingia katika hatua ya mtoano. Mechi hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa Adrar huko Agadir, Morocco, ilimshuhudia Salah akifunga bao hilo kupitia mkwaju wa penalti na kuifanya Misri kuwa timu ya kwanza ya mashindano hayo kusonga mbele. Misri iliichabanga Zimbabwe mabao 2-1 katika mechi yao ya ufunguzi wa mashindano hayo. Afrika Kusini pia ilirekodi ushindi wa mabao 2-1 katika mechi yao ya kwanza walipovaana na Angola. Wenyeji wa michuano ya AFCON 2025, Morocco walitoshana nguvu na Mali kwa kutoa sare ya kufungana bao 1-1 katika dimba la Prince Moulay Abdullah wenye uwezo wa kubeba mashabiki 69,500. Morocco inaongoza Kundi A kwa pointi 4, na magoli mawili ya ziada, ikifuatwa na Mali wenye alama 2, sawa na Zambia, huku Wangazija wakivuta mkia kundini kwa alama 1. Bao la kusawazisha la Sadio Mane liliwapa mabingwa wa mwaka 2022 Senegal sare ya bao 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika pambano lao la Jumamosi. Timu zote mbili zina pointi nne, lakini Senegal wana tofauti kubwa ya mabao kabla ya mechi yao ya mwisho ya makundi dhidi ya Benin Jumanne. Benin wana pointi tatu baada ya ushindi wa 1-0 Jumamosi iliyopita mjini Rabat dhidi ya Botswana, ambao wanavuta mkia bila pointi wala bao. Cedric Bakambu alikuwa amewapa Leopards uongozi muda mfupi baada ya saa moja mjini Tangier, lakini mshambuliaji wa Al-Nassr Mane alijibu mara baada ya hapo, na matokeo hayo yanahakikisha Senegal inabaki kileleni mwa Kundi D huku kukiwa na raundi moja ya mechi zilizosalia. Wakati huo huo, nahodha Riyad Mahrez alifunga katika kila kipindi huku mabingwa wa 2019 Algeria wakipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sudan iliokuwa na wachezaji 10 katika mchezo wao wa ufunguzi katika Uwanja wa Moulay El Hassan huko Rabat. Winga huyo wa zamani wa Manchester City, ambaye sasa anachezea Al-Ahli ya Saudi Arabia, alifunga bao lake la pili na la timu yake muda mfupi baada ya saa moja, na Ibrahim Maza akakamilisha ushindi mwishoni mwa mchezo huku Algeria ikianza kwa njia bora zaidi katika Kundi E. Huku hayo yakiarifiwa, mabao mawili katika dakika za lala salama yaliifanya Burkina Faso kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Equatorial Guinea waliokuwa na wachezaji 10 katika mechi ya ufunguzi ya Kundi E mapema siku hiyo.

Mchezo wa Mozambique na Gabon Jumapili hii ulimalizika kwa vijana wa Kisumbiji kuvuna ushindi wa mbinde wa magoli 3-2. Aidha Kodivaa na Cameroon walitoshana nguvu Jumapili kwa kutoa sare ya bao 1-1. Michuano hiyo ya AFCON inaendelea kuroroma katika viwanja mbali mbali nchini Morocco. Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika CAF, bingwa wa duru hii ya 35 AFCON 2025 atajinyakulia kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 7 huku mshindi wa pili akipokea Dola Milioni 4. Timu zitakazofanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali zitapokea Dola Milioni 2.5 kila moja, huku zile zitakazotinga robo fainali zikipata Dola Milioni 1.3 kila timu.
Dondoo za Hapa na Pale
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupitia Kamati ya Nidhamu, imeishushia rungu zito klabu ya AS FAR Rabat ya Morocco, uamuzi ambao utawabeba mabingwa wa soka nchini Tanzania, Yanga katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Waarabu hao. AS Far Rabat imeshushiwa adhabu kali na CAF kufuatia vurugu za mashabiki wa timu hiyo katika mechi ya nyumbani dhidi ya Al Ahly ya Misri iliyopigwa Novemba 28, 2025, mchezo ulioishia kwa sare ya bao 1-1. Al Ahly ndio iliyolalamikia vurugu hizo za mashabiki wa AS FAR Rabat. Waarabu hao wa Morocco kwa adhabu hiyo watalazimika kucheza mechi zao mbili za nyumbani bila mashabiki watakapokutana na JS Kabylie ya Algeria mnamo Januari 30, 2026 kisha ule wa Yanga utakaochezwa Februari 6, 2026. Maamuzi hayo endapo yatasimama, yataibeba Yanga katika mechi ya marudiano dhidi ya AS FAR Rabat ikikumbukwa wababe hao wa Tanzania waliwachapa Waarabu hao kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza makundi, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, Novemba 22,2025.
Kwenye masumbwi, bondia Hassan Mwakinyo wa Tanzania ameibuka mshindi kwa gumi zito la Knock Out (K.O), dhidi ya mpinzani wake Stanley Eribo kutoka Nigeria, baada ya kumaliza pambano katika raundi mbili. Pambano hilo lilifanyika usiku wa Ijumaa katika ukumbi wa Warehouse Masaki, jijini Dar es Salaam. Akizungumzia pambano hilo, Mwakinyo amesema imekuwa rahisi kwake kumshinda mpinzani wake kutokana na mazoezi anayofanya bila kujali ana mchezo au hana. Katika pambano jingine Mtanzania Hamadi Furahisha aliibuka mshindi kwa pointi dhidi ya Mmalawi Hanock Phiri katika pambano la raundi 10.
Na kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, Manchester City walivuna ushindi laini wa mabao 2-1 wikendi hii, huku Arsenal wakizidi kutuama kileleni kwa ushindi mwembamba pia wa mabao 2-1 dhidi ya Brighton Albion, na kubaki kama vinara wa EPL Jumamosi. City ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Nottingham Forest, huku Rayan Cherki akifunga bao na kutoa pasi ya bao na kufanikiwa kupanda hadi kileleni kwa muda mfupi.

Klabu hiyo ya London inayotiwa makali na Mikel Arteta ina pointi 42 kutokana na michezo 18, huku City ikiwa na pointi 40. Mbali na hayo, Florian Wirtz alifunga bao lake la kwanza la Liverpool walipowashinda Wolverhampton Wanderers mabao 2-1 huko Anfield. Aston Villa inayozidi kujiimarisha ikifunga orodha ya tatu bora kwa sasa wakiwa na alama 39, iliichabanga Chelsea mabao 2-1, siku chache baada ya kutoa dozi kama hiyo kwa Manchester United.
……………….TAMATI……………