Dar es Salaam. Asilimia kubwa ya wananchi waliolipwa fidia ya makaburi ya Bongololo yaliyopo Mtaa wa Shimo la Udongo, Kata ya Kurasini, kwa ajili ya kupisha ujenzi wa bandari kavu, wamekacha kwenda kuzika.

Kazi hiyo ya uhamishaji imeanza leo Jumatatu, Desemba 29, 2025, baada ya kumalizika kwa ulipaji wa  fidia iliyofanyika kwa takribani wiki mbili.

Katika ulipaji fidia huo, kila kaburi mtu alilipwa Sh300,000 kama rambirambi huku gharama za kuyahamisha, ikiwemo majeneza, sanda na watu wanaofukua, zikigharamiwa na mwekezaji.

Kazi hiyo itaendelea kwa siku nane, ambapo makaburi zaidi ya 2,800 yameutambuliwa, huku mabaki ya miili yakihamishiwa katika makaburi ya Halmashauri ya Sako yaliyopo Mbagala jijini humo.

Akizungumza na Mwananchi, Mwakilishi wa mwekezaji wa bandari hiyo, Mohammed Kamilagasa, amesema katika kazi ya leo ya kuanza kuhamisha waliwapigia simu watu 500, lakini waliojitokeza kwenda kushiriki ni watu 12 pekee.

“Hii inasikitisha sana kwa kuwa ibada ya kuzika ilikuwa ni muhimu kuliko tukio la kuchukua hela, lakini ndivyo ilivyo,” amesema Kamilagasa.

Pamoja na hayo, amesema haiwazuii kuendelea kuyahamisha na kueleza kuwa katika kazi hiyo kwa leo tu wamefukua makaburi 50, huku kwa wale ambao hawatafanikiwa kushiriki, watakapotaka kuyaona wametengeneza vibao vyenye majina kwa ajili ya kuyatambua huko yalipohamishiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Shimo la Udongo, Stanley Lima, amesema licha ya kufikia hatua hiyo bado kuna watu wengine wanaendelea kujitokeza kuonyesha makaburi, huku akionya uwapo matapeli.

Lima amesema katika kuwadhibiti watu hao wameshikilia vitambulisho vyao kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria zaidi.

“Wakati tunaanza shughuli hii tulikamata watu 19 kwa utapeli wa kusema uongo kuwa wana makaburi, na hivyo kaburi moja unakuta lina watu zaidi ya wawili wa uongo, hali ambayo imeendelea hadi leo tunapoanza kuyahamisha,” amesema.

Baadhi ya makaburi yakiwa yameshafukuliwa.

Changamoto nyingine waliyokumbana nayo, amesema, ni baada ya kufukua kutokuta mabaki yoyote na hivyo wengine kulazimika kubeba mchanga kwenda kuzika.

Mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina moja la Salma, amesema sababu ya baadhi ya watu kukacha kushiriki shughuli hiyo ya kuhamisha ni kuogopa kufufua msiba upya, na baadhi leo walionekana wakilia.

Naye Ramadhan Hassan amesema hali hiyo imetokana na baadhi yao kuyatelekeza makaburi hayo kwa muda mrefu, na walichojua kufuata ni fedha iliyokuwa inatolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *