
Mamia ya wanachi wa Somalia jana Jumapili walifanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hyo, Mogadishu kupinga na kulaani uamuzi wa utawala haramu wa Israel wa kuitambua kana nchi huru Somaliland, eneo la kaskazini mwa Somalia ambalo lilijitangazia uhuru wake mwaka 1991.
Waandamanaji walianza maandamano kwa kuimba wimbo wa taifa wa Somalia, na kisha kupiga nara za kulaani hatua hiyo waliotaja kuwa batili ya Israel. Sanjari na kusisitiza juu ya uhuru na mamlaka ya kujitawala Somalia, waandamanaji walipaza sauti wakitamka maneno kama vile “Somalia haigawanyiki” na “Somaliland ni Somalia.”
Vikosi vya usalama vya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika vilitumwa kwa wingi ili kudumisha amani kwenye maandamano hayo. Mohamed Abor, mmoja wa waandamanaji hao aliliambia shirikam la habari la Anadolu kwamba, Somalia haijawahi na katu haitawahi kuachia hata shibri mojaya ardhi yake.
Amesisitiza kwamba, hakuna ardhi ya Somalia ambayo itakabidhiwa Israel au dola lingine lolote. Amesema, “Somalia ni moja na itabaki kuwa moja,” akiongeza kwamba Wasomali wako tayari kufanya chochote kwa ajili ya kuilinda nchi yao. Muandamanaji mwingine, Abdi Ismail, anasema uamuzi wa Israel haukubaliki na kuuita uamuzi huo kuwa “shambulio la wazi dhidi ya uhuru wa Somalia.”
Waandamanaji hao mjini Mogadishu wamesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa haipaswi kukaa kimya mkabala wa uamuzi huo batili wa utawala wa Kizayuni.
Somalia imeitaka Israel kubatilisha hatua hiyo na kuitaja kuwa kitendo cha “uchokozi ambacho kamwe hakitavumiliwa. Ali Omar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia ameiambia televisheni ya al Jazeera kwamba, serikali itafuata njia zote za kidiplomasia ili kupinga kile ilichokitaja kuwa kitendo cha “uchokozi wa kiserikali” na uingiliaji wa utawala wa Israel katika masuala ya ndani ya Somalia.