s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Siku chache zijazo tutauhitimisha mwaka uliokuwa na mambo mengi wa 2025. Ulikuwa na mambo mengi kisiasa na kimichezo. Lakini makala haya yana lengo la kutazama matukio makubwa katika uwanda wa michezo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Nikisema michezo, simaanishi mpira pekee. Ni kuanzia mbio, raga, baiskeli na mpira wenyewe kwenye ngazi ya taifa na klabu, kwa upande wa wanawake na wanaume. Kuna mengi yametokea. Tuyadurusu!

Pia unaweza kusoma

CHAN 2024 Afrika Mashariki

Mashindano ya Chan ya wachezaji wa ndani, kwa ushirikiano na Kenya, Tanzania, na Uganda, kwa mara ya kwanza yaliandaliwa na mataifa matatu, nayo ni kutoka Afrika Mashariki.

Harambee Stars ya Kenya, iliongoza Kundi A na kufikia robo fainali kabla ya kuondolewa na Madagascar waliofika fainali.

Tanzania iliondolewa baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya mabingwa mara mbili Morocco katika mechi ya robo fainali katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika Uwanja wa Kitaifa wa Mandela jijini Kampala, Uganda ilitolewa kwenye robo ya michuano ya CHAN 2024 baada ya kushindwa 1-0 na Senegal.

Ushindi katika mashindano hayo ulienda kwa Morocco, ambayo iliishinda Madagascar katika fainali iliyofanyika katika uwanja wa Kasarani, Nairobi.

Kenya yaendeleza ubabe mbio

s

Chanzo cha picha, @WilliamsRuto/X

Faith Kipyegon na Beatrice Chebet walivunja rekodi 2025. Kipyegon, bingwa mara tano wa Mbio za Diamond, alivunja rekodi ya dunia ya mita 1500 katika mashindano ya Diamond Legue huko Eugene, Marekani kwa muda wa saa 3:48.68 mara ya tatu kufanya hivyo katika misimu mitatu mfululizo.

Chebet pia aligonga vichwa vya habari, akivunja rekodi ya dunia ya mita 5000 huko Eugene na kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kukimbia chini ya dakika 14.

Mashindano ya Riadha Duniani (Tokyo, Japan), yalifanyika Septemba, ambapo Timu ya Kenya ilimaliza ya pili kwa ujumla duniani. Wakimbiaji wa Kenya, walishinda mataji yote kutoka mita 800 hadi marathon.

Timu ya Kenya ilimaliza katika nafasi ya pili ya kihistoria kwenye jedwali la medali kwa medali 11 dhahabu 7, fedha 2, na shaba 2 ikiwa nyuma ya Marekani pekee, ambayo ilishinda medali 12 za dhahabu.

Mashindano ya dunia ya baiskeli Rwanda

dc

Chanzo cha picha, | Netherlands Embassy |

Tukio kubwa zaidi la michezo nchini Rwanda mwaka 2025 yalikuwa ni Mashindano ya 98 Baiskeli ya Dunia ya UCI Road ya 2025 jiji Kigali, mara ya kwanza mashindano hayo kufanyika barani Afrika.

Jumla ya mashindano kumi na tatu ya mbio za baiskeli yalifanyika. Mashindano hayo hufanyika katika mzunguko wa kilomita 15.1 (maili 9.4) kuzunguka Kigali, na kunakuwa na idadi tofauti ya mizunguko kwa matukio tofauti.

Mashindano ya Raga Afrika Uganda

cx

Chanzo cha picha, rugbyafrique

Kombe la Raga Afrika ni mashindano ya kila baada ya miaka miwili ya timu za raga za wanaume yanayoshirikisha mataifa 16 bora ya Afrika kulingana na viwango vyao vya Raga Duniani, yanaandaliwa na Rugby Africa. Mashindano hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2000.

Kombe la Raga Afrika Mashindano kwa mwaka 2025 yalifanyika Kampala Uganda kuanzia Julai 8-19, yakizikutanisha timu za taifa kutoka Afrika.

Zimbabwe iliishinda Namibia 30 –28 na kushinda Raga Afrika jijini Kampala, Uganda. Wamefuzu Kombe la Dunia la Raga kwa mara ya kwanza tangu 1991. Zimbabwe itajiunga na Afrika Kusini kuiwakilisha Afrika katika Kombe la Dunia la Raga la 2027 nchini Australia.

Soka la Tanzania lakua

D

Chanzo cha picha, TFF

Mwaka huu, timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake “Twiga Stars” imefanikiwa kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (WAFCON 2026) yatakayofanyika Morocco mwakani. Hii itakuwa mara ya tatu baada ya 2010 na 2024,

Twiga Starts ilikuwa Morocco katika mashindano ya Wanawake Afrika 2024 (ambayo yalifanyika 2025), wakiwa kundi C ambapo walichuana na Mali, Afrika Kusini na Ghana na kuishia makundi.

Fauka ya hayo, Twiga Stars imepanda kwa nafasi saba katika viwango vya soka duniani kwa wanawake vya Shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa) mwezi Machi 2025, kutoka nafasi ya 145 iliyokuwepo katika chati iliyopita ya Desemba 13, 2024 hadi nafasi ya 138, 2025.

Mwaka huu ilikuwa ndio mara ya kwanza Tanzania kupeleka timu nne kwenye hatua ya Makundi ya Michuano ya CAF ya Klabu Bingwa Afrika, Simba SC na Yanga SC, na Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC na Singida Black Stars. Mashindano hayo bado yanaendelea.

Mafanikio ya Tanzania, yalipigiwa msumari na mshambuliaji wa Young Africans pamoja na timu ya taifa ya Tanzania, Clemence Mzize kwa kuchukua tuzo ya goli bora la mwaka Afrika katika tuzo za CAF zilizotolewa nchini Morocco 2025.

Simbu na Munyua walivyong’ara duniani

k

Chanzo cha picha, Mtandao/TRC

David Munyua, ameingia kwenye vitabu vya historia kwa kuwa Mkenya wa kwanza kutwaa ubingwa wa dunia wa mchezo wa vishale, maarufu kama ‘Darts’. Disemba 18, 2025, Munyua alitoka nyuma kwa seti mbili, na kumshinda Mike de Decker kutoka Ubelgiji kwa seti 3-2.

Mwaka 2025 Mwanariadha Alphonce Felix , ameweka historia kwa ushindi wake wa dhahabu katika mbio za dunia zilizofanyika mjini Tokyo Japan, na kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu ya mashindano makubwa kabisa ya riadha duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *