
Jana Jumatatu, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ilithibitisha kwamba msemaji wa harakati hiyo, Abu Obeida aliuawa shahidi mapema mwaka huu katika shambulio la anga la Israel.
Katika kila wakati Israel ilipofanya mauaji ya kimbari ya dhidi ya Wapalestina huko Ghaza, sauti ya Abu Obeida ilisikika ikiwa na mguso mkubwa usioyumba.
Kuanzia Oktoba 7, 2023 hadi kuuawa kwake shahidi, Abu Obeida, msemaji – aliyekuwa anafunika uso wake kwa kitambaa cha keffiyeh – wa Brigedi za Izz al-Din al-Qassam, Tawi la Kijeshi la HAMAS, alikuwa anajitokea na kutoa taarifa mpya za uwanja wa vita, akidhihaki madai ya uongo ya Israel ya kwamba ni dola lisiloshindwa na akiitangaza kwa walimwengu Ghaza kwamba ni chuo bora zaidi cha kijeshi kwa watu wanaoishi kwenye Muqawama na mapambano ya kukabiliana na adui katili mno.
Tangazo la kuuawa shahidi Abu Obeida lilitolewa jana na msemaji mpya wa HAMAS, ambaye hakutoa maelezo yoyote kuhusu wakati au eneo la kuuawa shahidi kamanda Abu Obeida.
Taarifa hiyo ilifichua pia kwamba jina halisi la Abu Obeida ni Huthaifa Samir al-Kahlout. “Tunatangaza kwa fakhari kuuawa shahihi kiongozi mkuu… Abu Obeida,” alisema msemaji mpya wa HAMAS na kusisitiza kuwa: “Tumerithi cheo chake.”
Utambulisho halisi wa Abu Obeida haukufichuliwa wakati wa uhai wake. Kama mtangulizi wake, Imad Aqel, aliyeuliwa shahidi na Israel mwaka wa 1993, alifunika uso wake na keffiyeh nyekundu na alionekana akiwa amevaa sare za kijeshi pekee. Usiri huo uliongeza nguvu yake ya isiyo na mfano.
Mwezi Juni 2006, Abu Obeida alitangaza kutekwa nyara mwanajeshi wa Israel “Gilead Shalit” katika Operesheni “Fallen Illusion” na nyota yake ilianza kung’aa kimataifa tangu wakati huo.