Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 5
Disemba 30, 2025 mjini Rabat, Morocco macho ya watanzania na hata Afrika Mashariki yatakuwa Stade Prince Moulay Abdellah Olympique Annexe. Kutaka kushuhudia Tanzania ikikipiga na Tunisia.
Ni mechi inayobeba zaidi ya alama tatu. Tanzania na Tunisia zinapambana si tu kwa kutaka kushinda tu bali kufuzu kutoka kundi C, kwa tiketi ya moja kwa moja kwenda hatua ya mtoano (16 bora) ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).
Kwa Tanzania, hii ni safari ya kutafuta ushindi wa kwanza kabisa katika historia ya AFCON, ushindi unaoweza pia kuweka historia nyingine ya kufuzu kwa mara ya kwanza 16 bora. Kwa Tunisia, ni kurejesha hadhi ya kigogo aliyeteleza katika toleo mashindano yaliyopita.
Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa mataifa haya mawili kukutana kwenye fainali za AFCON. Historia yao pekee inatoka kwenye mechi za kufuzu AFCON 2021, ambako Tunisia ilishinda 1-0 Radès kabla ya kutoka sare ya 1-1 Dar es Salaam. Lakini historia hiyo haibebi mzigo mkubwa katika mazingira ya sasa. Tanzania inaingia uwanjani ikiwa bado haijapoteza matumaini, huku Tunisia ikijua kosa dogo linaweza kuwagharimu.
Tunisia – Mbuyu mkubwa usioimbwa sana Afrika
Chanzo cha picha, Getty Images
Tunisia mara chache hutajwa kwenye orodha sawa na majina mengine kama Nigeria, Misri au Cameroon. Lakini kwa takwimu, ni moja ya timu kubwa zaidi barani Afrika. AFCON 2025 ni fainali yao ya 21, na kufuzu kwao hatua ya mtoano mara hii kutakuwa ni mara ya 15, rekodi inayoweka wazi ukubwa na uthabiti wao wa kihistoria.
Katika mashindano haya, Tunisia imeonyesha sura mbili. Walianza kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Uganda, wakionesha ufanisi mkubwa mbele ya lango. Kisha wakapoteza 3-2 dhidi ya Nigeria, licha ya kufunga mabao mawili ikiwa ni mara ya kwanza tangu 2008 kupoteza mechi ya AFCON baada ya kufunga angalau mabao mawili.
Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuna hatari yao, wamefunga mabao matano katika mashuti manane yaliyolenga lango, moja ya ufanisi w akuvutia langoni, wakiwa na kiwango cha asilimia 26 kwenye kutumia nafasi zao, ikiwa ni kiwango bora kuliko timu yoyote kwenye mashindano haya mpaka sasa.
Lakini kuna ufa mdogo kwenye ngome ya mbuyu huu. Tunisia imeshindwa kushinda mechi ya mwisho ya makundi katika AFCON tatu zilizopita. Tangu ushindi wa 4-2 dhidi ya Zimbabwe mwaka 2017, wamepata sare mbili tasa na kupoteza mara moja. Aidha, walitoka hatua ya makundi kwenye AFCON 2023, na kushindwa kufanya hivyo tena kutamaanisha kuondolewa mara mbili mfululizo katika hatua ya makundi, jambo ambalo halijatokea tangu 1982 na 1994.
Kwa maneno mengine, Tunisia ni mbuyu mkubwa, lakini si mbuyu usioyumba. Ni timu yenye makovu ya hivi karibuni na presha ya kurejesha heshima.
Tanzania – mbuyu mteke unaokua taratibu
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa Tanzania, AFCON 2025 tayari ni hadithi ya tofauti. Taifa Stars wamecheza mechi mbili, wakipoteza 2-1 dhidi ya Nigeria na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya ndugu zao Uganda. Bado hawajashinda mchezo hata mmoja katika fainali nne za AFCON walizowahi kushiriki, lakini pia hawajafanya vibaya sana kwa kiwango chao. Rekodi inaonyesha, wamepoteza mechi moja tu kati ya michezo minne ya mwisho ya AFCON, wakitoka sare 3.
Tanzania inasaka ushindi wake wa kwanza katika mechi 11 za AFCON, rekodi ambayo inatisha kwa macho ya nje. Lakini ndani ya takwimu hizo kuna dalili za kupiga hatua. Wamefunga katika mechi zote mbili za mashindano haya mwaka huu, jambo walilowahi kufanya mara ya mwisho mwaka 1980. Wameepuka kipigo katika mechi zao za mwisho za makundi mara mbili kati ya tatu zilizopita, ikiwemo sare ya 0-0 dhidi ya DR Congo mwaka 2023.
Hii ni Tanzania inayojifunza kushindana. Kocha Miguel Gamondi amebadilisha mtazamo wa timu kwa kiwango kikubwa. Timu inacheza unaiona ikibeba ujasiri dhidi ya majina makubwa. Dhidi ya Nigeria, walitengeneza nafasi kadhaa kama wangetumia vyema matokeo yangekuwa tofauti. Dhidi ya Uganda, walianza kupata bao, na dakika za mwisho walipata nafasi muhimu ya wazi, lakini walikosa. Kutengeneza nafasi za kufunga hasa dhidi ya timu kubwa ni ishara kubwa ya kupiga hatua kisoka.
Na katikati ya hadithi hii yupo Simon Msuva. Akiwa amefunga dhidi ya Uganda, Msuva sasa amefunga mabao matatu ya AFCON katika matoleo matatu tofauti, rekodi ya kipekee kwa Tanzania. Ni mchezaji wa kwanza wa Taifa Stars kufunga katika AFCON tatu tofauti, na kila bao lake limewahi kuwapa Tanzania uongozi wa mechi, hata kama ushindi haukufanikiwa.
Gamondi anakiri Tunia ni bora na ina wachezaji wenye uzoefu wa kutosha, hivyo kikosi chake kitaongeza umakini zaidi.
Kwanini Tanzania inaweza kuangusha mbuyu mkubwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Soka la Afrika lina kumbukumbu ndefu za mshangao. Katika AFCON 2021, Comoros iliwashangaza Ghana kwa ushindi wa 3-2 na kuwatupa nje ya mashindano. Ghana iliyokuwa na Thomas Partey, Andrey Ayew aliyelimwa kadi nyekudu katika mchezo huo, Jordan Ayew na wengine.
Mwaka 2022, Gambia ilifunga Tunisia 1-0 katika mechi ya makundi. Hata katika mchujo wa AFCON 2025, Tunisia yenyewe ilishawahi kufungwa 1-0 na Comoros nyumbani tukio lililobadilisha kabisa mwelekeo wa timu hiyo.
Kwa hivyo Tunisia inafungika. Inaruhusu kufungwa na imewahi kufungwa na timu za kawaida.
“Watanzania wanataka ushindi, mafanikio yenu yanabeba ndoto kubwa mtaani Tanzania”, anasema Naibu Waziri wa Michezo, Paul Makonda wakati akihamasisha kikosi hicho kuelekea mchezo huo.
Uzuri ni kwamba. Tanzania inaingia kwenye mechi hii bila mzigo wa historia ya ushindi, lakini pia bila hofu ya kupoteza kitu kikubwa. Kitaalamu, wanafunga. Kisaikolojia, wanapambana. Kimbinu, wameonyesha uwezo wa kuvunja mifumo ya timu kubwa.
Wachambuzi wengi wa Tanzania wanasema ili kushinda inahitaji vitu vitatu muhimu; kuwa wakatili na kuongeza utulivu wakati wa kushambulia, kujilinda na kumuheshimu mpinzani wake.
“Umakini wakati wakati wa kujilinda ni moja ya kitu cha msingi sana, mechi mbili (Tanzania) imeruhusu magoli matatu hizi sio takwimu nzuri kiulinzi”, anasema Salama Ngale, mmoja wa wachambuzi.
Tunisia inaweza kuwa na ubora wa majina na takwimu, lakini Tanzania ina jambo ambalo mara nyingi halipimiki kwa namba, jambo hilo ni wakati. Wakati sahihi wa kuandika historia. Wakati ambapo timu inajifunza, inaamini, na iko tayari kuchukua hatari.
Ikiwa kuna mechi ambayo shoka dogo linaweza kupata mpasuko kwenye mbuyu mkubwa, basi ni hii. Sio kwa sababu Tanzania ni bora kuliko Tunisia, bali kwa sababu soka la Afrika linaishi kwenye nyakati hizi ambapo mantiki inapinduliwa, na historia mpya inaandikwa.
Na kama Tanzania ambayo imehaidiwa na Serikali kila goli moja watapewa shilingi milioni 200 itavuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza kabisa, haitakuwa bahati tupu. Itakuwa matokeo ya mchakato unaokua, unaoanza kuzaa matunda mbele ya macho ya Afrika.