
Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imetoa tamko rasmi na kutangaza wasiwasi wake kuhusu tangazo la hivi karibuni la utawala wa Kizayuni la kuitambua Somaliland kama nchi huru.
Katika taarifa yake hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini imesema kuwa, hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni ya kutambua kujitenga Somaliland na ardhi nyingine ya Somalia ni tishio la moja kwa moja kwa amani na usalama wa eneo zima la Pembe ya Afrika.
Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema kuwa, Afrika Kusini itaendeelea kuunga mkono kanuni ya Umoja wa Afrika ya kuheshimiwa mipaka ya nchi wanachama wa umoja huo ikiwemo Somalia.
Katika taarifa hiyo, Afrika Kusini imeihimiza jamii ya kimataifa kuzuia hatua za baadhi ya madola kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kuunga mkono umoja wa ardhi yote ya Somalia.
Kwa upande wake, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) imesema katika kikao chake cha dharura kwamba inalaani kitendo cha Israel cha kuitambua Somaliland kama “nchi huru.”
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo limekemea hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kulitambua eneo la Somalia la Somaliland kama nchi huru. Baadhi ya mataifa yameelezea wasiwasi wao kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa hali ya Wapalestina huko Ghaza.
Naye Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei amesema mbele ya waandishi wa habari kwamba, hakuna taifa linalounga mkono kujitenga Somaliland na kwamba kitendo hicho cha Wazayuni ni hatua isiyo na msingi wowote wa kisheria wala kisiasa.