
Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu amesema hatua ya Chuo Kikuu cha Georgetown cha Marekani ya kukata uhusiano naye ni sehemu ya vikwazo alivyowekewa na Washington kwa kufichua mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza, na ushiriki wa Marekani katika jinai hizo.
“Uamuzi wa Georgetown wa kuvunja uhusiano wangu wa miaka 10 ni matokeo mengine ya vikwazo ambavyo Marekani iliniwekea Julai iliyopita kwa kufichua mauaji ya kimbari ya Israel na ushiriki wa Marekani,” Albanese amesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii X Jumatatu.
“Maelezo mengine yoyote ni propaganda ya kawaida ya kuchekesha ya wafuasi wanaounga mkono mauaji ya kimbari,” ameongeza Albanese. Chuo Kikuu cha Georgetown kimetangaza kwamba, hakina mfungamano wowote tena na Albanese, ambaye aliwekewa vikwazo na Marekani mapema mwaka huu.
Julai mwaka huu 2025, Marekani ilitangaza kumwekea vikwazo ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Vikwazo hivyo vilifuatia ripoti kali aliyoitoa Albanese tarehe 30 Juni, ambapo aliyataja makampuni zaidi ya 60, yakiwemo makampuni makubwa ya kiteknolojia ya Marekani kama Google, Amazon na Microsoft, ambayo alisema yamehusika kwa njia moja au nyingine katika mauaji ya kimbari Gaza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Robio alisema Washington imemuwekea vikwazo afisa huyo wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, kutokana na eti hatua zake ‘zisizo halali’ na za ‘kuaibisha’ kutaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ichukue hatua dhidi ya maafisa na makampuni ya Marekani na Israel, na watendaji wao.