Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepinga kwa mara nyingine hatua ya utawala wa Kizayuni kutangaza kutambua eneo la Somaliland la Somalia kama nchi huru, ikieleza kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuleta machafuko katika eneo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu, alisema hakuna taifa lililounga mkono hatua hiyo, akisisitiza kuwa kutambua sehemu ya ardhi ya Somalia kama nchi huru ni hatua isiyo na msingi msingi wowote wa kisheria wala kisiasa.

Baghaei aliongeza kuwa kitendo hicho, kilichotekelezwa na utawala usio na uhalali, kimekusudiwa kugawanya nchi za Kiislamu, kuharakisha kuvunjika kwa mshikamano wa kikanda, na kuacha eneo likiwa dhaifu mbele ya tamaa na hujuma za Israel.

Amesema taasisi muhimu za kieneo ambazo ni Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Kiarabu, na Umoja wa Afrika, zote zimepinga waziwazi tangazo hilo la utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidha, amesisitiza kuwa hakuna msingi wa hatua hiyo ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa wala chini ya sheria za kimataifa, hususan kuhusu kuheshimu mipaka na mamlaka ya kitaifa.

Baghaei amesema kitendo hicho cha Israel kinazidi mipaka ya jaribio la kutenganisha sehemu ya nchi ya Kiislamu, bali ni sehemu ya mkakati mpana wa kuleta machafuko katika ukanda mzima wa Asia ya Magharibi, Pembe ya Afrika na Bahari Nyekundu.

Akihitimisha, Baghaei amesema ana matumaini kuwa tukio hilo litakuwa kengele ya tahadhari kwa mataifa ya eneo na kwingineko, akisisitiza kwamba Iran inazitazama hatua za utawala wa Kizayuni kama ambazo “kimsingi ni dhidi ya amani” na zinakusudia kuchochea mivutano, mgawanyiko na migogoro.

Utawala wa Kizayuni ulitangaza Ijumaa kutambua jimbo la Somalia la Somaliland kama “taifa huru”, hatua iliyozua ukosoaji mkubwa kimataifa. Baghaei ameongeza kuwa lengo la Israel ni kuona eneo likiwa “bila ulinzi”, lakini akabainisha kuwa mataifa ya kikanda sasa yamekubaliana kwamba njia pekee ya kufanikisha amani na uthabiti wa kudumu ni kuuzuia utawala wa Kizayuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *