
Uamuzi wa Serikali kuanzisha kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mkoani Lindi, unaanza kubadili taswira ya mkoa huo ambao kwa muda mrefu ulikuwa nje ya mkondo mkuu wa maendeleo ya elimu ya juu.
Kampasi hiyo, itakayojikita katika programu za kilimo, sayansi ya udongo, teknolojia na usindikaji wa chakula, biashara za kilimo pamoja na maeneo shirikishi kama madini, mazingira, ikolojia na urithi wa mambo ya kale, imefikia hatua ya asilimia 60 ya ujenzi.
Desemba 20, 2025, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba aliweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi wa kampasi hiyo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jakaya Kikwete, kampasi ya Lindi inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi katika mwaka wa masomo wa 2026/2027.
Mwananchi limezungumza na wakazi wa Mkoa wa Lindi, hususan vijiji jirani na eneo la Ngongo ambako kampasi hiyo inajengwa.
Wakazi hao wameeleza matumaini makubwa ya elimu ya juu kufika katika mkoa ambao kwa miaka mingi haukuwa na historia imara ya kitaaluma.
Wengi wao wanaona kampasi hiyo kama mwanzo wa ukurasa mpya wa maendeleo na fursa, wakisema kwa muda mrefu walishuhudia vyuo vikuu vikubwa vikijengwa katika kanda nyingine huku Kusini ikibaki nyuma.
Mkazi wa Lindi Mjini, Hassan Mfaume, anasema uamuzi huo umeleta hisia ya kutambuliwa na kufungua milango mipya ya maendeleo ya kielimu.
“Kwa muda mrefu tulihisi kama Lindi haisikiki. Vyuo vikuu vilikuwa mbali nasi. Kampasi hii ni ujumbe kwamba na sisi ni sehemu ya Tanzania ya maendeleo,” anasema.
Kwa upande wake, Halima Bakari, mzazi na mkazi wa Mpilipili, anasema uwepo wa chuo kikuu karibu na jamii utapunguza gharama na vikwazo kwa familia za kipato cha chini.
“Mzazi wa kijijini anapomsikia mtoto amepata chuo Dar es Salaam, anaanza mawazo. Sasa watoto wetu wanaweza kusoma bila familia kuingia kwenye madeni makubwa,” anasema.
Mkazi wa Ruangwa, Mussa Mtonya, anaeleza kuwa uwepo wa chuo kikuu utabadilisha mtazamo wa watoto na vijana kuhusu elimu.
“Mtoto akiona chuo kiko jirani, anaamini anaweza kufika. Hii itaongeza bidii shuleni na kupunguza mimba za utotoni na ajira duni,” anasema.
Mwalimu mmoja wa shule ya kata, ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema tayari wanafunzi wameanza kuuliza maswali kuhusu kozi zitakazofundishwa katika kampasi hiyo.
“Hapo awali wanafunzi hawakuwa na mwelekeo. Sasa wanazungumza kuhusu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiwa Lindi. Hili limetupa matumaini makubwa,” anasema.
Mbali na elimu, wananchi wanaiona kampasi hiyo kama kichocheo cha shughuli za kiuchumi.
Wafanyabiashara wadogo na watoa huduma wanasema tayari kuna dalili za mabadiliko.
Salum Khamis, dereva wa bodaboda, anasema eneo la ujenzi limeanza kuvutia watu wengi zaidi.
“Kabla hapakuwa na watu wengi. Sasa mafundi, wahandisi na wageni wanaingia. Tukipata wanafunzi na walimu, kipato kitaongezeka zaidi,” anasema.
Maelezo ya UDSM
Akizungumza kuhusu mradi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, anasema uamuzi wa kuanzisha kampasi ya kilimo mkoani Lindi umetokana na utajiri mkubwa wa rasilimali zilizopo katika mkoa huo.
Anasema kampasi hiyo ni fursa si kwa Mkoa wa Lindi pekee, bali pia kwa mikoa jirani, kwani itatoa elimu ya juu inayojikita katika mafunzo kwa vitendo na sayansi tumizi.
“Lindi ni kinara wa uzalishaji wa mazao ya kimkakati kama korosho na ufuta, yenye mchango mkubwa katika uchumi wa mikoa ya Kusini na Taifa kwa ujumla. Pia kuna mazingira mazuri kwa tafiti za kilimo endelevu, mazingira na mabadiliko ya tabianchi,” anasema.
Anaongeza kuwa mkoa huo una rasilimali nyingine muhimu, ikiwemo madini ya grafiti na urithi wa kihistoria na kisayansi kupitia mabaki ya dinosaur ya Tendaguru.
“Kupitia kampasi hii, tutaimarisha elimu ya juu, tafiti na ubunifu unaolenga matumizi bora ya rasilimali, kukuza teknolojia na kuongeza mchango wa sayansi na historia asilia katika maendeleo ya Taifa,” anaeleza.
Anasema mkazo utawekwa katika huduma za ugani na tafiti za kilimo kwa mazao kama korosho, ufuta, mbaazi na mengineyo, ili kuwawezesha wakulima wadogo, vijana na wanawake kuongeza thamani ya mazao na kufungua masoko mapya.
Athari za kiuchumi kwa Kusini
Kwa mtazamo wa kiuchumi, mtaalamu wa uchumi Fredrick Rwehumbiza anasema kampasi ya UDSM Lindi ina uwezo wa kubadilisha uchumi wa mkoa ikiwa itaunganishwa na mipango madhubuti ya maendeleo.
“Vyuo vikuu ni injini za uchumi wa maeneo yanayovipokea. Huongeza ajira, huleta maarifa mapya na kuimarisha sekta za huduma. Hata hivyo, bila mipango bora ya ardhi na miundombinu, manufaa yanaweza yasiwafikie wananchi wengi,” anasema.
Anashauri serikali za mitaa kupanga mapema masuala ya makazi, barabara, maji na umeme ili kuendana na ongezeko la watu.
Mhadhiri wa sayansi ya jamii, Dk Jemina Swai, anasema uwepo wa chuo kikuu unaweza kuibua kazi za kitafiti zitakazolenga kutatua changamoto mahsusi za kusini, ikiwemo kilimo, mazingira na ajira kwa vijana.
“Lindi inaweza kuwa kitovu cha elimu na utafiti Kusini mwa Tanzania kama fursa hii itatumika ipasavyo,” anasema.
Usuli wa mradi
Serikali imetenga Sh14.8 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kampasi ya Lindi. Mradi huo unahusisha jengo la utawala na taaluma lenye ofisi za watumishi na madarasa sita yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 360, karakana ya kilimo, maabara yenye uwezo wa wanafunzi 125, pamoja na mabweni mawili ya wanafunzi 200.
Aidha, mradi unajumuisha ujenzi wa Kituo cha Utafiti cha Ruangwa chenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 50, kikijumuisha bweni, darasa, bwalo la chakula na huduma za kijamii.