Diamond

Chanzo cha picha, WCB

Muda wa kusoma: Dakika 5

Mwaka 2025 uliingia katika historia ya Tanzania si kwa sababu ya uchaguzi pekee, bali kwa namna ulivyobadilisha kabisa uhusiano kati ya wasanii na jamii, hasa vijana.

Huu ulikuwa mwaka ambao umaarufu ulipimwa kwa msimamo, na burudani ikavuka mipaka yake ya kawaida na kuingia moja kwa moja kwenye siasa, maadili na dhamira ya kiraia.

Ras Inno Nganyagwa mchambuzi wa masuala ya sanaa ya muziki na burudani anasema kwamba wasanii walitumika katika namna ambayo ilisababisha mgawanyiko kwenye jamii na kwa sehemu kubwa kutokana na 2025 kuwa na uchaguzi mkuu.

”Kwa upande wa sanaa tunaweza kusema ulikuwa mwaka “nusu” kutokana na shughuli za uchaguzi kupamba moto kuanzia mwezi wa nane” alieleza Ras Inno

Kuanzia Agosti hadi uchaguzi wa Oktoba 29, Tanzania ilishuhudia mgawanyiko mkubwa wa maoni.

Kulikuwa na waliotaka uchaguzi ufanyike kama kawaida, na wengine waliodai mabadiliko ya kikatiba na nafasi zaidi ya kidemokrasia kupitia maandamano.

s

Chanzo cha picha, WCB

Ndani ya mvutano huu, wasanii hasa wanamuziki, waigizaji na watu maarufu mitandaoni walijikuta katikati ya macho ya umma.

Kilichoshangaza wengi ni kwamba karibu asilimia kubwa ya majina makubwa ya sanaa yaliamua kusimama upande mmoja na kuunga mkono uchaguzi na mara nyingine kuonekana kuhalalisha hatua za serikali dhidi ya maandamano.

Kwa upande wao, huenda waliona ni uamuzi wa kawaida wa kiraia au hata fursa ya kikazi.

Lakini kwa vijana wengi, hasa walioko mitandaoni, hatua hiyo haikuchukuliwa kama jambo la kawaida.

Hapo ndipo harakati ya kususia wasanii ilipozaliwa. Haikuwa maandamano ya barabarani, bali ya kimya na ya kidijitali: ku-unfollow, kutosikiliza muziki kwa njia ya mtandao, kutoshirikisha kazi zao, na kuwapuuza kabisa.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa ya Tanzania, vijana walitumia nguvu yao ya pamoja kuamua nani atasikika na nani atapotea.

S

Chanzo cha picha, Roma Mkatoliki

Ulikuwa ujumbe mzito umaarufu hauko tena mikononi mwa redio na televisheni, bali kwenye simu za mashabiki.

Uchaguzi ulipomalizika na baadhi ya maandamano kutokea, gharama za kisiasa za umaarufu zilianza kuonekana wazi.

Biashara za baadhi ya wasanii zikaharibiwa, hali iliyoamsha mjadala mpya: Je, msanii ana jukumu gani kwa jamii? Je, umaarufu una wajibu wa kusimama na wananchi au ni haki binafsi kuchagua upande wowote?

Zaidi ya mwezi mmoja baada ya matukio hayo, harakati za mtandaoni hazikupoa. Badala yake, ziliongezeka.

Kauli za kuomba radhi zilianza kutolewa kwa niaba ya tasnia, na baadaye wasanii mmoja mmoja wakaanza kuzungumza.

Lakini hata kauli hizo hazikutosha kuzima mjadala. Vijana walihoji si maneno tu, bali msimamo wa dhati.

Wasanii wengine wakongwe na wanaharakati waliweka wazi msimamo wao: hili halikuwa suala la chama, bali la msanii kushindwa kusimama na wananchi.

Kauli hizo ziliongeza uzito wa mjadala na kuufanya uwe wa kizazi kizima, si wa mashabiki pekee.

Kilichofanya 2025 kuwa mwaka wa kipekee ni ukweli kwamba hakuna upande uliokuwa “umekosea” kabisa.

Wachambuzi wengi walikubaliana kuwa msanii ana haki ya kuchagua upande wowote wa kisiasa. Vivyo hivyo, vijana wana haki ya kuchagua nani wa kumpa muda, pesa na usikivu wao. Mgongano ulikuwa kati ya haki hizi mbili.

Hatimaye, mwaka 2025 uliweka wazi dhana mbili muhimu. Kwanza, kizazi kipya hakitaki mastaa wa kupendwa tu, bali mastaa wanaoonekana kuwa pamoja nacho, hata kama hawakubaliani kila jambo.

Pili, msanii ni binadamu ana ndoto, mahitaji na maamuzi magumu ya kufanya, ikiwemo kukubali au kukataa dili za kisiasa.

Ni mwaka ambao uliwaacha wasanii wengi njia panda: kusikiliza sauti ya mashabiki wao wakuu au kusimama na misimamo yao binafsi bila kujali gharama. Jibu la swali hilo bado halijapatikana, lakini athari zake zitaishi muda mrefu katika historia ya sanaa ya Tanzania.

Mwaka 2025 umeendelea kuonyesha taswira mchanganyiko wa tasnia ya sanaa nchini Tanzania.

Upande mmoja, kumekuwepo na matamasha ya kitamaduni na muziki yaliyozoeleka kama Busara Zanzibar na ZIFF pamoja na matukio ya Utamaduni Bagamoyo ambayo yameendelea kudumisha hadhi yake kama majukwaa rasmi ya sanaa.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, kumekuwa na mabadiliko ya namna muziki unavyowasilishwa kwa umma hasa kupitia matukio yanayohusishwa moja kwa moja na mpira wa miguu.

Kwa mwaka huu, klabu kubwa za Simba na Yanga zimeendelea kutumia muziki kama sehemu ya utambulisho wao wa matukio makubwa.

Uzinduzi wa jezi, sherehe za mashabiki na matukio ya kihistoria ya vilabu hivi yameambatana na burudani za muziki zilizopangwa rasmi, zikihusisha wasanii wakubwa na kuzitambua kama sehemu halali ya ratiba za sanaa.

Kwa mara ya kwanza, matukio haya hayakuonekana kama burudani ya pembeni, bali kama majukwaa rasmi ya wasanii kufikia hadhira kubwa.

Je kuna mafanikio ya kudumu?

S

Chanzo cha picha, Getty Images

Hata hivyo, pamoja na mwanga huo, mabadiliko ya kimuundo katika tasnia ya sanaa bado yamekuwa yakisuasua. Hali hii imefananishwa na mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini matarajio ni makubwa, lakini utekelezaji umekuwa wa taratibu na mara nyingine kukwama kabisa.

Moja ya mifano ni juhudi za kuanzisha taasisi za kukusanya na kusimamia mirabaha kwa maslahi ya wasanii wenyewe (CMO).

Akizungumza kuhusu suala hilo, mchambuzi wa masuala ya sanaa Ras Inno anaeleza kuwa:

“CMO ziliasisiwa kwa nia njema, lakini zilikumbwa na changamoto nyingi za kiutendaji. Kiwango cha utekelezaji wa vitendo ni kama asilimia 45 tu. Mabadiliko yamekwenda kwa kiasi fulani, lakini hayajadumu wala hayajaweza kusukuma tasnia mbele ipasavyo.”

Kauli hiyo inaakisi hali halisi ya wasanii wengi ambao bado hawajaona manufaa ya moja kwa moja ya mifumo hiyo, hali inayosababisha kukata tamaa na kutoamini mifumo iliyopo.

Pamoja na changamoto hizo, tasnia haijakosa mafanikio. Wasanii waliovuka mipaka ya ndani ya nchi, hasa kutoka kizazi kipya, wameendelea kuonyesha mwelekeo mpya wa kimataifa.

Ushiriki wao katika tuzo za nje ya nchi, maonyesho ya kimataifa na kutumbuiza katika mataifa jirani umeipa Tanzania mwonekano mpana zaidi katika ramani ya muziki wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Ras Inno anasisitiza kuwa “Kizazi kipya cha wasanii kimevuka mipaka ya kawaida. Tumeona wakishiriki tuzo za nje, kutumbuiza nchi jirani na kuwakilisha Tanzania kimataifa. Hili ni jambo kubwa kwa tasnia.”

Hata hivyo, mafanikio hayo hayajaondoa changamoto ya msingi ya ubunifu. Kwa mtazamo wa wachambuzi wengi, Tanzania bado haina kasi kubwa ya kuzalisha ubunifu mpya unaoakisi mabadiliko ya kijamii na kitamaduni. Kuna dalili za mgando wa kimtindo, ambapo sauti na maudhui yanajirudia bila kuleta mapinduzi makubwa ya kisanaa.

Mitandao ya kijamii, kwa upande wake, imeendelea kuwa chombo chenye nguvu kubwa katika tasnia.

Imewawezesha wasanii kufikia mashabiki wao moja kwa moja bila kupitia vichujio vya redio na televisheni. Leo, msanii anaweza kusikika Afrika Mashariki, Ulaya au Marekani kwa wakati mmoja kupitia majukwaa ya kidijitali.

“Mitandao ya kijamii imefanya makubwa sana. Imewapa wasanii uwezo wa kuwafikia mashabiki wao popote walipo, si Afrika Mashariki tu bali duniani kwa ujumla.” alisisitiza Ras Inno.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *