Wataalamu wa Palestina wamefichua ukatili na ukandamizaji unaowakabili mahabusu na mateka wa Palestina katika magereza ya utawala wa Israel na mienendo isiyo ya kibinadamu na ukatili wa Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala huo dhidi ya wafungwa wa Kipalestina.

Abdul Nasser Farwaneh, mtaalamu wa masuala ya wafungwa wa Palestina, amesema: “Vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya watu wa Palestina vimehusisha watu wote, wakiwemo mateka na mahabusu wa Palestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.”

Ameongeza kuwa: “Uhalifu wa Wazayuni dhidi ya mateka na mahabusu wa Kipalestina, wanaume na wanawake, tangu Oktoba 7, 2023 hautasawariki wala hauna kikomo. Kilichosemwa hadi sasa ni tone la baharini ikilinganishwa na uhalifu uliofanywa.”

Farwaneh amesema: “Wapalestina hao wananyimwa usingizi na huduma za matibabu, na wanateswa kwa njaa, kiu na mateso mengine ya kimwili na kiakili.” Ameongeza kuwa: Gereza la Sde Teiman ni nembo ya ukatili huo wa kutisha. 

Ameendelea kusema kuwa: “Hali hii ni ushahidi wa hatua zilizochukuliwa kwa makusudi na Israel dhidi ya mabahusu wote wa Kipalestina, hasa wale waliofungwa kutoka Gaza.”

Mtaalamu huyo amesema: “Vitendo vinavyofanywa dhidi ya Wapalestina  ni uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya ubinadamu chini ya sheria ya kimataifa. Ameiomba jamii ya kimataifa itimize majukumu yake na kuiwajibisha Israel kwa uhalifu huo.

Kwa upande wake, Amjad Al-Najjar, Mkurugenzi wa Klabu ya Wafungwa wa Palestina, amesema Israel inaendeleza sera ya mauaji ya makusudi dhidi ya mahabusu wa Palestina ndani ya magereza ya utawala huo, akisisitiza kuwa: “Mahabusu hao wanapambana na hali ngumu ndani ya magereza ya Israel.” 

Al-Najjar amesema mauaji ya wafungwa wa Palestina yamepangwa kwa amri ya moja kwa moja ya Itamar Ben-Giver, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Israel, na viongozi wengine wa utawala huo.

Amesema, kuuawa shahidi Hassan Sakhr Zawul na Abdul Rahman Al-Sabateen katika siku za karibuni ni ushahidi wa wazi wa mbinu ya serikali ya Israel ya mauaji ya kupanga dhidi ya mahabusu wa Kipalestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *