Vikosi vya Ulinzi vya Iran vimetangaza kuwa, vimejiandaa kikamilifu kutoa majibu makali kwa tishio lolote la usalama wa Jamhuri ya Kiislamu na watu wake na kuonya kwamba, uchokozi wowote mpya wa uadui dhidi ya Iran utakuwa mkali zaidi, angamizi zaidi na wenye madhara makubwa zaidi kuliko huko nyuma.

Katika taarifa yake ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 16 ya maandamano ya nchi nzima ya wananchi wa Iran ya kuulinda mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusambaratisha fitna za maadui mwaka 2009 maarufu kwa jina la Dey 9, Komandi Kuu ya Majeshi ya Iran imesema kuwa,  maandamano hayo yalikuwa ni dhihirisho la umakini na uimara wa umma, umoja na uaminifu wa wananchi kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Taarifa hiyo imetolewa sambamba na matamshi ya Admirali Ali Shamkhani, Mshauri mwandamizi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ambaye amelaani vikali vitisho vipya vya Marekani vya kuishambulia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu, akiapa kuwa jibu kali litatolewa endapo utafanywa uchokozi wowote ule.

Shamkhani ameyasema hayo katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii jana Jumatatu na kubainisha kwamba, kwa mujibu wa doktrini ya ulinzi ya Iran, majibu dhidi ya vitisho hupangwa kabla ya kutolewa vitisho hivyo na kwamba uwezo wa makombora na wa ulinzi wa Iran si kitu cha kujadiliwa na hauwezi kuwekewa udhibiti au kutegemea ruhusa ya mtu yeyote.

Jibu hilo limetolewa baada ya rais wa Marekani Donald Trump kusema kwamba ataunga mkono shambulio la kijeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran ikiwa Tehran itaendelea na mipango yake ya makombora ya balestiki na shughuli zake za matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *