Makabila atumia Mil.20 kwenye video mpyaMakabila atumia Mil.20 kwenye video mpya

MSANII wa muziki wa kizazi kipya na miondoko ya Singeli, Abdallah Ahmed, maarufu kama ‘Dulla Makabila’, amesema ameweka rekodi mpya katika safari yake ya sanaa baada ya kutumia Sh milioni 20 kwa ajili ya kutayarisha video ya wimbo wake mpya.

Dulla Makabila amebainisha hayo kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Instagram, akieleza kuwa matumizi ya kiasi hicho cha fedha ni hatua kubwa ya ukuaji binafsi na juhudi za kuinua hadhi ya muziki wa Singeli nchini ili uweze kushindana kimataifa.

Akilinganisha uwekezaji huo na hali halisi ya sasa katika tasnia ya Singeli, “kwa mara ya kwanza nimelipia Sh milioni 20 kwa ajili ya video moja. Jambo hili linaweza kuonekana la kawaida kwa wasanii kama Diamond Platnumz, lakini kwa upande wetu wa Singeli ni hatua kubwa. Wasanii wengi wa miondoko hii hulipia gharama ndogo, hali inayopelekea video zetu kukosa ubora unaotakiwa,” aliandika Dulla.

Msanii huyo amesema uamuzi huo ni sehemu ya uwekezaji wa kimkakati ambao anaamini utaleta tija katika siku zijazo, huku akiwashukuru wadau mbalimbali wa tasnia ya burudani kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kukuza sanaa nchini. SOMA: Dulla Makabila aitwa Basata kuhusu wimbo Pita Huku

Aidha, alimpongeza mwongozaji wa video hiyo, anayefahamika kwa jina la Fole_x, akibainisha kuwa ubora wa maudhui na picha unapaswa kuendana na thamani ya fedha iliyowekwa ili kumpa mlaji (shabiki) kile anachostahili.

Dulla ametoa wito kwa wasanii wenzake wa muziki wa Singeli kubadilika na kuanza kuuchukulia muziki kama biashara inayohitaji uwekezaji mkubwa ili kupata matokeo bora, badala ya kutegemea njia rahisi ambazo hazileti ushindani katika soko la kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *