Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
-
- Author, Stewart Maclean
- Nafasi, BBC
-
Muda wa kusoma: Dakika 6
Matukio ya kutisha ya Oktoba nchini Tanzania yanatoa muhtasari wa baadhi ya matukio ambayo yametokea katika mwaka mgumu kisiasa barani Afrika.
Waandamanaji walipigwa risasi na polisi na kufa walipokuwa wakipinga kile walichokiona kuwa ni uchaguzi uliokuwa na udanganyifu – uliokosolewa na vyombo vya kikanda na vya bara – na kuharibu sifa ya nchi hiyo ya amani na utulivu.
Huku wagombea wa upinzani wakiwekwa ndani au kuzuiwa kugombea, Rais Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kwa asilimia 98 ya kura.
Nchi kadhaa zilishuhudia maandamano na mizozo ya wakati wa uchaguzi mwaka 2025, huku viongozi wa kijeshi wakiimarisha mamlaka yao, na wachambuzi wanaamini mwaka ujao unaweza kuwa wa misukosuko zaidi.
“Tukiangalia picha jumla kote barani, hali inatia wasiwasi,” anasema Mo Ibrahim, ambaye taasisi yake inafuatilia hali ya utawala bora barani Afrika.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu utawala, ripoti ambayo inaangazia mambo kama usalama, ushiriki katika kufanya maamuzi na hali ya afya na elimu, yaonekana maendeleo yamesimama ikilinganishwa na muongo mmoja nyuma hadi 2022.
“Ongezeko la mapinduzi [katika miaka ya hivi karibuni], kurejea kwa serikali za kijeshi na kuminywa kwa demokrasia, vyote vinaashiria tatizo moja: kushindwa kwa tawala.”
Kuongezeka kwa gharama ya maisha kumekuwa cheche iliyowasha moto wa kutoridhika katika sehemu nyingi za Afrika.
Bw. Ibrahim aliiambia BBC, “hatari kwa Afrika ni kwamba mifumo hii mibaya imeenea bila kudhibitiwa, maendeleo mengi yaliyopatikana katika miongo ya hivi karibuni yanaweza kurudi nyuma.”
Hofu na matumaini
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Licha ya yote hayo, kwa wale wanaoamini demokrasia ndiyo njia bora ya kutimiza mahitaji ya watu, kumekuwa na mambo chanya mwaka 2025 kutokana na viongozi kupishana madarakani kwa amani na uchaguzi huru na wa haki.
Nchini Malawi, kwa mfano, kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Peter Mutharika, alishinda tena urais baada ya kipindi cha kuwa mpinzani.
Shelisheli ilishuhudia chama tawala cha muda mrefu United Seychelles kikirejea madarakani, miaka mitano baada ya kupoteza madaraka.
Viongozi wote wawili walio madarakani walipoteza nafasi zao kutokana na kushindwa kupunguza athari za mfumuko wa bei.
Kushindwa huko pia kumeleta athari kwa vyama tawala mwaka 2024.
Nchini Afrika Kusini, Chama cha African National Congress kilipoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza tangu 1994 na kuingia katika serikali ya kugawana madaraka pamoja na chama cha upinzani.
Nchini Senegal, mchanganyiko wa maandamano ya mitaani na mahakama, vilizuia majaribio dhahiri ya rais ya kuongeza muda wake madarakani na mwanasiasa asiyekuwa na umaarufu alichaguliwa kuwa rais baada ya kiongozi mkuu wa upinzani kupigwa marufuku.
Lakini wachambuzi wanasema mabadiliko hasi katika baadhi ya nchi ni ushahidi kuwa demokrasia barani Afrika inapingwa.
Mfano, uwepo wa serikali za kijeshi katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi.
Mali, Niger, na Burkina Faso zote zilijitenga na jumuiya ya kikanda, Ecowas, na kuunda muungano mpya wa serikali ambao ulichukua madaraka kupitia mapinduzi.
Vijana na Wazee
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Afrika ni bara lenye idadi kubwa zaidi ya vijana lakini ina viongozi wazee zaidi duniani. Katika nchi nyingi mitandao ya kijamii inasaidia kuelimisha kizazi kipya ambacho kinazidi kuhitaji kusikilizwa.
Nchini Cameroon, wastani wa umri, kulingana na Umoja wa Mataifa, ni zaidi ya miaka 18. Lakini mwaka huu nchi hiyo ilishuhudia Paul Biya akiendelea kukaa madarakani – rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 92, ambaye ameshikilia wadhifa huo kwa miaka 43, aliapishwa kwa muhula wa nane, ambao utamfanya kuwa rais hadi atakapofikisha karibu miaka 100.
Ni baada ya duru ya uchaguzi uliogawanya watu mwezi Oktoba, ulioshutumiwa na wakosoaji kuwa haukuwa huru wala wa haki – tuhuma zilizokataliwa na serikali.
Vikosi vya usalama havikufanya matukio ya kutisha, lakini ni kama ilivyokuwa Tanzania, hasira kuhusu matokeo ya uchaguzi yaligeuka kuwa siku za maandamano – ishara dhahiri jinsi vijana wanavyompinga hadharani rais wa muda mrefu wa Cameroon.
Maandamano ndio jibu?
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maandamano nchini Cameroon na Tanzania hayakusababisha mabadiliko. Lakini kwa wale wanaofikiria kuchukua hatua kama hiyo, kuna la kujifunza mwaka 2025 kuhusu jinsi maandamano yanavyoweza kutoa matokeo.
Septemba, taifa la kisiwa cha Bahari ya Hindi la Madagaska lilikumbwa na maandamano ya wiki kadhaa yaliyoongozwa na vijana dhidi ya huduma duni za kijamii, na kumlazimisha Rais Andry Rajoelina wa nchi hiyo kulifuta baraza lake lote la mawaziri.
Lakini hilo halikutosha kuokoa uongozi wake. Maandamano yaliendelea na mwezi Oktoba, Rajoelina aliondolewa madarakani kwa mapinduzi. Jeshi la nchi hiyo tangu wakati huo limemweka afisa wa zamani Michael Randrianirina kama rais wa mpito.
Ingawa serikali za kijeshi ni kikwazo kwa demokrasia, lakini zinaweza kutumika kama ukumbusho kwa viongozi wa kiraia kwamba wanahitaji kusikiliza madai ya wapiga kura wao.
Wachambuzi wanaamini maandamano yanaweza kuwa sehemu ya siasa za Afrika kadiri muda unavyosonga.
“Tunaona maandamano mengi,” anasema Nerima Wako, mkurugenzi mtendaji wa Saisa, shirika la Kenya linalofanya kazi kuwasaidia vijana kushiriki katika siasa. “Sio njia bora ya kuleta mabadiliko, lakini mara nyingi ndiyo njia pekee.”
“Barua pepe, ujumbe mfupi wa simu kwa wabunge, malalamiko – unaambiwa hizi ndizo njia unazohitajika kutumia. Zipofanya kazi, kinachobaki ni maandamano.”
“Tunaona huduma za kijamii zikiporomoka,” anaongeza. “Kote barani Afrika vijana wanataka upatikanaji wa huduma za afya, maji, na fursa.”
“Wanaomba vitu sahihi, haya ni mambo ambayo serikali zinatakiwa kutoa, lakini hatari ni kwamba serikali hazifanyi vya kutosha.”
Adem Abebe, mshauri katika Taasisi ya Kimataifa ya Demokrasia na Usaidizi wa Uchaguzi, anasema: “Hisia ya kuridhika inapungua. Watu hawafurahii wanachopata, kuna hisia inayoongezeka ya hasira kuhusu kudhoofika kwa uhuru wa kisiasa na ukosefu wa huduma za kijamii.”
Washirika wa Kimataifa

Lakini mchambuzi huyo pia anataja kuhusika kwa siasa za nje ya bara – kwani serikali nyingi za Magharibi zimepumbazwa na migogoro ya maeneo mengine.
Anasema siasa za kijiografia zimezipa serikali za bara hilo uhuru zaidi kuendelea na tawala za kimabavu.
Marekani, ambayo hapo awali ilionekana kuwa na nia ya kutumia nguvu na ushawishi wake kuimarisha demokrasia, sasa inajali zaidi uhusiano wa kibiashara chini ya Rais Donald Trump.
“Hapo awali, Ulaya na Magharibi zilisisitiza mifumo ya kidemokrasia kama kigezo cha usaidizi wao barani Afrika,” anasema Adem.
“Washirika wa kidemokrasia wanarudi nyuma na serikali za Afrika zina uwezo wa kujinufaisha – zina chaguzi, kama vile China au Urusi, na zina fursa ya kutekeleza malengo yao bila kuogopa onyo la washirika wa kimataifa.”
Wiki za mwisho za mwaka 2025 zimeshuhudia mapinduzi mengine, Guinea-Bissau, Afrika Magharibi, na kufikisha jumla ya nchi nane barani humo ambazo sasa zinaendeshwa na jeshi.
Pia kulikuwa na jaribio la mapinduzi nchini Benin ambalo lilisababisha uingiliaji kati wa haraka kutoka Ecowas. Uingiliaji kati huo unaashiria ulinzi wa demokrasia katika Afrika Magharibi.
Wiki za kwanza za Januari kutakuwa na uchaguzi nchini Uganda – iliyotawaliwa kwa miaka 40 na Rais Yoweri Museveni, 81. Chaguzi zilizopita nchini humo zimegubikwa na madai ya ukiukwaji wa sheria na vurugu.
Kwa Ibrahim, swali muhimu sasa ni jinsi serikali za Afrika zinavyojibu kile wanachokisikia kutoka kwa vijana wa bara hilo.
“Vijana wa Afrika wako idadi kubwa ya watu,” anasema. “Hili lazima litafsiriwe katika utendaji wa kidemokrasia.
“Tukiwasikiliza, tukiwekeza kwa ajili yao, tukiheshimu haki zao na kuzingatia matarajio yao, basi miaka ijayo inaweza kuwa ya mabadiliko makubwa kwa bara.”
“Tuko katika mgogoro,” anasema Bi. Wako. “Tazama kote Afrika na unaona serikali nyingi ambazo zinachelewa kutekeleza mahitaji ya watu.”
“Serikali zitakazojibu haraka, ndizo zitakazosalia.”