Tabora. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia mtu mmoja kati ya watuhumiwa sita wanaodaiwa kulivamia lori la mizigo lililokuwa likitoka Afrika Kusini kuelekea mkoani Arusha, baada ya tukio lililotokea katika moja ya pori mkoani humo.

Mtuhumiwa huyo anaendelea kupatiwa matibabu, kufuatia majeraha aliyoyapata wakati wa majibizano ya risasi kati ya majambazi hao na Jeshi la Polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Desemba 30, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema lori hilo lilivamiwa na majambazi katika eneo la pori, lakini Jeshi la Polisi lilifanikiwa kudhibiti hali hiyo kwa wakati.

Ameeleza kuwa hakuna mali iliyopotea, huku watuhumiwa watano wa tukio hilo wakifanikiwa kutoroka na kuendelea kutafutwa.

Mkuu wa Mkoa amesema lengo la kuzungumza na waandishi wa habari lilikuwa ni kutoa taarifa kuhusu hali ya ulinzi na usalama mkoani Tabora, pamoja na kukumbusha baadhi ya matukio makubwa ya kiusalama yaliyotokea mkoani humo katika mwaka 2025.

 β€œWatu hawa tunaweza kuwaita watekaji wa magari usiku yaani zile tabia za miaka ya nyuma ndiyo wanataka kuleta hapa, lakini jeshi letu liko imara na limeweza kupambana nao na mmoja amepigwa risasi ya mguu limemkamata tunaye tayari,” amesema.

Amesema tukio hilo halitaruhusiwa kujirudia tena katika Mkoa wa Tabora na haiwezekani kuruhusu wananchi wasumbuliwe waogope kutoka usiku kwenda kwenye kazi zao kwa sababu ya kuhofia usiku, Tabora haitakiwi matendo ya namna hiyo kabisa na sio utamaduni wake.

Waandishi wa habari wakisikiliza taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha ofisini kwake

Katika matukio mengine amesema kwa mwaka 2025 lipo tukio la kushtusha la kulawitiwa mtoto wa darasa la pili katika shule binafsi iliyopo Kata ya Mtendeni Manispaa ya Tabora mwenye umri wa miaka saba, ambapo alilawitiwa na mwalimu wake katika vyoo vya shule hiyo.

β€œMwalimu huyu tulimkamata tukamchukulia hatua ili kukomesha matukio ya aina hiyo mkoani Tabora ambapo mtoto huyo mwenye jinsia ya kiume na kumuharibu maumbile yake,” ameongeza.

Mwaka 2025, Mkoa wa Tabora ulishuhudia tukio la kushangaza baada ya mwanamke mmoja, Hadija Jimmy (39), mkazi wa Manispaa ya Tabora, kudaiwa kujiteka mwenyewe kwa lengo la kumshawishi mume wake amtumie fedha za matumizi.

Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, ilibainika kuwa mwanamke huyo alijificha wilayani Urambo, ambako alidaiwa kuwa akiishi kwa nyakati tofauti na wanaume watatu.

Amesema akiwa huko, alikuwa akimpigia simu mume wake na kudai ametekwa, akimtaka atume fedha ili aachiwe huru.

Hata hivyo, uchunguzi wa vyombo vya usalama ulibaini kuwa hakukuwa na tukio la utekaji, na kwamba fedha zilizokuwa zikitumwa zilidaiwa kutumiwa na mwanamke huyo kwa matumizi binafsi na starehe.

Tukio hilo limeendelea kutajwa kama miongoni mwa matukio yaliyoibua mshangao mkubwa mkoani Tabora katika mwaka 2025, na lilisababisha vyombo vya usalama kuchukua hatua za kisheria dhidi ya muhusika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *