Miundombinu iliyoathiriwa kwa mvua yaanza kurekebishwaMiundombinu iliyoathiriwa kwa mvua yaanza kurekebishwa

SERIKALI imeanza kurekebisha miundombinu iliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha ili kuhakikisha usalama wa wananchi na miundombinu inarejea katika hali yake ya awali.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Uchukuzi iliwataka wananchi kuwa wavumilivu wakati kazi za urejeshaji wa huduma zikiendelea.

Aidha, serikali imewasihi wananchi wote kuchukua tahadhari kwa kutosafiri katika maeneo yaliyoathiriwa pale inapowezekana pamoja na kuzingatia maelekezo ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka za usafiri.

Pia, imewataka wananchi kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na serikali na vyombo husika pamoja na kuepuka kusogea karibu na miundombinu ya reli na barabara zilizoathiriwa ili kuepuka ajali.

“Kutokana na tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwepo wa mvua kubwa zinazoambatana na upepo mkali katika maeneo mbalimbali nchini, mvua hizo zimeanza kusababisha athari katika madaraja ya reli ya zamani (MGR) katika maeneo ya Kidete, Wilaya ya Kilosa – Mkoa wa Morogoro na Gulwe, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma,” ilisema taarifa hiyo.

Sambamba na hayo, taarifa hiyo ilieleza kuwa kumekuwepo na hitilafu za umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na umeme wa Reli ya Kisasa (SGR), hali iliyoathiri uendeshaji wa huduma za reli.

Vilevile, ilisema Barabara Kuu ya Morogoro – Iringa, imeathirika pia hususani eneo la Mama Marashi – Mikumi, lililoathirika na maporomoko ya mawe pamoja na mkusanyiko wa tope barabarani, jambo linalohatarisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo.

Hivi karibuni Shirika la Reli Tanzania (TRC), liliripoti kutokea kwa changamoto ya kiuendeshaji katika Kituo cha Ruvu na kusababisha usafiri wa treni kukwama kwa saa tano.

Hata hivyo, Msemaji wa TRC, Fred Mwanjala aliliambia HabariLEO kwamba pamoja na hitilafu hizo shughuli za usafiri za SGR zilirejea kama kawaida kuanzia saa 7:00 mchana siku ya Jumapili baada ya wataalamu wa shirika hilo kushughulikia changamoto hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, mvua hizo zilizoambatana na upepo mkali kuanzia usiku wa kuamkia jana zimesababisha hitilafu katika mfumo wa umeme wa SGR na umeme wa Tanesco, hali iliyoathiri kwa kiasi kikubwa usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *