Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Gervas Kasiga, amesema kuelekea mwaka 2026, wamejipanga madhubuti kuendelea kusimamia maadili ya wanatasnia hapa nchini.

Akizungumza na Mwananchi, Kasiga amesema wao kama bodi watahakikisha wanaongeza uelewa kwa wanatasnia wa maigizo kuhusu maadili katika kuandaa kazi zao.

“Kuelekea 2026 tutahakikisha kunakuwa na ongezeko kubwa la uelewa kwa wanatasnia kuhusu maadili katika kuandaa kazi na maisha yao binafsi kwasababu wao ni sehemu ya viongozi, tutalifanya kwa kuhakikisha wanapatiwa elimu kupitia makongamano na matamasha mbalimbali,” amesema.

Ameongezea kuwa, Bodi ya Filamu Tanzania itaendelea kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa kazi za wasanii wa maigizo mitandaoni.

“Tutaendelea na zoezi la kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa kazi za wasanii kwa maudhui yao mtandaoni na majukwaa ya kawaida, mitandao kama YouTube, Instagram, TikTok na Facebook kwasababu huwa tunapita kote huko kuhakiki hayo maudhui na kuhakikisha kwamba maadili yanaendelea kusimamiwa,” amesema Kasiga.

Amesema mara nyingi wamekuwa wakishusha kazi za wasanii na sio lazima wengine waitwe ofisini bali huhitajika kushusha maudhui ambayo yapo kinyume na maadili ya Mtanzania.

“Mara nyingi watu wengi hawajui ila tumekuwa tukishusha kazi nyingi za mtandaoni sio lazima wengine tuwaite, tunawaambia wanatasnia kuwa hiyo haifai shusha kwasababu ya kulinda taswira zao na nchi yetu ya Tanzania.

“Kuna wasanii kama 20 hivi tutawaita kwa pamoja na kuwapa mafunzo, baada ya hapo kama wataenda kinyume na yale ambayo tumeyafundisha tutaanza kuchukua hatua kali dhidi yao, lakini pia tutakuwa na kampeni maalum kwaajili ya uwajibikaji na maadili kwa wanatasnia,” amesema Kasiga.

Amesema Bodi ya Filamu imepewa jukumu la kusimamia sanaa hiyo ikue bila kuharibu maadili na utu wa Mtanzania.

“Tumepewa jukumu la kuisimamia filamu sio tu ikue bali iwe na maadili bora na utu katika kazi za wanatasnia zinazooneshwa kwenye Tv na mitandaoni,” amesema Kasiga.

Aidha amesema wataendelea kufanyakazi kwa ukaribu na taasisi zingine kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na wamiliki wa mitandao ya kijamii ili kuwabaini na kuwawajibisha wanaoenda kinyume na kanuni za bodi hiyo.

“Tutaendelea kufanyakazi kwa ukaribu na Shirikisho la Filamu Tanzania ambalo lipo chini ya bodi ya filamu, na kwa wasanii watakao kuwa wamekiuka maadili tutawaita na kama onyo halitatosha watafungiwa kujihusisha na filamu kwa mujibu wa sheria japo hili sitamani litokee kwahiyo ninawasii wanatasnia mwaka 2026 na miaka ijayo tuendelee kufanyakazi ambazo zipo ndani ya maadili.

“Tutaongeza ushirikiano na taasisi nyingine kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) lakini pia na vyama vya wasanii na wamiliki wa mitandao ya kijamii mfano Meta ili watusaidie na kuhakikisha sheria zinafuatwa katika sanaa ya maigizo hapa nchini,” amesema Kasiga.

Mwisho amesema watahamasisha wanatasnia kujikita katika kuandaa maudhui bora yanayolenga kukuza utamaduni wa Mtanzania.

“Tutahamasisha jamii kuandaa maudhui bora yanayolenga kukuza utamaduni wetu kama mila na desturi na tajiriba ambazo kwa uhakika tukiongeza maarifa na taaluma zitasaidia sana kutangaza nchi yetu kuongeza kipato na kujitangaza duniani kuwa sisi ni watu wa namna gani,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *