MWAKA 2025 umekuwa na huzuni kubwa kwa Tanzania baada ya kupoteza baadhi ya viongozi wake wakuu waliochangia kwa kiasi kikubwa katika siasa, uongozi na maendeleo ya taifa. Vifo vyao vimewaacha Watanzania wengi huzuni.
Miongoni mwa viongozi maarufu waliofariki ni Cleopa David Msuya, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Makamu wa Kwanza wa Rais. Msuya alizaliwa mwaka 1931 na alihudumu kama Waziri Mkuu katika nyakati mbili tofauti kuanzia 1980 hadi 1983 na 1994 hadi 1995.
Pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini. Msuya alifariki dunia 7 Mei 2025 akiwa na umri wa miaka 94 Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam. Mazishi yake yalihudhuriwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine wakuu wa taifa, huku wananchi wakimkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika siasa na uongozi wa Tanzania.

Tanzania pia ilimpoteza Juma Volter Mwapachu, aliyefariki 28 Machi 2025 akiwa na umri wa miaka 82. Mwapachu aliheshimiwa kwa nafasi yake kama Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo aliiongoza Jumuiya hiyo kuanzia 2006 hadi 2011.
Mbali na kazi yake ya kimataifa, alihudumu kama balozi wa Tanzania, mjumbe wa kudumu wa UNESCO, na mratibu wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Kifo chake kilisikitisha viongozi wa EAC na wananchi wa Tanzania. SOMA: Rais Samia aongoza Watanzania maziko ya Cleopa Msuya

Agosti 6 mwaka huu, Tanzania ilimpoteza Job Yustino Ndugai, aliyewahi kuwa Spika wa Bunge wa Tanzania. Ndugai alihudumu kama Mbunge wa Kongwa kwa zaidi ya miongo miwili na pia alikuwa Naibu Spika kabla ya kuchaguliwa kuwa Spika.
Alijulikana kwa uelewa wake wa masuala ya sheria na katiba, na alichangia kuimarisha majadiliano ya kisiasa ndani ya Bunge. Mazishi yake yalifanyika Agosti 11, 2025 Dodoma, ambapo viongozi wa serikali na wananchi walimkumbuka kwa heshima kubwa.
Kiongozi mwingine Abbas Ali Mwinyi aliyefariki 25 Septemba 2025 akiwa Unguja. Abbas alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Fuoni ni ndugu wa Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi. Kifo chake kilisababisha huzuni kubwa ndani ya familia na katika siasa za Zanzibar. Mazishi yake yalihudhuriwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine wakuu wa nchi.

Desemba Tanzania ilipata pigo jingine kumpoteza Jenista Mhagama aliyefariki dunia Desemba 11, 2025,katika kipindi cha uhai wake Jenista alikuwa Mbunge wa Peramiho na Waziri katika wizara mbalimbali. Mhagama alihudumu katika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Waziri wa Afya, Waziri Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu akihusika na sera, Bunge, ajira, vijana na watu wenye ulemavu.
Kifo chake kilisikitisha Watanzania wengi, na Rais Samia Suluhu Hassan alimtaja kama kiongozi aliyethubutu na mwenye kujitolea kwa wananchi. Mazishi yake yalifanyika Desemba 16, 2025 katika kijiji cha Ruanda, mkoani Ruvuma, huku maelfu ya wananchi, viongozi wa serikali na wanasiasa wakihudhuria kumuaga.
Viongozi hawa wote walitumikia taifa hili kwa njia mbalimbali wakiwa kama wanasiasa, wabunge, watendaji serikalini na viongozi wa kanda. Vifo vyao vimeacha pengo kubwa katika uongozi wa taifa na vimeibua mijadala juu ya urithi wao kwa vizazi vijavyo na maendeleo ya Taifa.
