MAMLAKA ya Vitambulisho ya Taifa (NIDA) imezindua namba ya kutuma ujumbe mfupi wa kufahamu namba ya utambulisho ya mwombaji wa kitambulisho itakayowezesha wananchi kufahamu namba zao za vitambulisho bila kufika ofisini na kupunguza msongamano wa kupata vitambulisho vya taifa.
Imesema namba hiyo itawezesha waombaji wa vitambulisho hivyo kufuatilia hali ya maombi yao hatua kwa hatua na kuondoa gharama za usafiri na usumbufu wa kufika ofisini kufuata huduma.
NIDA kwa kushirikiana na mitandao ya simu imeanzisha namba ya bure ya kutuma ujumbe mfupi wa maandishi ya 15274 itakayorahisisha kufahamu namba ya utambulisho kwa wananchi na kupata taarifa za maombi ya kitambulisho.
SOMA: NIDA yaita makundi manne kubadili taarifa
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene alisema kupitia namba hiyo waombaji watafahamu hatua za maombi yao na kuwezesha mamlaka hiyo kupunguza mlundikano wa vitambulisho ambavyo havijachukuliwa.
“Hatua hii inaenda kutatua matatizo ya muda mrefu. Hivi leo (jana) katika wilaya zetu kuna vitambulisho vingi havijachukuliwa kwa sababu waombaji wengi hawajui hatua za uombaji, kupitia mfumo huu sasa utajibiwa,” alisema Simbachawene.
Alisema faida nyingine ni kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa waombaji, kupunguza gharama na muda wa kufuata huduma ofisini na kupunguza foleni.
Simbachawene ameiagiza mamlaka hiyo kuhakikisha hadi Februari mwakani wawe wameshatoa vitambulisho kwa wananchi walioomba.
Alisema mamlaka hiyo imeendelea kuboresha huduma kwa ufanisi na kuendana na kasi ya ukuaji sayansi na teknolojia katika utoaji wa huduma, ikitoa huduma kwa haraka, urahisi bila malipo, akisisitiza kuwa lengo la serikali ni kuwa na kitambulisho kimoja kwa matumizi tofauti.
“Mwelekeo wetu sasa hata baada ya masahihisho (ya vitambulisho vilivyofutika) ni kwenda kwenye kitambulisho kimoja kwenye matumizi mengi, tunataka mtu asibebe vitambulisho vingi; kiwe kimoja, kitumike kurahisisha huduma,” alieleza Simbachawene.
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji alisema mamlaka hiyo imeunda mifumo 120 ya utoaji huduma kwa wateja iliyosaidia kuokoa gharama za kiuendeshaji kwa taasisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Kaji alisema namba hiyo itapunguza mlundikano na msongamano wa wananchi katika ofisi za wilaya kwani wananchi wengi hawajapata vitambulisho vyao licha ya NIDA kuvipeleka hadi ngazi ya kata.
“Namba hii itaweza kumrahisishia mtu kuweza kufahamu na kutambua namba yake ya utambulisho, endapo mwananchi hajui au amesahau namba yake utambulisho wa taifa kwa kuandika ujumbe mfupi kwa simu ya mkononi kwenda 15274,” alieleza Kaji.
