Dar es Salaam. Kiungo wa Singida Black Stars anayekipiga Pamba Jiji kwa mkopo, Kelvin Nashon ni miongoni mwa nyota 28 walioitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachoshiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo yanaendelea kutimua vumbi huko Morocco.
Kocha wa Taifa Stars Miguel Gamondi, leo Jumanne Desemba 30, 2025 atakiongoza kikosi chake kitakachokuwa kinatupa karata yake ya tatu dhidi ya Tunisia katika mashindano hayo ambapo Nashon naye atakuwa ni miongoni mwa nyota wa Stars watakaokuwa katika sehemu ya kikosi hicho ambacho kitakuwa kikitafuta ushindi wake wa kwanza tangu kianze kushiriki katika mashindano hayo mwaka 1980 kule Nigeria, ikafuatia 2019 Misri, kisha 2023 (ilifanyika 2024) kule Ivory Coast na sasa 2026 Morocco.
Nashon mwenye umri wa miaka 25, historia yake ya soka ilianzia jijini mwanza katika mashindano ya Airtel Rising Star mwaka 2013 kisha akaitumikia timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys ambayo kwa wakati huo ilifanya makubwa ilipokuwa na nyota wengine wanaowika hivi sasa kama Dickson Job, Nickson Kibabage, Kelvin John, Kibwana Shomari pamoja na Abdul Suleiman maarufu kama Sopu anayekipiga Azam FC.
Baada ya hapo kiungo huyo alipita JKT Tanzania ambako hakupata nafasi ya kutosha kuonyesha zaidi kiwango chake ndipo akajiunga na Geita Gold FC ambayo aliitumikia kwa kipindi cha miaka miwili kisha akajiunga na Singida Black Stars mwaka 2022 ambayo yupo hadi sasa.
Kiungo huyo mkabaji alipelekwa kwa mkopo kujiunga na timu ya Pamba Jiji ya Mwanza kutokana na ushindani mkubwa wa namba uliokuepo Singida BS baada ya usajili wa dirisha kubwa. Kocha, Gamondi aliyemjumuisha kwenye kikosi cha Taifa Stars ndiye aliyemtoa kwa mkopo kwenda Pamba Jiji, bila shaka Muargentina huyo ameridhika na kiwango alichokionyesha Nashon katika michezo tisa ya Ligi Kuu ambayo amecheza akiwa na wababe hao wa Mwanza.
Hadi sasa Nashon, amechangia Pamba Jiji kupata ushindi mara nne, sare nne na kupoteza mechi moja katika mechi tisa ilizocheza kwenye Ligi Kuu huku ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 16 sawa na Yanga inayoshika nafasi ya pili. Nashon ameonyesha ukomavu mkubwa katika kikosi hicho kinachonorewa na kocha, Francis Baraza ambapo hadi sasa amepachika bao moja ndani ya kikosi hicho ambacho kimefunga jumla ya mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.
Vigogo wa Kariakoo walimtaka
Alipokuwa Geita Gold, Nashon aliwahi kuhitajika na Wekundu wa Msimbazi, Simba lakini dili hilo liligonga mwamba baada ya Simba kuchelewesha malipo ya kumchukua kiungo huyo na ndipo Singida Black Stars ikaingilia kati na kumnasa.
Mmoja kati ya watu wa karibu na Nashon aliyehusika kwenye kukamilisha dili hilo la kutua Singida alisema kuwa, Nashon na Simba walimalizana kila kitu ikabaki kuingiziwa pesa kwenye akaunti yake tu ili amwage wino wa kuwatumikia Wana Msimbazi hao lakini vigogo hao wa Kariakoo wakachelewesha malipo hayo ndipo Singida ikamchukua kiulaini.
Nashon tayari alikuwa ameshaaga Geita na kuwaambia baadhi ya wachezaji wenzake anaenda Simba lakini Singida ikagundua kinachosubiriwa ni pesa kuingia kwenye akaunti ndio ikatumia nafasi hiyo na kummwagia mkwanja mrefu kisha akasaini.
“Nashon mwanzoni alijua anakwenda Simba, lakini walichelewa kumuingizia pesa na muda huohuo akiwa hajatulia ndipo Singida ikaja na pesa keshi na kumchukua,” kilieleza chanzo hicho na kuongeza;
“Siyo kwamba pesa ya Singida ni kubwa kuliko ile ya Simba, lakini mchezaji mwenyewe amecheza na muda kwani ukute wangemwambia wanamwekea pesa na wasiweke hadi dirisha la usajili linafungwa na akawa amekosa vyote.”
Sababu nyingine ambazo zilipenyezwa ni kuwa, Nashon ameogopa kuchezea fursa kama ilivyokuwa misimu miwili nyuma akiwa JKT Tanzania ambapo alipata ofa kibao ikiwamo ya Azam FC na Namungo za mkwanja mrefu lakini aligoma kujiunga nao kwani JKT ilikuwa imemuahidi ajira ya Jeshi na baadaye akakosa vyote.
Akizungumzia jambo hilo katika kipindi cha nyuma, Nashon ambaye anatajwa kati ya viungo bora hapa nchini alikiri kuongea kila kitu na Simba lakini aliamua kujiunga na Singida kwakuwa ndiyo iliyokuwa makini zaidi.
“Simba niliongea nao na tukafika sehemu nzuri lakini wakawa kama wanasita kuweka pesa, Singida wamekuja mara moja na tukamaliza kila kitu,” alisema fundi huyo wa Taifa Stars na kuongeza;
“Nafurahia hapa, naamini ni sehemu salama kwangu na kwa kiwango changu na kwa kushirikiana na wenzangu nimejipanga kuisaidia timu kufikia malengo.”
Yanga nao wamo
Yanga ilituma ofa ya kumtaka Nashon kwa mkopo katika dilisha dogo la usajili la mwezi Januari na mambo yalikwenda vizuri, lakini ghafla hakukamilisha dili na baadaye aliibuka beki Israel Mwenda wa klabu hiyo kujiunga na Mbingwa hao wa Ligi Kuu kwa mkopo.
Katika kulizungumzia hilo, Nashon alisema sababu kubwa ya dili kukwama Yanga ni kutokana na kutocheza mara kwa mara, na Yanga ilikuwa inahitaji mchezaji ambaye ataingia moja kwa moja kikosini kuonyesha ushindani.
“Ni kweli dili la kujiunga na Yanga limekufa, sitaweza kucheza tena sababu kubwa ni viongozi kuogopa kunipa presha ya kuwapa kile walichokuwa wanatarajia na ukizingatia kipindi wananihitaji timu ilikuwa kwenye presha ya kukosa matokeo, hivyo walihitaji mchezaji ambaye atawapa matokeo ya ubora moja kwa moja,” alisema mchezaji huyo.
“Baada ya kufika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumalizana na Yanga ili niweze kusaini mkataba ndipo nilipokutana na viongozi kuniambia kuwa wananiamini, lakini sijacheza muda wanahofia kuniongeza kikosini nitashindwa kuwapa kitu kizuri kwa uharaka, hawataki mtu wa majaribio.”
Nashon alisema viongozi wanaamini katika uwezo wake, lakini hawataki kumuingizia presha ambayo itamtoa mchezoni, kitu ambacho kama mchezaji alikubali na kukipokea licha ya kujiamini kuwa ni mshindani, hivyo ameona bora ajitafute kwanza.
Akizungumzia sababu ya kukosa nafasi, alisema changamoto ni ongezeko la wachezaji na benchi la ufundi jipya ndivyo vitu vilivyomtoa mchezoni huku akikiri pia kuwa maingizo mapya yalikuwa na nyota wengi wazoefu na nafasi yake anayocheza imejaa mastaa wengi wa kigeni.
Nashon ambaye nje ya soka anapenda kusikiliza muziki wa Hip Hop na Bongo Fleva aliwahi kusema kwamba ndoto yake ni kufikia kiwango cha juu zaidi ili kuisaidia timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ jambo ambalo limeonekana kutimia baada ya kujumuhishwa kwenye kikosi hicho kinachocheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu nchini Morocco.
“Wakati ambao sijaitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, huwa nashukuru Mungu kwa sababu nakuwa najiona kama nahitaji kuongeza bidii ili siku nikiitwa, wale ambao hawajaitwa waone kama nimestahili kuitwa timu ya Taifa,” alisema Nashon.
Kwa sasa kiungo huyo yupo na kikosi cha Stars huko Morocco kinachojiandaa na michezo miwili iliyobakia ya kundi C ambapo leo Jumatatu , Desemba 27, 2025, Stars itashuka kwenye Uwanja wa El Barid katika mchezo wa pili kuvaana na majirani zetu Uganda kabla ya kukutana na Tunisia, Desemba 30 katika mchezo wa mwisho