Ripoti mpya inaonyesha kwamba mawimbi ya joto yaliyovunja rekodi, vimbunga vya kitropiki na mvua zilizosababisha mafuriko makubwa kote duniani, vimeufanya mwaka unaomalizika wa 2025 kuwa moja ya miaka yenye hasara kubwa zaidi kwa majanga ya hali ya hewa, huku hasara za kiuchumi zikikadiriwa kuwa karibu dola bilioni 120.

Ripoti hiyo, iliyotolewa na Christian Aid, imetokana na makadirio ya hasara yaliyotolewa na kampuni ya bima ya Aon, na ina orodha ya majanga 10 ya asili yanayojumuisha moto wa nyikani, vimbunga, mvua kubwa na mafuriko na ukame ulioenea katika mabara manne. Majanga haya kwa pamoja yalisababisha hasara ya kiuchumi ya dola bilioni 120.

Moto wa nyikani wa Los Angeles uliozuka Januari mwaka huu umeongoza orodha ya majanga, huku vifo 31 vya moja kwa moja vikirekodiwa; lakini utafiti mwingine uliofanywa Agosti ulionyesha kuwa watu 400 zaidi waliaga dunia kutokana na mambo yanayohusiana na moto huo, ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa hewa na kuchelewa kupata huduma za afya.

Watu 200 walifariki dunia kwa janga la mafuriko Nigeria, Juni 2025

Watafiti wanasema kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yalizidisha matukio ya moto, ambao ulisababisha hasara ya zaidi ya dola bilioni 60. Wanasayansi pia wamehusisha mabadiliko ya hali ya hewa na vimbunga vikali na mafuriko yaliyoua zaidi ya watu 1,800 katika nchi kadhaa Kusini na Kusini-Mashariki mwa Asia, mwishoni mwa mwezi Novemba.

Mafuriko hayo yaliyosababishwa na vimbunga viwili vya kitropiki vilivyolikumba eneo la Sumatra la Indonesia na rasi ya Malaysia kwa wakati mmoja, yalisababisha hasara ya takriban dola bilioni 25, na kulifanya janga la pili lenye hasara kubwa zaidi la hali ya hewa.

Orodha hiyo pia imejumuisha mafuriko yaliyotokea nchini China, India, Pakistan na Texas, pamoja na vimbunga vinne vya kitropiki, ambavyo chenye hasara kubwa zaidi kilikuwa Kimbunga Melissa katika eneo la Karibiani.

Ripoti ya Christian Aid haikuzingatia katika uchambuzi wake hasara ambazo ni vigumu kuzipima kwa usahihi, kama vile uharibifu wa vyanzo vya riziki, kupoteza pato, uharibifu wa mazingira wa muda mrefu na kuhama daima kwa jamii za watu. Shirika hilo limesema kwamba “hasara halisi zilizosababishwa na majanga mwaka huu wa 2025 ni kubwa zaidi kuliko hasara zilizo na bima.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *