Hatua ya utawala vamizi wa Israel ya kulitambua rasmi eneo la ‘Somaliland, ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili.imekabiliwa na radiamali kali ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeitisha mkutano huo wa dharura ikiitikia ombi la Mwakilishi wa Kudumu wa Somalia katika jumuiya hiyo kama sehemu ya juhudi za pamoja za nchi za Kiarabu za kushughulikia kile ambacho serikali ya Somalia inasema ni hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa iliyochukuliwa na Israel, inayokiuka wazi mamlaka ya kujitawala ya Somalia na umoja wa ardhi ya nchi hiyo.

Taarifa ya Jumuiya ya Kiarabu sambamba na kulaani hatua yoyote ya kurahisisha kuhamishwa kwa nguvu wa watu wa Palestina, nchi za Kiarabu zinasisitiza kwamba eneo la kaskazini magharibi mwa Somalia ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na Jamhuri ya Shirikisho ya Somalia, na kwamba kutambua rasmi eneo hilo kama linalojitawala ni sehemu ya njama chafu za utawala wa Israel za kuvuruga usalama na amani duniani.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepanga kuitisha mkutano wiki hii kujadili matokeo ya hatua ya Israel ya kulitambua rasmi eneo la ‘Somaliland, ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili. Kikao hicho kitafanyika kufuatia ombi la Somalia.

Abdul-Malik al-Houthi kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen

Abdul-Malik al-Houthi kiongozi wa harakati ya Ansarullah amelaani vikali hatua ya Israel ya kuitambua rasmi Somaliland kama taifa huru na kutoa mwito kwa nchi za Kiarabu na Kiislamu kuiunga mkono mamlaka ya kujitawala ya Somalia, akihimiza kuzidisha mashinikizo kwa washirika huko Somaliland na kuchukua misimamo imara katika taasisi za kimataifa. 

Upinzani wa jamii ya kimataifa dhidi ya mpango wa utawala wa Kizayuni wa kuitambua Somaliland una sababu mbalimbali za kisiasa, kijiografia, na kiusalama. Nchi za Kiarabu na Kiislamu zinaona hatua hii kama sehemu ya mradi wa utawala wa Kizayuni wa kuyumbisha uthabiti katika eneo hilo na kusababisha ukosefu wa usalama katika eneo la Pembe ya Afrika.

Somaliland ina umuhimu mkubwa wa kimkakati kutokana na eneo lake la kipekee la kijiografia katika Pembe ya Afrika. Eneo hilo liko kaskazini magharibi mwa Somalia na lina ufikiaji wa Bahari Nyekundu, ambayo ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za nishati na biashara duniani.

Lango Bahari la Bab Al–Mandab ni njia muhimu kati ya Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden, na uwepo wowote wa kijeshi huko Somaliland unaweza kuathiri usalama wa njia hii. Somaliland pia ina mipaka na Djibouti, Ethiopia, na Yemen, na kuifanya kuwa nukta ya kuiunganishi kati ya Afrika na Asia Magharibi.

Hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuitambua Somaliland inamaanisha kudhoofisha mamlaka ya kitaifa ya Somalia na kusababisha ukosefu wa usalama na utulivu katika Pembe ya Afrika. Hatua hii inaweza kuwa mfano hatari wa kudhoofisha umoja wa ardhi wa nchi zingine.

Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 kufuatia vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe lakini haijawahi kutambuliwa rasmi na nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Jamhuri hiyo iliyotangaza kujitenga na Somalia imeanzisha sarafu yake, bendera na bunge, ingawa maeneo yake ya mashariki yameathiriwa na mzozo.

Kieneo pia Umoja wa Afrika (AU) umepinga vikali jaribio lolote la kutambua eneo lililojitenga la Somaliland kama taifa huru, ukisisitiza tena dhamira yake thabiti ya kulinda umoja, mamlaka na mipaka ya ardhi ya Somalia.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imevunja ukimya wake kuhusu hali ya mvutano unaoendelea nchini Somalia na Somaliland, na kuthibitisha uungaji mkono wake kwa Somalia.

Jumuiya ya Afrika Mashariki imesema kuwa, inaunga mkono kikamilifu nmamlaka ya nkujitawala Somalia kufuatia hatua ya Israel ya kulitambua rasmi eneo la ‘Somaliland, ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili.

Ripoti zinaeleza kuwa Israel inapanga kujenga kituo cha kijeshi katika Somaliland, hatua ambayo itaiwezesha kudhibiti eneo muhimu la kistratijia la Ghuba ya Aden na kuendesha mashambulizi dhidi ya serikali ya Ansarullah nchini Yemen. Aidha utawala wa Israel unalenga kutekeleza mpango wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka Gaza hadi Somaliland ikiwa ni katika fremu ya sera zake za maangamizi ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *