
RABAT, MOROCCO: TAIFA Stars imekaza msuli na kutoka sare ya bao 1-1 na Tunisia katika mchezo wa Kundi C la mashindano ya Kombe la Matiafa ya Afrika (Afcon) na hivyo timu hizo zote kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye mikikimikiki hiyo inayofanyika Morocco, Jumanne.
Katika kipute hicho kilichofanyika uwanjani Stade Olympique de Rabat, Tunisia iliyokuwa ikihitaji sare tu kutinga mtoano ilitangulia kwa bao la mkwaju wa penalti kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa Ismael Gharbi, lakini Stars ilikuwa kusawazisha dakika ya tatu tu baada ya kuanza kipindi cha pili kwa shuti la nje ya boksi la Feisal ‘Feitoto’ Salum baada ya pasi ya Novatus Miroshi.
Matokeo hayo yameifanya Stars kumaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi C ikiwa na pointi mbili na hivyo ikifuzu kupitia timu bora ya tatu, ikishika namba nne kwenye msimamo huo na hivyo kutinga hatua ya 16 bora ya mikikimikiki ya Afcon 2025 ikiiondoa Angola kwa mabao ya kufunga baada ya kulingana kwenye tofauti ya mabao, zote zikiwa na -1.
Na sasa Stars itakabiliwa na mechi ngumu ya kuwakabili wenyeji Morocco katika mechi hiyo ya mtoano, itakayopigwa Jumapili huko Rabat.
Kuhusu mchezo wa usiku wa Jumanne, mfungaji wa bao la penalti la Tunisia, Gharbi nusura afunge kabla ya mkwaju huo baada ya shuti lake kugonga kugonga mwamba wakati kipa Hussein Masalanga aliporuka bila ya mafanikio.
Mkwaju huo wa penalti ulitolewa na VAR baada ya mwamuzi Jean Jacques Ndala Ngambo kuamriwa kwenda kuangalia kwenye skrini ya pembeni mwa uwanja tukio la beki Ibrahim Hamad kumzuia kwa kumshika mchezaji Hazem Mastouri, aliyekuwa akikimbilia mpira wa adhabu wa Hannibal Mejbri ndani ya boksi la Stars.
Lakini, Stars ilitambua wazi sare ingeweza kuwavusha hatua inayofuata, hivyo walipambana na kufanikiwa kusawazisha, ikipata sare ya pili kwenye katika mechi tatu ilizocheza Kundi C.
Stars ilianza kwa kufungwa 2-1 na Nigeria, kabla ya kufungana 1-1 na Uganda katika mechi ya pili na kumalizia sare hiyo ya 1-1 kwa Tunisia na kutinga mtoano.
Tunisia kwa kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi C, itamenyana na washindi wa pili kwenye Kundi A ambao ni Mali, ambapo kipute hicho kitafanyika Jumamosi, Januari 3 huko Casablanca na Tanzania itacheza na Morocco mjini Rabat dhidi ya Morocco, Jumapili, Januari 4, 2026.
Katika mchezo mwingine wa Kundi C, Uganda ilikubaki kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Nigeria na hivyo kusukumwa nje ya michuano hiyo ikiishia kwenye hatua ya makundi kwa kujikusanya pointi moja katika mechi tatu.