Dodoma. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji amekabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya Sh3.25 bilioni kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kwa lengo la kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za misitu nchini.

Vitendea kazi hivyo vilivyokabidhiwa leo Jumanne, Desemba 30, 2025 katika makao makuu ya TFS jijini Dodoma ni pamoja na magari 33 ya shughuli za misituni, pikipiki 36 na ndege nyuki (drone) tatu za kisasa zenye uwezo wa kuruka umbali wa hadi kilomita 20 na kufikia kimo cha mita 5,000 juu ya usawa wa bahari. Ndege hizo zitasaidia katika ulinzi na upimaji wa mipaka ya hifadhi za misitu nchini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dk Kijaji amesema takribani theluthi moja ya eneo la Tanzania limetengwa kwa ajili ya hifadhi mbalimbali ikiwamo hifadhi za taifa, misitu na mapori, hivyo kuna umuhimu wa taasisi zinazohusika kupewa vifaa stahiki ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

 β€œTumeona TFS ikiendelea kuanzisha misitu katika maeneo mbalimbali na kuitunza ile iliyopo ndani ya halmashauri kwa kushirikiana na wadau wengine. Lengo ni kuhakikisha Taifa letu linaendelea kuwa la kijani na wananchi wanufaike na rasilimali hizi,” amesema Dk Kijaji.

Ameongeza kuwa vitendea kazi hivyo vitasambazwa katika kanda zote saba za TFS nchini ili kuhakikisha huduma zinafika kwa wananchi popote walipo, huku uhifadhi wa misitu ukiimarishwa kwa kuzingatia utu na masilahi ya jamii.

Dk Kijaji pia amebainisha kuwa moja ya mipango mikubwa ya TFS kwa mwaka wa fedha unaoendelea ni kuifanya Dodoma kuwa ya kijani kwa kupanda miti na kuanzisha misitu kwenye vilima vyote vilivyopo ndani ya jiji hilo, kabla ya mpango huo kusambazwa katika mikoa mingine nchini.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo amesema vitendea kazi vilivyopokelewa vitaiwezesha taasisi hiyo kufika katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa magumu kufikika kutokana na changamoto za miundombinu.

Amesema magari yaliyokabidhiwa yamekusudiwa kutumika kwenye shughuli za misituni katika maeneo ambayo magari ya kawaida hayawezi kupita, huku pikipiki zikitumika pale ambako hakuna njia kabisa, ili kuhakikisha maeneo yote ya hifadhi yanalindwa ipasavyo.

β€œHata hizi ndege nyuki tulizopata ni za kisasa sana. Zina uwezo wa kuruka umbali wa kilomita 20 na kufikia mita 5,000 juu ya usawa wa bahari. Zitatusaidia kuimarisha ulinzi, tofauti na zile za awali ambazo zilikuwa na uwezo wa kilomita tatu pekee na kushindwa kufikia baadhi ya maeneo, hususan vilele vya milima mirefu,” amesema Profesa Silayo.

Naye Mhifadhi wa TFS, Ally Msuya, amesema ndege nyuki hizo zina teknolojia ya kisasa inayowezesha kutambua maeneo yenye moto na kutoa taarifa kwa wakati, kugundua vitendo vya ujangili, pamoja na kutoa sauti zinazoweza kuwafukuza wanyamapori hatari kama tembo wanaovamia makazi ya watu na kuwarejesha kwenye hifadhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *