TISEZA yavunja rekodi, yasajili miradi ya dola bilioni 10TISEZA yavunja rekodi, yasajili miradi ya dola bilioni 10

BAGAMOYO: MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imevunja rekodi kwa kusajili jumla ya miradi 915 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 10.95 kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 29, 2025. Idadi hiyo ni ongezeko ikilinganishwa na miradi 901 iliyosajiliwa mwaka 2024.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati wa hafla ya kukabidhi hati za uwekezaji kwa wawekezaji wa eneo la Bagamoyo na kuwasilisha taarifa ya uwekezaji kwa mwaka 2025. Hafla hiyo imefanyika leo, Desemba 30, 2025, Bagamoyo mkoani Pwani.

Profesa Mkumbo amesema miradi hiyo imesajiliwa katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, ujenzi wa majengo na usafirishaji, na inatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 161,678 kwa Watanzania. Ameeleza kuwa kati ya miradi hiyo, 182 ni ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na nje, miradi 284 inamilikiwa na Watanzania, huku miradi 442 ikimilikiwa na wawekezaji wa kigeni.

Katika hafla hiyo, Profesa Mkumbo amekabidhi hati za uwekezaji kwa wawekezaji watano wa eneo la Bagamoyo. Miongoni mwao ni mwekezaji wa kiwanda cha Canal Industries kinachozalisha vifungashio vya plastiki, pamoja na kiwanda cha kuunganisha magari cha MCGA Auto kilichowekeza dola za Marekani milioni 50. Wawekezaji wengine waliokabidhiwa hati hizo ni Jaribu Cashew Production Limited, Novara Steel Global Limited na Grosso Engineering and Fabricator Limited.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa hati za uwekezaji, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilliard Teri, amesema wawekezaji waliopatiwa maeneo maalum ya uwekezaji wanapaswa kuanza kuyaendeleza ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu kukabidhiwa.

SOMA ZAIDI: Prof Mkumbo atoa maagizo TISEZA, ataka mapinduzi kiuchumi

Kwa upande wake, Profesa Mkumbo amewatahadharisha wawekezaji watakaoshindwa kutekeleza masharti hayo kuwa serikali itawanyang’anya ardhi waliyopewa bure kwa ajili ya kuanzisha viwanda.

Wakati huo huo, Profesa Mkumbo amesema Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 11 hadi nafasi ya 9 barani Afrika kwa mwaka 2025, ikiwa miongoni mwa nchi zenye mazingira bora yanayovutia uwekezaji, na hivyo kuzipiku baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.

Ameeleza kuwa kupanda kwa nafasi hiyo kunatokana na maboresho mbalimbali ikiwemo uwepo wa Kituo cha Uwekezaji Mahala Pamoja (One Stop Centre), vivutio vya kikodi kwa wawekezaji, pamoja na uwekezaji katika maeneo maalum ya kiuchumi. Amesisitiza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, Tanzania inashika nafasi ya tatu bora barani Afrika kwa kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti iliyotolewa na Africa Business Insider, Profesa Mkumbo amesema nchi zinazoongoza kwa mazingira bora ya uwekezaji barani Afrika ni Shelisheli (Seychelles), ikifuatiwa na Mauritius na Afrika Kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *