UWEKEZAJI uliofanywa na serikali katika Bandari ya Tanga umeanza kuleta tija kutokana na ongezeko la shehena za mizigo kutoka mataifa mbalimbali katika bandari hiyo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti HabariLEO kupitia vyanzo na njia mbalimbali, uboreshaji huo umefungua fursa mbalimbali za uwekezaji si tu kwa usafirishaji wa mizigo, bali pia katika sekta nyingine kama uhifadhi wamizigo, usafirishaji na sekta za viwanda.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Peter Milanzi anasema kutokana na uboresho huo, Bandari ya Tanga imevuka lengo la upokeaji wa shehena za mizigo kutoka mataifa mbalimbali kutoka tani 137,000 Oktoba hadi kufikia tani zaidi ya 200,000 Novemba 2025.
Anabainisha hayo wakati bandari hiyo ikipokea shehena ya lami ya mapipa 660 kutoka nchini Iran kwenda
Malawi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. Kwa mujibu wa Milanzi, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, Bandari ya Tanga iliwekewa lengo la kuhudumia tani milioni 1.6 sawa na wastani wa tani 137,000 kwa mwezi.

Hata hivyo, Milanzi anasema kuanzia Julai mwaka huu, kumekuwa na ongezeko la shehena na hivyo kuvuka lengo la kuhudumia watani wa tani 137,000 kwa mwezi. “Tulianza kwa tani 152,000 mwezi Julai baadaye tukafika tani 157,000 lakini kuanzia Septemba hadi Novemba tumefikisha tani 200,000 kwa mwezi,” anasema.
Anasema ongezeko la shehena hiyo ya mizigo linatokana na huduma bora zenye ufanisi sambamba na uwepo wa vifaa vya kisasa huduma ambazo zinatolewa na bandari hiyo. Milanzi anasema uboreshaji huo uliofanywa na serikali umesaidia na kuchangia kuendelea kupokea aina mbalimbali za mizigo kutokana na ufanisi wa bandari.
Hata hivyo anasema ili kuongeza ufanisi na kupunguza muda wa kuhudumia meli bandari hapo wameanza kupunguza muda wa kuhudumia shehena za mizigo katika meli kutoka siku saba hadi kufika siku tatu.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani anasema ongezeko hilo la shehena ya mizigo ni ishara ya kufunguka kwa uchumi wa mkoa huo pamoja na Uchumi wa taifa kwa ujumla. Anasema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2025, Bandari ya Tanga imepokea shehena ya mizigo ya zaidi ya tani 508,000 huku lengo likiwa kuingiza tani 420,000.
Katika kipindi kama hicho mwaka 2024 bandari hiyo ilipokea tani 333,000 hali inayoakisi wastani wa ongezeko la kati ya asilimia 35 hadi 40. Kuhusu makusanyo ya mapato, Dk Buriani anasema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2025, wamekusanya Sh bilioni 31 wakati lengo lilikuwa kukusanya Sh bilioni 20.
“Idadi ya meli imekuwa ikiongezeka kwani katika miezi mitatu, tayari bandari hii imepokea meli 53 zenye shehena ya mizigo mbalimbali ikiwemo ya vifaa vya ujenzi, magari, malighafi za viwandani zinazosafirishwa kutoka bandari hapa kwenda maeneo mbalimbali ya nchi za Afrika ya Mashiriki na SADC (Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Afrika),” anasema.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huyo, mnyororo wa thamani katika Bandari ya Tanga umeanza kuonekana na kudhihirika kutokana na wigo wa ajira kwa vijana waliopo mkoani humo na katika maeneo ya jirani.
Buriani anawataka wafanyabiashara wa mkoani Tanga na wa mikoa ya jirani kuchangamkia fursa ya ujio wa meli
za mizigo katika bandari hiyo kwa kuhakikisha zinarudi katika nchi zao zikiwa shehena ya mzigo kutoka Tanzania. “Wafanyabiashara wa katani, mazao ya viungo sambamba na kahawa, hii ni fursa kwenu kupeleka bidhaa hizo nchini Iran na maeneo mengine ulimwenguni kwani kuna uhitaji mkubwa wa bidhaa,” anasema.
Kwa upande wake, mmoja wa maofisa kutoka kampuni ya Amura inayojihusisha na uwakala wa meli, Zakaria Mohamed anasema wameridhishwa na utoaji wa huduma katika Bandari ya Tanga. “Hivi karibuni tunatarajia kuleta mzigo mwingine wa makasha 20 ambayo tutapitishia katika Bandari ya Tanga na hata sasa hivi tuna mzigo wa makasha zaidi ya 300 yanayohudumiwa na Bandari ya Tanga,” anasema Mohamed.
Anaongeza: “Kwetu sisi kampuni ya Amura tumeweza kufungua njia nzuri ya usafirishaji kwa kutumia Bandari ya Tanga kutokana na muda mfupi wa huduma katika bandari hii jambo linalotuepushia hasara zitokanazo na kukawia.” Wakala mwingine wa meli, Athuman Kimaro anasema ujio wa meli za mizigo katika Bandari ya Tanga utaongeza fursa ya kiuchumi na kufungua milango zaidi ya biashara mkoani Tanga.

meli yenye shehena ya lami kutoka Iran hivi karibuni
“Tumejipanga kuhakikisha ndani ya kila mwezi tunaleta meli tatu hadi nne kutoka nchini Iran kuja katika Bandari ya Tanga kutokana na kuimarika kwa huduma katika bandari hiyo,” anasema Kimaro. Kwa upande wao, wafanyabiashara mkoani Tanga wanasema wameanza kuona matunda ya uboreshaji wa Bandari ya Tanga katika biashara zao.
Mwenyekiti wa Masoko wa Mkoa wa Tanga, Athumani Mohamed anasema, “Kuna mwitikio mkubwa wa ufanyaji biashara kutoka na kufunguka kwa bandari yetu. Hali hiyo inatufanya tuanze kufikiria kupanua wigo wa biashara zetu kwenda maeneo mengine nje ya nchi.”
Mjasirimali Latifa Shehoza anasema uwekezaji huo ni neema kwa wajasiriamali kwani sasa wanapata uhakika wa kuuza bidhaa zao kwa haraka na kwa wakati. “Tuna kila sababu ya kuiunga mkono serikali kutokana na fursa hii kubwa uwekezaji ambayo imeweza kufika hapa mkoani Tanga kutokana na mzunguko wa kipato ambapo kwa sasa umeweza kuongezeka kwenye shughuli zetu,” anasema Shehoza.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mwanyoka anasema sasa jukumu lao ni kuhakikisha bandari hiyo inapata mizigo ya kutosha kwa kufanya uhamasishaji kwa wafanyabiashara wenzao waliopo ndani na nje ya nchi kutumia bandari hiyo.
Anasema wameanza kufanya ushawishi wa kuwavuta wafanyabiashara kuona umuhimu wa kuitumia Bandari ya Tanga kutokana na huduma bora na za haraka katika uhudumiaji mizigo.
“Jukumu letu ni kuongeza wigo wa kufanya uwekezaji kwenye viwanda vidogo vidogo ili hii bandari yetu iweze kuendelea kunufaika na fursa ya shehena za mizigo ikiwemo kurahisisha shughuli za usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya nchi,” anasema Mwanyoka.
Naye Fred Mmassy anashauri serikali kuendelea kufanya uboreshaji wa miundombinu mengine ikiwamo ya barabara sambamba na maeneo ya kuhifadhi mizigo.
“Kutokana na kufunguka kwa Bandari ya Tanga, kuna uwezekano mkubwa siku za hivi karibuni tukakumbana na changamoto ya maeneo ya kuhifadhi mizigo na foleni barabarani, hivyo serikali ione umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi kufanya uwekezaji katika maeneo hayo mapema,” anasema.