MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amezindua kampeni ya uhamasishaji wananchi kujiunga na mpango wa serikali wa Bima ya Afya kwa wote unaolenga kuwapa fursa ya matibabu wananchi bila vikwazo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizundua mpango huo jijini Arusha, DC Mkude amesema kilio cha muda mrefu cha wananchi ambao hawapo kwenye sekta rasmi ya bima kimepatiwa ufumbuzi na serikali kuweka mpango utakaojumuisha wananchi wote bila kujali hali za vipato vyao.

Amesema mageuzi hayo katika sekta ya afya yanakuja ili kuwawezesha wananchi kugharamia matibabu yao kwa njia nafuu na kuwataka watendaji wa mitaa na madiwani kuhamasisha wananchi kujiunga kwa wingi kwenye mfuko huo.

Mkude amesema kwa nyakati tofauti serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya wamefanya juhudi za kuboresha huduma za afya zikiwemo kambi za matibabu mikoa mbalimbali, ujenzi wa zahanati, vituo vya Afya, hospitali za wilaya na rufaa ambazo zimesaidia kupunguza mzigo mkubwa wa huduma za afya.
SOMA: Sheria Bima ya Afya kwa wote kuanza 2025/26
Amesema gharama za matibabu kwa wananchi walio wengi zimekua changamoto.
“Mpango huu wa Bima ya Afya kwa wote ni mkombozi kutokana unafuu wake,” amesema Mkude.

Naye Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Julius Sekeyani ameahidi kuwahimiza madiwani kutoa elimu ya mpango huo kwa wananchi wao.
“Wananchi wetu ambao hawapo kwenye utaratibu wa kawaida wa Bima ya Afya, tunatarajia wataupokea kwa furaha na kuchangia kiasi tulichoambiwa cha sh, 150,000 ambazo zitawapa matibabu kulingana na utaratibu uliowekwa na serikali. Ninaamini wananchi wenye afya njema wanaweza kujenga uchumi wa nchi yetu kikamilifu,”amesema Sekeyani.

Naye Ofisa Uanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Arusha, Miraji Kisile amesema utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote ni utekelezaji wa sheria unaowataka wananchi kwenye makundi yao kuchangia mfuko huo kupitia utaratibu maalumu.