Takwimu mpya zinaonesha kuwa zaidi ya watu 3,000 wamefariki dunia wakati wakijaribu kufika Uhispania kwa njia ya baharini katika mwaka huu 2025 unaoelekea kuisha.

Vyombo vya habari vimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, katika kipindi cha miezi 12 iliyopita yaani tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2025, zaidi ya watu 3,000 wameripotiwa kufa maji wakati walipokuwa wanajaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea katika nchi ya Ulaya ya Uhispania.

Makundi ya haki za wahamiaji yanasema kwamba ijapokuwa idadi hiyo inaonesha kupungua ikilinganshwa na mwaka jana 2024, lakini hii haina maana kwamba safari za wahamiaji hao za kukabiliana na mawimbi makali ya baharini kwa kutumia boti dhaifu, zimekuwa salama.

Kwa upande wake, shirika lisilo la kiserikali la Caminando Fronteras limetangaza kuwa, watu 3,090 wameripotiwa kufa maji kati ya mwezi Januari hadi katikati ya mwezi huu wa Disemba 2025, wakiwemo wanawake 192 na watoto wadogo 437.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uhispania nayo imetangaza kuwa, idadi ya wahamiaji waliofariki dunia mwaka huu ni chini ya waliokufa mwaka jana katika kipindi cha baina ya mwezi Januari hadi katikati ya Disemba na kusisitiza kuwa, idadi hiyo imepungua kutokana na udhibiti mkali wa mipaka, hasa nchini Mauritania, ambayo ni sehemu muhimu ya kuondokea wahamiaji wanaoelekea Uhispania. Mauritania imesaini mkataba wa uhamiaji wa euro milioni 210 kati yake na Umoja wa Ulaya ili kupunguza wimbi la wahamiaji wanaoelekea barani humo.

Lakini Human Rights Watch inaishutumu serikali ya Mauritania kwa unyanyasaji wa kimfumo dhidi ya wahamiaji, ikiwa ni pamoja na kuwakandamiza na kuwayanyasa wahamiaji hao, madai ambayo serikali ya Nouakchott inayakanusha vikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *