Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewaandikia barua mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa nchi jirani na kutaka kulaaniwa waziwazi na kwa uthabiti; bwabwaja na upayukaji wa Trump na Netanyahu akitangaza kwamba, Iran haitosita kutoa jibu kali na la kumjutisha yeyote atakayeshiriki kwenye uchokozi dhidi yake.

Katika barua yake hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema kuwa, vitisho vya rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na amemtaka kila mtu kulaani kwa uwazi na kwa uthabiti kauli hizo za kichochezi.

Jumatatu usiku, Disemba 29, na katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Donald Trump alitoa bwabwaja mpya alizozitia chumvi akisema: “Ikiwa Iran itaendelea na mpango wake wa makombora, nitaunga mkono kushambuliwa Iran. Ikiwa wataendelea na mpango wao wa nyuklia, tutashambulia mara moja.”

Katika barua yake hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia upayukaji huo wa Trump na kusema: Tishio la kutumia nguvu dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao unakataza kutoa vitisho au matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa na kuhatarisha uhuru wa kitaifa wa nchi nyingine.

Akikumbushia mashambulio ya pamoja ya kijeshi na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran yaliyoanza mwezi Juni 2025, Araghchi amesisitiza kwamba, vitisho hivyo vinaonesha nia mbaya na ya wazi ya Marekani na kwamba lawama za uchokozi wowote ule zitabebwa na yeye mwenyewe Trump.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema pia kuwa, kama Trump anataka mazungumzo na Iran basi anapaswa kumdhibiti kwanza Netanyahu. Pia amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitishwi na vita, lakini kwa vile dirisha jembamba la mazungumzo bado liko wazi, Tehran inafadhilisha mazungumzo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *