
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesisitiza upinzani wa moja kwa moja wa Tehran dhidi ya hatua yoyote ya vitisho dhidi ya ardhi, uhuru na mamlaka ya kujitawala Venezuela, akisisitiza kuwa ana imani kuwa taifa hilo la Amerika Kusini litalinda uhuru wake.
Araghchi aliyasema hayo alipozungumza kupitia mawasiliano ya video na Balozi wa Iran mjini Caracas, Ali Chegini, pamoja na wanadiplomasia walioko katika ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Venezuela.
Araghchi amesisitiza misimamo thabiti ya Iran dhidi ya vitendo vya haramu na vya mabavu dhidi ya Venezuela, akisema kwamba wananchi wa Venezuela kwa kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, watalinda uhuru na maslahi ya kitaifa ya nchi yao mkabala wa hatua zisizo halali za Marekani.
Kadhalika Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amepongeza juhudi na huduma za wanadiplomasia wa Iran na alifahamishwa kuhusu maendeleo ya hivi karibuni katika uhusiano wa pande mbili kati ya Iran na Venezuela.
Kwa upande wake, Balozi wa Iran mjini Caracas amewasilisha ripoti kuhusu hatua ambazo tayari zimechukuliwa na juhudi zinazoendelea zinazolenga kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Caracas.
Juzi Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilipuuzilia mbali madai kwamba wanadiplomasia na wafanyabiashara wa Iran wanaoondoka Venezuela, na kusisitiza kwamba ujumbe wa kidiplomasia wa Tehran katika taifa hilo la Amerika ya Latini unaendelea kufanya kazi kikamilifu.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, na mwenzake wa Venezuela, Yvan Gil Pinto walifanya mazungumzo kwa njia ya simu na kulaani uwepo wa jeshi la Marekani katika eneo la Caribbean, huku wakiishutumu Washington kwa kukiuka sheria za kimataifa, na kusisitiza dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika kupinga sera za upande mmoja.
Venezuela imelaani kukamatwa kwa meli zake za mafuta kwenye fukwe zake, ikiishutumu Marekani kwa kutekeleza “uharamia” kama sehemu ya kampeni pana ya kuipindua serikali ya Caracas na kupora rasilimali kubwa ya nishati ya nchi hiyo.