Dar es Salaam. Baada ya kukabiliana na changamoto mbalimbali mwaka 2025, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitauanza mwaka 2026 kwa mbinu mpya za kisiasa zenye lengo la kujiimarisha na kushughulikia changamoto zilizojitokeza.

Kwa mujibu wa chama hicho, mwaka 2026 kitasimamia siasa za kipekee zitakazojikita kwenye mchakamchaka, zikilenga kuhamasisha wananchi na zitakazosaidia wananchi kupata majibu kwa maswali kuhusu utawala bora na demokrasia.

Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini, kimeeleza zaidi kuwa siasa hizo zitakuwa zaidi ya zile za ‘No reforms, no election’, zikionyesha njia mpya ya kushughulikia masuala ya kidemokrasia na usimamizi wa utawala.

Hata hivyo, kimesema uhalisia na undani wa mwenendo, aina ya siasa na mwelekeo wa Chadema kwa mwaka 2026 utafafanuliwa kupitia hotuba kwa Watanzania, inayotarajiwa kutolewa kati ya Desemba 31, 2025 na Januari 2, 2026.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa wakati akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Desemba 30, 2025, kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo mpango na mikakati ya chama ya kuhitimisha mwaka 2025 na kuupokea mwaka 2026.

Golugwa amesema kuwa licha ya matukio ya Oktoba 29, 2025, ambayo chama hakikuyakubali, Chadema bado kimeendelea kuungwa mkono na wananchi, jambo linalothibitisha ushawishi wake katika siasa za upinzani nchini.

 “Kwa imani ya Watanzania walionayo kwa Chadema, siasa za 2026 zitakuwa za kipekee na tofauti, zitakazotufikisha katika Taifa na Watanzania kupata kile wanachokitaka.

“Chadema tupo tayari, tumejiandaa kuongoza hiyo ‘show’ itakayokuwa kubwa zaidi ya iliyotoka ya ‘No reforms no election’. Tunakwenda kwenye kipindi tutakachofanya siasa za mchakamchaka mzito kuliko za ‘No reforms no election,” amesema Golugwa.

Golugwa amesisitiza kuwa, chama hicho kimemaliza kaulimbiu ya ‘No reforms no election, hivyo kinaelekea mwaka 2026 kufanya siasa mpya na za kipekee.

Kwa mujibu wa Golugwa, mwaka 2026 watatoa hotuba iliyosheheni mambo mbalimbali, ikiwemo yaliyotokea mwaka 2025 na mwelekeo wa chama hicho.

“Tunajiandaa kueleza kile wanachokitarajia, hii ni hotuba ya kuufunga na kuufungua mwaka. Ni hotuba itakayoonyesha tunataka nini mbele na tutashika wapi,” amesema Golugwa.

Alipoulizwa nani atakayeitoa hotuba hiyo, Golugwa amejibu, “bado tunaiandaa, tukimaliza tutajua nani ataisoma kwa niaba ya chama.”

Kuhusu suala la rasilimali fedha inayotokana na chama hicho kukosa ruzuku, Golugwa amesema hiyo sio tatizo kwao kwa sababu licha ya magumu walioyoyapitia katika kipindi cha mwaka 2025 unaoisha, bado Watanzania wanakiunga mkono.

“Changamoto ya kifedha si tatizo kwetu, bado tunaungwa mkono na kuaminiwa na wananchi walio wengi,” amesema Golugwa.

Mwaka 2025 umekuwa wa moto kwa Chadema kutokana na kile walichokipitia ikiwemo misukosuko ya viongozi wake wakuu kukamatwa kwa nyakati tofouti, huku mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu akisalia gerezani akikabiliwa na kesi ya uhaini.

Si hilo tu, kwa mara kwanza tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1992, kilishiriki chaguzi zote kuu, lakini katika hali isiyotarajiwa kwenye uchaguzi mkuu 2025 kilisusia mchakato kikishinikiza mabadiliko katika mfumo wa sheria za uchaguzi.

Sambamba na hilo, ni mwaka 2025 ambao Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ilisitisha ruzuku kwenda Chadema, kwa maelezo chama hicho hakina viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na mrejesho wa fedha hizo za umma, baada ya kuwasimamisha karibu watendaji wote wa juu, ikielezwa walipataikana bila akidi ya Baraza Kuu.

Kama hiyo haitoshi, Mahakama Kuu ilitoa amri ya kusimamisha shughuli zote za chama hicho hadi kesi iliyofunguliwa na kiongozi wake wa zamani na baadhi ya wadhamini wake kuhusu mgawanyo wa rasilimali, itakapomalizika.

Zaidi ya hato, Mei 7, 2025, ilishuhudiwa vigogo na makada wa Chadema wakitimka ndani ya chama hicho na kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kwa kile walichodai kuwa ni kutafuta mustakabali wao kisiasa, baada ya kubaini kisingeshiriki uchaguzi.

Vigogo hao ni wale wanaodaiwa kumuunga mkono aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe aliyeshindwa katika uchaguzi wa ndani uliosababisha mtikisiko na ushindani wa aina yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *