Jana Jumanne, kona zote za Iran ya Kiislamu zilishuhudia maandamano makubwa ya wananchi ya kuadhimisha siku inayojulikana kwa jina la Dey 9 ambapo tarehe kama hiyo mwaka 1388 Hijria Shamsia (Disemba 30, 2009) mamilioni ya wananchi wa Iran walimiminika mitaani kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusambaratisha fitna kubwa ya adui.

Miongoni mwa nguzo muhimu zinazouimarisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nguvu za wananchi ambao mara zote wako tayari katika medani za kila namna kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Jana pia vyombo vya habari kutoka mikoa yote ya Iran viliripoti kufanyika maandamano ya wananchi ya kuadhimisha siku hiyo adhimu kwa taifa la Iran na kukumbushia jinsi mwamko wa viongozi na wananchi ulivyofanikiwa kusambaratisha fitna kubwa ya maadui wa taifa hili ya mwaka 2009.

Tarehe 9 Dey kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia ni uwanja wa kudhihirisha heshima, hamasa, mwamko, uhuru na nguvu za wananchi wa Iran kwa walimwengu, na kila mwaka siku hiyo inatumika kutangaza utiifu na uungaji mkono wa wananchi wa Iran kwa mfumo wao wa kiutawala wa Jamhuri ya Kiislamu.

Dey 9 ni somo la milele kwa marafiki na maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na ni ukumbusho kwamba kila pale usalama, umoja na uhuru wa Iran unapotiwa majaribuni, wananchi wa taifa hili hujitokeza kwa mamilioni, kwa mwamko na kwa muono wa mbali, kulihami taifa na nchi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *