s

Chanzo cha picha, Instagram Mange Kimambi

Muda wa kusoma: Dakika 5

Mwaka 2025 uliendelea kuthibitisha nguvu ya mitandao ya kijamii katika kuibua sura mpya za umaarufu, hasa barani Afrika. Watu binafsi waliweza kujijengea majina makubwa kupitia ubunifu, uhalisia na kugusa maisha ya watu wa kawaida.

Miongoni mwa waliotawala mijadala ya mitandaoni mwaka huo ni Mange, Mwandambo, King’amuzi, Dogo Patten, Mama Amina, na Bonge la Dada.

Kwanini hawa?

Mange aliendelea kuwa sauti isiyopuuzwa mitandaoni kwa kutumia majukwaa ya kidijitali kufungua mijadala ya kijamii, kisiasa na haki za wananchi. Umaarufu wake ulitokana na ujasiri wa kusema yaliyo moyoni mwa wengi, jambo lililompa wafuasi wengi na pia wakosoaji.

Mwanamitindo aliyebadilika kuwa mwanaharakati wa siasa, ndie muasisi wa maandamano yaliyotokea octoba 29 kwa kupinga kile anachokiita kuwa ni muendelezo wa ukiukwaji wa haki za binadamu na uminywaji wa haki za kiraia nchini Tanzania.

Amekuwa akihamasisha mabadiliko ya kimfumo ikiwemo tume ya uchaguzi, katiba mpya, kupinga rushwa na viongozi kujilimbikiza mali.

Amekua akitumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii ambayo yanawafuasi wengi kutoka Tanzania.

Mange ni mama wa watoto watatu anayeishi Los Angeles, nchini Marekani. Harakati za Mange kupinga serikali ya Tanzania zilianza tangu wakati wa rais wa awamu ya tano John Magufuli takribani miezi sita tu baada kuingia madakari na rais huyo kupinga kuonyeshwa mubashara kwa mikutano ya bunge. Alijaribu bila mafanikio kuitisha maandamano wakati wa Magufuli Aprili 2018.

Mange, akiwa na wafuasi karibu milioni tatu kwenye ukurasa wake wa Instagram miaka minne iliyopita alitumia umaarufu wake mitandaoni kumuunga mkono Rais Samia alipoingia madarakani baada ya kifo cha mtangulizi wake John Magufuli, na hata kuhudhuria katika ziara yake ya kwanza nchini Marekani na wawili hao walipiga picha. Hata hivyo, mambo yakabadilika na leo hii anautumia ukurasa huo huo na ushawishi wake kumpinga.

Mange ni mmoja wa watu wa awali nchini Tanzania miaka ya mwanzo ya 2000, kufungua blogu na kuzungumzia maisha yake na marafiki zake pamoja na mitindo ya mavazi. Lakini Mange alizungumzia pia habari binafsi mbalimbali za watu maarufu waishio ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo walimbwende, wanamuziki na waigizaji filamu.

Clemence Mwandambo “Nachoka baba yenu”

s

Chanzo cha picha, Instagram Clemence Mwandambo

Mwandambo alipata umaarufu mkubwa kupitia maudhui ya vichekesho na simulizi zinazoakisi maisha ya kila siku, akitumia lugha rahisi, ya moja kwa moja na inayogusa watu wa rika mbalimbali.

Mwaka 2025, alitikisa mitandao ya kijamii kupitia kibwagizo chake maarufu “Nachoka mimi baba yenu Clemence Mwandambo”, ambacho kilipokelewa kwa mvuto na kicheko, na baadaye kuanza kutumiwa na watumiaji wengi wa mitandao kama njia ya kuonesha kuchoshwa, kutoridhishwa au kukosoa hali fulani ndani ya jamii.

Uhalisia na mtindo wake wa kusimulia ulifanya hadhira kubwa ijione ndani ya hadithi zake, jambo lililomjengea ufuasi mpana na wenye hisia ya ukaribu naye. Hata hivyo, umaarufu wake uligubikwa na sintofahamu mnamo mwezi Desemba, baada ya Jeshi la Polisi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Mbeya kuthibitisha kumshikilia Clemence Mwandambo kwa tuhuma za uchochezi, pamoja na madai ya kukashifu imani za Kiislamu na Kikristo kupitia baadhi ya machapisho yake ya mitandaoni.

Hatua hiyo ilizua hisia mseto miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, ambapo wengi walijitokeza kumtetea wakieleza kuwa maudhui yake yalikuwa ya kijamii na ya kiutani zaidi, huku wengine wakisisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika matumizi ya majukwaa ya kidijitali.

King’amuzi

Kijana ambaye alijizolea umaarufu mtandaoni kupitia kuiga kuimba nyimbo mbalimbali za wasanii wa Bongo Fleva hususan Diamond Platnumz na kumfanya watu wamfuatilie na kufurahia vituko vyake na na uchezaji wake anapoimba.

Dogo Pattern

s

Chanzo cha picha, Instagram Dogo Patten

Pia unaweza kusoma

Msanii wa singeli aliyepata umaarufu mkubwa kupitia wimbo wake maarufu “Afande Nilegezee Kamba” aliendelea kupanua wigo wa safari yake ya muziki baada ya kushirikiana na msanii wa lebo ya Wasafi, Zuchu.

Ushirikiano huo ulimfungulia milango mipya katika tasnia ya muziki, ambapo alipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wadau pamoja na kuongezeka kwa ufuasi wake katika mitandao ya kijamii.

Mama Amina

Binti Mtanzania ambaye ni msanii wa singeli alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na mtindo wake wa kipekee wa kuimba singeli kwa lafudhi inayofanana na mtu anayeng’ata ulimi, sambamba na uchezaji wake wa kuvutia jukwaani.

Umaarufu huo ulimuwezesha kutambulika zaidi kitaifa, hatua iliyompelekea kuchaguliwa kuwa miongoni mwa wasanii walioshiriki katika kampeni za kumtangaza mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, kuanzia mwezi Agosti hadi Oktoba.

“Bonge la dada”

s

Chanzo cha picha, Instagram Queen Aviola

Jina halisi Queen Fraison mzaliwa wa Mbeya nchini Tanzania.

Ni mnenguaji aliyepata umaarufu kupitia mitandao ya kijamii kwa kuonesha umahiri wake katika mitindo mbalimbali ya kunengua, akitumia miondoko na mitikisiko ya mwili wake kwa ustadi mkubwa.

Umahiri huo ulimfanya kujipatia ufuasi mkubwa mtandaoni. Umaarufu wake uliongezeka zaidi baada ya msanii Mboso kuachia wimbo “Aviola 2025”, ambapo Bonge la Dada alionekana kwenye video hiyo akiinogesha kwa mitindo yake ya kunengua, jambo lililovutia mashabiki wengi zaidi.

Aidha, aliendelea kuimarisha ushawishi wake kwa kucheza na kusambaza video za nyimbo mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii.

Mwaka 2025 umeendelea kudhihirisha nguvu kubwa ya mitandao ya kijamii katika kubadili maisha ya watu wengi, hususan vijana walioweza kujipatia ushawishi mkubwa mtandaoni.

Umaarufu walioupata kupitia ubunifu wao katika muziki, uchezaji, au maudhui mbalimbali uliwafungulia fursa za kipato, matangazo na ushirikiano uliowawezesha kujikimu kimaisha kama alivyoeleza Bonge la Dada kupitia mojawapo ya mahojiano na vyombo vya habari nchini Tanzania.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, baadhi yao walijikuta wakikumbana na changamoto, ikiwemo kuingia kwenye migogoro ya kisheria kutokana na matumizi yasiyo na mipaka ya umaarufu wao au kuvuka maadili na sheria za jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *