
Kwanza, nitoe salamu zangu, za Bi Mkubwa, na watoi tunapofunga na kuanza mwaka. Kipekee, nichukue fursa hii kuwakumbuka na kuwaombea ambao hawakuumaliza wala hawatauona mwaka mpya waliokufa ima kwa vifo vya kawaida au vya kufyatuliwa, waliotekwa, na kupotezwa hata waliowafanyia kitu mbaya nikiwataka waache na kumaliza na kuanza mwaka kwa nia safi kabisa.
Tumalize mwaka na kuuanza mwingine kwa usalama si kwa kufungana kamba na kuumizana au kuitwishana mkenge.
Turidhiane kweli kweli na si kuridhishana na kuendeleza upuuzi ule ule ili tusionekane hamnazo wala wanafiki waliojitoa ufahamu. Aaaamina.
Nije kwenye inshu. Mafyatu walipofyatua, si walifyatuliwa hadi kukawa kufyatuana! Baada ya kugundua kuwa kufyatuana na kufyatukiana hakuwafikishi mbali, sasa nasikia kamba za usuluhishi! Usuluhishi au usulutishi? Nani anasuluhishwa na nani na kwanini na ili iweje? Nifyatue wazi.
Ili kuepuka kuendelea kufyatua, kufyatuana na kufyatuliwa, lazima huu usuluhishi uwe usuluhishi. Nani anataka usulubishi tena kwa usulutishi, ulushi na magumashi?
Kama profesa emeritus wa migogoro na utatuzi wake, leo nafyatua lecture ya bure. Najitolea bure lau kusaidia mafyatu na kaya yetu tusiendelee kufyatuana na hata kunyotoana roho.
Kitaaluma, tuna kitu kinaitwa give and take kinacholenga kufikia win-win situation. Ili kufikia hapa, mosi, lazima wahusika wawe wakweli.
Wakubwa na wadogo hukosea. Waelezane ukweli kwa ukweli na uhuru na si kuzidiana ujanja, ujanja ujanja, na sanaa. Pili, waathirka lazima wapewe nafasi ya ku-vent au kutapika nyongo.
Tatu, lazima watuhumiwa wawe na kifua si cha kupinga au kufyatuana bali kuwasikiliza wale waliowafyatua na kuomba msamaha au kuwajibika. Nne, lazima kuwepo na yule tunayemuita third party ambaye sina kimakonde chake. Huyu, lazima awe ni fyatu anayeaminiwa au wanaoaminika na wahusika wote. Sitaki niwachoshe na lugha za kitaaluma na kifyatu.
Sasa, nini kifanyike?
Hapa, kuna mambo kadhaa muhimu ya kufanya ndiposa usuluhishi, siyo usulubishi wala usulutishi, uanze.
Mosi, lazima tukiri kosa au makosa ambayo, kimsingi, ndiyo yanayosukuma kuwapo usuluhishi.
Pili, lazima iundwe tume, si timu ya kufadhiliana, kulindana, kupendeleana, na kupeana ulaji wa dezo ya kuchunguza kadhia nzima.
Je, nani aiunde? Ili hii tume ikubalike kwa pande zote, lazima wahusika washirikiane kuiunda kuepuka na kuepusha mtuhumiwa au mhalifu kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, karani wa mahakama, mahakama, na hakimu katika kesi yake.
Kwa waliosoma sharia, kimakonde, hii, ni katazo na uvunjaji wa haki usio kifani. Huitwa ‘nemo judex in causa sua.’
Tatu, kwa kuangalia mambo yanavyokwenda ambapo upande mmoja unataka kuutwisha mwingine mkenge uonekane makenge, nimewiwa kufyatua hii kitu lau nifungie na kufungulia mwaka.
Hapa, nasisitiza kuhusu kuundwa kwa tume ya maridhiano si maridhishano, usuluhishi, siyo usulutishi n usulubishi.
Nasema wazi. Tume yoyote ambayo haiakisi haya si tume bali timu ya kupendelea wale walioiunda ili kuwaepushia lawama wanazostahiki.
Hapa, walalamikiwa lazima wakubalia lawama na kufanya hivyo siyo makosa wala udhaifu bali nguvu. Kimsingi, timu kama hii haitatua tatizo bali kulikuza. Inakosa kile ambacho kimakonde tunaita impartiality, yaani kutoegemea upande. Tukumbuke, amlipaye mpiga zumari ndiye huitisha wimbo. Tahadharini hili.
Nne, suala jingine nyeti ni je, ni nani amchunguze nani na kupata nini? Hapa, niseme wazi. Kama tutaamua kusuluhishana, tusuluhishane na si kusulutishana ili tusipoteze fursa na muda.
Kuna usemi kuwa sometimes, a conflict can present an opportunity if it is addressed constructively.
Hivyo, tutafute chanzo cha yote na kukishughulikia kisayansi na kwa nia safi tukijiapiza na kuapa kutorudia uzwazwa uliotufikisha tulipofikishwa na waliotufikisha pale.
Tano, baada ya uchunguzi huru na wa kweli kukamilika, linakuja suala na swali la nani awe mshitaki na nani awe mshitakiwa?
Tulenge kuepusha ukenge wa mshitaki kuwa mshitakiwa na mshitakiwa kuwa mshitaki kama ilivyo kwa sasa ambapo mkosefu anamlaumu aliyemkosea tena bila aibu wala sababu isipokuwa ukosefu wa aibu, utu, na mizania kimamlaka.
Kwenye usuluhishi wa kweli, pande mbili zinakuwa na hadhi na kutenzwa sawa bila kujali nani ni nani.
Sita, tukimaliza kujua pande mbili husika ambazo kimsingi na kitaaluma, ndizo hufanya kesi iwe ya kimahakama au ya usuluhishi, tunakuja na suala jingine.
Je, nini adidu za rejea? Bila kuwa nazo, mambo mengi yasiyopaswa yataibuliwa na kufanya usuluhishi kuwa usulubishi kwa wasuluhishaji. Mwisho, tukifanya hayo, tukumbuke. Pande mbili husika zina hasira na nyingine hata jinai. Hivyo, kila fyatu atajitahidi kuja na za kuja ili aonekane hana makosa. Je, nani atamfunga paka kengele bila kufanyiwa au kufanyiana ukenge?
Heri ya Mwaka Mpya.