
Iran imetangaza kulitambua Jeshi la Wanamaji la Canada kama shirika la kigaidi, ikijibu uamuzi wa huko nyuma wa Ottawa wa kuliorodhesha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) kama kundi la kigaidi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema hayo jana Jumanne.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema hatua hiyo imechukuliwa chini ya sheria ya ndani inayotaka kuchukuliwa hatua za kujibu maigo dhidi ya nchi zinazounga mkono au kufuata kibubusa hatua ya Marekani ya kuiorodhesha IRGC kama shirika la kigaidi. Wizara hiyo imesema uamuzi wa Canada ulikiuka kanuni za kimsingi za sheria za kimataifa kwa kulitaja tawi rasmi la Jeshi la Iran kuwa ni kundi la kigaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Tehran imechukua hatua kwa kuzingatia kanuni ya kujibu mapigo ya Kifungu cha 7 cha Sheria ya mwaka 2019, ambacho kinasema kwamba, “nchi zote ambazo kwa njia yoyote ile zitafuata au kuunga mkono uamuzi wa Marekani wa kulitambua Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kama shirika la kigaidi zitachukuliwa hatua za kujibu mapigo.”
Ikumbukwe kuwa, Canada ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran na kufunga ubalozi wake wa Tehran katika hatua ya kushtukiza mwaka 2012, ikitaja vijisababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uungaji mkono wa Iran kwa Syria, miradi yake ya nyuklia, na madai ya tisho kwa utawala wa Israel.
Mnamo Juni mwaka jana, Ottawa iliiorodhesha IRGC kama shirika la kigaidi, hatua ambayo ililaaniwa vikali na serikali ya Tehran. Ndani ya mwaka huo huo, Ottawa ililiondoa kundi la kigaidi la Munafiqeen (MKO) kutoka kwenye orodha yake ya mashirika ya kigaidi.
Hivi karibuni, Alireza Tangsiri, Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) akikaribisha kurejea nchini msafara wa tano wa manowari za Iran baada ya kukamilisha kazi maalumu ziliyopewa alisema: “leo Vikosi vya Wanamaji vya Jeshi na IRGC, vinavyofanya kazi kwa kutegemea imani na azma thabiti na kwa kutumia uwezo wao wa kiulinzi na wa kijeshi wa kisasa na wa kuzuia hujuma, ni jinamizi kwa maadui wa eneo na wa nje ya eneo.