
Dar es Salaam. Kampuni ya Bima ya First Assurance Company Limited, imekimbilia Mahakama Kuu ya Tanzania, kupinga hatua ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), kuijulisha kuwa leseni yake inatarajiwa kusitishwa ndani ya miezi sita.
Kupitia maombi namba 21841 ya 2025 ya kuomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama, Jaji Hussein Mtembwa wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, amekubali maombi ya kampuni hiyo.
Katika uamuzi alioutoa Desemba 23, 2025 ambao umepakiwa katika tovuti ya mahakama Desemba 29, 2025, ameipa kampuni hiyo siku 14 iwe imefungua shauri la maombi ya mapitio kupinga uamuzi wa Tira.
“Kwa masilahi ya haki na kuzuia madhara zaidi, amri ya kusitisha utekelezaji wa maagizo yaliyomo katika barua iliyoandikwa Julai 15, 2025 inatolewa hadi pale maombi ya msingi ya mapitio ya mahakama yatakapoamuliwa,” amesema jaji.
Kampuni hiyo imekwenda mahakamani kutokana na barua ya Tira ya Julai 5, 2025 inayokusudia kufuta leseni ya bima ya kampuni hiyo baada ya miezi sita na kuongeza muda ambao mwombaji atakuwa chini ya mwongozo wa kisheria.
Mwombaji kupitia maombi ya kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama, barua ya Tira anayodai ilitolewa kwa upande mmoja na bila mashauriano, iliitaka kampuni hiyo iongeze mtaji wa Sh15 bilioni.
Vilevile, Tira ambaye alikuwa mjibu maombi wa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kama mjibu maombi wa pili, aliitaka kampuni hiyo kulipa majukumu yaliyosalia ya bima ya Sh5.8 bilioni.
Mwombaji pia anadai kupitia barua hiyo, Tira iliitaka kampuni hiyo inayojishughulisha na bidhaa mbalimbali za bima zikiwamo za magari, moto, bahari na ya uhandisi, kulipa madai ya bima ya jumla ya Sh7.8 bilioni.
Katika majibu yao, wajibu maombi kwa kiasi walipinga madai hayo, wakikubali baadhi ya mambo yaliyodaiwa na mwombaji.
Walieleza maagizo yametolewa ikiwa ni utaratibu endelevu wa kudhibiti uzingatiaji wa matakwa ya kisheria na kwamba, uamuzi huo umefikiwa kutokana na vikao vya mashauriano kati ya mwombaji na Tira.
Mbali ya hayo, walieleza mlalamikiwa wa kwanza anaweza kumteua meneja yeyote wa kisheria kutekeleza majukumu, kulingana na aina ya suala hilo.
Wakati wa usikilizaji wa maombi hayo, mwombaji aliwakilishwa na wakili Jonathan Mndeme, wakati wajibu maombi waliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Ditrick Luambano na Oscar Malya.
Hoja za kisheria
Akijenga hoja ili kupata kibali cha mahakama, Mndeme alieleza sheria za Tanzania zinasema ombi la kufungua maombi ya mapitio ya mahakama siyo la moja kwa moja, bali kuna vigezo vya kutimizwa.
Moja ni kwamba, ni lazima mwombaji aonyeshe kuna kesi ya kujadiliwa na kuna ukiukwaji wa Katiba ya nchi au ukiukwaji wa haki, hakuwa na mamlaka, siyo ya kisheria au kuna ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa.
Wakili huyo alieleza kwa kutazama kiapo cha mwombaji na majibu ya wajibu maombi, inaonyesha wazi kuwa maombi hayo yamekidhi vigezo vya kisheria vilivyowekwa na maombi hayo yamewasilisha ndani ya miezi sita.
Alieleza mteja wake ana hoja za msingi zinazohitaji kuamuliwa na mahakama na kwamba, sheria inataka kuwe na usikilizwaji wa haki kabla ya kufanya uamuzi wowote ambao unakwenda kuathiri haki za kisheria za mwombaji.
Alinukuu ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Tanzania ambayo inaeleza kuunyima upande haki ya kusikilizwa kunafanya uamuzi uwe batili.
Alieleza kiapo cha mwombaji kinaonyesha hapakuwa na notisi yoyote ya kuwepo usikilizwaji au uchunguzi wa suala linalobishaniwa hadi kufikia uamuzi wa kusitisha leseni ya kampuni hiyo ya bima.
Wakili huyo alieleza ukweli unaonyesha ukiukwaji wa wazi wa haki ya asili, haki za kikatiba na kupindukia kwa mamlaka kulikofanywa na Tira.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Killaghai alieleza maombi hayo hayana mashiko, akaiomba mahakama kuyatupa akisema ili mtu au taasisi iwasilishe maombi ya aina hiyo ni lazima yafunguliwe ndani ya miezi sita.
Alieleza ni lazima aonyeshe ana masilahi na suala hilo na kuna kesi ya kubishaniwa. Alisema barua ya Julai 5, 2025 ilikuwa ni maelekezo halali ya kisheria ya usimamizi na siyo ubatilisho.
Ameeleza barua hiyo ilitolewa baada ya ushiriki wa kina, taarifa ya awali, mikutano na uteuzi wa meneja wa kisheria na kwa hivyo, madai ya mwombaji kunyimwa haki ya kusikilizwa na ukosefu wa suluhisho mbadala ni ukweli na haikubaliki.
Uamuzi wa Mahakama
Jaji Mtembwa ameeleza wakati anajiandaa kuandika uamuzi alibaini Desemba 19, 2025, wajibu maombi waliwasilisha pingamizi mbili za awali ambazo baada ya kusikilizwa alizitupilia mbali.
Kuhusu maombi hayo, amesema ameyazingatia kwa ujumla wake, amepitia mabishano ya kisheria, hati za viapo na mawasilisho ya mawakili wa pande zote mbili na swali linabaki, maombi hayo yana mashiko?
Akiegemea misimamo ya kesi zilizokwishaamuliwa, amesema mwombaji asiwe mtu wa kutojali au kuchoka wakati wa kuomba kibali na ni lazima airidhishe mahakama zaidi kuwa ana kesi inayobishaniwa ikiwa ruhusa itatolewa.
“Ni lazima aonyeshe ni kwa namna gani ameathirika na kitendo au uamuzi unaopingwa. Ile kufungua maombi ndani ya muda uliowekwa (ndani ya miezi sita) inaonyesha namna mwombaji ameathirika ndiyo maana ameleta ombi,” amesema.
Amesema baada ya kupitia maombi hayo, ameridhika yamefunguliwa ndani ya muda wa kisheria na yamekidhi vigezo vya kisheria vya kupewa kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama, hivyo anayakubali.
Ametoa siku 14 kwa mwombaji kuwasilisha maombi ya mapitio ya mahakama na kutoa amri ya kuzuia utekelezaji wa maagizo ya Tira hadi mahakama itakaposikiliza maombi yatakayofunguliwa na kuyatolea uamuzi.