SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) lina msemo wake maarufu ‘Play Fair, Be Positive’ ukiwa na maana kwamba ‘Cheza kwa Haki, Kuwa Chanya’.
Sasa katika kuhakikisha mchezo wa mpira wa miguu unakuwa wa haki au kiungwana katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026 yanayoendelea kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, kuna zawadi ya Mchezaji Muungwana ambapo katika kila mechi anakabidhiwa Sh500,000 kwenye hatua ya makundi.
Kiasi hicho cha fedha ambacho kinakwenda hadi Sh1 milioni hatua ya nusu fainali na Sh2 milioni fainali, kinatolewa na mdhamini mkuu wa mashindano hayo, Benki ya NMB.
Hali hiyo imewapa mzuka wachezaji kwa kucheza kistaarabu kwani hadi kufikia sasa kabla ya jana, zilikuwa zimepigwa mechi tatu, hakukuwa na kadi yoyote iwe nyekundu au njano kutokana na wachezaji kucheza kiungwana.
Hii inatoa tafsiri ya kwamba, kila mchezaji anapoingia uwanjani anakuwa mlinzi wa mwenzake na kuepusha kuchezeana rafu hatarishi na kuepuka kuadhibiwa na waamuzi.
Akizungumzia zawadi hiyo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Mohamed Kabwanga ambaye pia ndiye msemaji wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, amesema imekuja kuongeza chachu ya kuufanya mchezo wa soka kuwa wa kiungwana zaidi.
Kabwanga amesema zawadi hiyo inatoa taswira kwamba, mchezo wa mpira wa miguu sio vita bali ni burudani ambayo inapaswa kutazamwa na kufurahiwa na kila mmoja.
“Tumekuwa tukitoa zawadi hii ambayo kila mchezaji anapewa laki tano na Benki ya NMB ambaye ndiye mdhamini mkuu wa mashindano haya.
“Kupewa kiasi hiki cha fedha kwa mchezaji mwenye nidhamu maana yake ni kwamba inampa chachu mchezaji mwenyewe lakini hata kuhamasisha kwa wengine kwa sababu mpira wa miguu ni wa haki.
“Wakati tunasema hivyo tufanye kwa vitendo, tuone wale wachezaji wanacheza mpira lakini watambue kuwa unapaswa kumjali mwenzako, ucheze kistaarabu na kadhalika.
“Sasa unapompa zawadi kama kumpongeza, utakuwa umemuimarisha katika kucheza kwa haki, lakini itawashawishi wengine kuwa kama mwenzao wanapokuwa ndani ya uwanja na kuboresha zaidi mchezo wa mpira wa miguu kuvutia kuuangalia.
“Mpira wa miguu sio vita, bali ni mchezo ambao watu wanapaswa waufurahie na anayestahili kushinda ashinde.
“Kwahiyo kwenye hili tuwapongeze NMB kwa kuweka mzigo huo wa shilingi laki tano kila mechi naamini itaongeza ushawishi wa ustawi wa mchezo wa mpira wa miguu kupitia mashindano haya,” amesema Kabwanga.
Naye Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard, amesema: “Kama Mdhamini Mkuu wa NMB Mapinduzi Cup, tutashirikiana na Kamati ya Maandalizi katika maeneo makuu ya maandalizi na uendeshaji wa mashindano, ambapo baadhi ya tutakayofanya ni pamoja na kukabidhi zawadi kwa mshindi wa tuzo za Fair Play katika kila mchezo.
“Kwa hatua ya makundi, NMB itatoa tuzo hiyo sambamba na pesa taslimu Sh500,000 kwa Mchezaji Mwenye Nidhamu, kiasi ambacho kitaongezeka na kuwa Sh1,000,000 kwenye hatua ya nusu fainali na Sh2,000,000 kwenye mechi ya Fainali mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.”
Katika mechi tatu zilizochezwa Desemba 28, 2025 na Desemba 29, 2025, wachezaji waliofanikiwa kupewa zawadi hiyo ni Aimar Hafidh ‘Haaland’ wa Mlandege dhidi ya Singida Black Stars, Yakoub Said Mohamed kutoka Muembe Makumbi katika mechi dhidi ya Fufuni na Michael Joseph wa KVZ walipocheza dhidi ya TRA United.