Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 7
Mwaka 2025 ulikuwa mwaka wenye matukio makubwa na ya kihistoria yaliyoacha alama katika jamii, taifa na dunia kwa ujumla. Kuanzia siasa, uchumi, usalama, michezo hadi masuala ya kijamii na teknolojia, kulishuhudiwa mabadiliko, mafanikio na changamoto zilizounda mwelekeo wa maisha ya watu wengi.
Matukio haya si tu ya kukumbukwa, bali pia yanatoa mafunzo na tafakari kuhusu tulipotoka, tulipo, na tunakoelekea. Haya ni baadhi ya matukio makubwa ya kukumbuka mwaka 2025.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alifunua ukurasa mpya katika historia ya maendeleo ya taifa kwa kuzindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuijenga Tanzania yenye uchumi imara, jamii jumuishi na ustawi kwa wote.
Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dodoma, ambapo Rais Samia amebainisha kuwa utekelezaji wa dira hiyo utaanza rasmi Julai 1 mwaka 2026, mara baada ya kukamilika kwa Dira ya Maendeleo 2025.
Katika hotuba yake, Rais Samia amesema kuwa Dira ya 2050 inalenga kuwa dira ya kizazi kijacho kwa kulenga sekta muhimu kama kilimo, viwanda, madini, utalii, uchumi wa buluu, michezo, ubunifu na huduma za kijamii, ambazo zitachochea ukuaji wa sekta nyingine na kuongeza thamani ya uzalishaji wa taifa.
Amesema thamani halisi ya dira hiyo itapimwa kupitia utekelezaji wa sera, bajeti na maamuzi ya kila siku ya serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla. Huku akisisitiza kuwa huu si wakati wa kusema bali ni wakati wa kutenda.
Katika uzinduzi huo, Rais Samia ametoa maagizo mahususi kwa wizara zote nchini kupitia upya sera zao na kuhakikisha zinaendana na maudhui ya Dira ya 2050, huku akiiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya uchambuzi wa sheria zinazohitaji maboresho ili kuwezesha utekelezaji wake.
Katika kuelekea malengo makuu ya kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu, yenye pato la taifa la zaidi ya Dola trilioni moja na pato la mtu mmoja la Dola 7,000 kwa mwaka, Rais Samia amesisitiza haja ya mabadiliko ya fikra, mitazamo na vitendo. Akibainisha kuwa hakuna nafasi ya kufanya kazi kwa mazoea na kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja katika utekelezaji wa dira hii. Rais Samia amemtaja Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, kuwa msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Dira ya 2050, akibeba jukumu kubwa la kuhakikisha dira hii inatekelezeka.
Pia, Rais Samia ameeleza kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi, hivyo serikali itaweka mazingira rafiki kwa maendeleo ya sekta hiyo, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa dira hii unahitaji ushirikiano wa karibu baina ya serikali, sekta binafsi na jamii nzima. Rais katika hotuba yake ameagiza kuandaliwa kwa mkakati wa mawasiliano, elimu kwa umma na uhamasishaji kuhusu Dira ya 2050 ili kuhakikisha kila Mtanzania anaifahamu na anashiriki katika ujenzi wa taifa.
Aidha, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika masuala ya kimataifa kwa kulinda maslahi ya taifa katika mazingira mapya ya dunia. Amesema kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi isiyofungamana na upande wowote, lakini yenye msimamo thabiti katika diplomasia ya kimataifa, maendeleo ya kijamii, utunzaji wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Mhe Rais ametoa wito kwa taifa kutumia teknolojia kwa manufaa ya maendeleo, huku tukilinda ajira na ustawi wa watu wote.
Rais Samia amesisitiza pia umuhimu wa taasisi za kisheria na haki za binadamu kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dira hii kwa kuhakikisha usawa, haki, uwajibikaji na utawala bora. Amesema kuwa Tanzania ya miaka 25 ijayo lazima ijengwe juu ya msingi wa haki, maadili na utamaduni wa uwajibikaji wa kitaifa.
Uzinduzi wa daraja refu na fursa ndefu za kikanda
Chanzo cha picha, URT
Juni 19, 2025, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi daraja la JPM maarufu kama daraja la Kigongo – Busisi, ambalo sasa ni moja ya alama kubwa za miundombinu barani Afrika.
Daraja hilo limeiweka Tanzania kwenye ramani ya bara kwa kuwa daraja refu zaidi Afrika Mashariki na kati, na la sita kwa urefu katika bara lote la Afrika. Lakini kwa maana ya kimkakati, kiuchumi, kijamii, na kijiografia, daraja hili lina uzito wa kipekee unaolihusisha mataifa zaidi ya sita.
Daraja hili si la Mwanza pekee ni la kanda ya ziwa na zaidi. Linaunganisha mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga, na Simiyu. Zaidi ya Watanzania milioni 15 wananufaika nalo moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Shirika la takwimu la Tanzania (NBS) kanda ya Ziwa, ambayo inachangia zaidi ya 20% ya pato la taifa, sasa ina nafasi mpya ya kuongeza thamani ya bidhaa zake kupitia viwanda vya usindikaji vilivyopo na shughuli nyingine za uchumi, zikiwemo biashara, uvuvi, na kilimo.
Kilimo cha mazao ya biashara (pamba, kahawa, mahindi), uvuvi (hasa sangara), na biashara ya samaki baridi ndizo nguzo kuu, kama anavyosisitiza aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega:
“Sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta yenye mchango mkubwa wa ukuzaji uchumi wa nchi, sekta hii imezalisha zaidi ya ajira milioni 4.5 zinazojumuisha wavuvi wa asili na wakuzaji na wakulima wa mwani na kusaidia kwa kiasi kikubwa kwenye usalama wa chakula”.
Kwa mantiki ya kijiografia na kiuchumi, daraja limefungua lango la biashara kuelekea mataifa ya Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, DRC na hata Sudan Kusini kupitia barabara kuu ya Central Corridor.
Hii ina maana biashara za kimataifa kupitia bandari ya Mwanza zitaongezeka kwa kiwango kikubwa. Kwa mujibu wa ESRF Economic Outlook 2023, takribani 40% ya mizigo ya kibiashara ya Uganda hupitia Ziwa Victoria, sehemu kubwa ikielekezwa Mwanza.
Biashara kati ya Uganda na Tanzania ilikua kwa kasi na kufikia takribani dola za kimarekani bilioni 2.23 mwaka 2024. Kukamilika kwa daraja hili kunasaidia kuongeza idadi ya mizigo ya transit kupitia Mwanza kwa kiwango cha hadi 60% kufikia mwaka 2027 na kuendelea kukuza biashara kati ya nchi hizi na nyingine jirani.
Uganda ni mfano tu, lakini Kenya, Rwanda, Burundi, DRC na hata Sudan Kusini wanafanya daraja hili kuwa daraja muhimu la kuchochea fursa za kiuchumi.
Daraja JPM (Kigongo-Busisi) limesitisha matatizo mengi ikiwemo muda wa kuvuka kutoka dakika 30 mpaka 60 mpaka ndani ya dakika 4 tu kwa gari, na dakika 15 kwa miguu. Tena kwa usalama, uhakika na kwa kiwango cha barabara ya kisasa.
Uchaguzi Tanzania
Chanzo cha picha, Getty Images
Oktoba 29, 2025, ilikuwa siku muhimu kwa Tanzania, siku ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani tukio la kikatiba linalotazamwa kama kilele cha demokrasia ya taifa.
Samia Suluhu Hassan alishinda kwa 98%, katika uchaguzi huo.
Lakini mwaka huu, siku hiyo hiyo ilichukua sura mbili. Wakati serikali na vyama vya siasa vinawahimiza wananchi kujitokeza kupiga kura, makundi mengine yaliyojitambulisha kama wanaharakati yanahamasisha maandamano, wakisema ni njia ya kupaza sauti zao dhidi ya kile wanachokiona kama kukwama kwa mageuzi ya kisiasa.
Wito huu wa pande mbili uliibua mjadala mpana kuhusu namna Watanzania wanavyotafsiri demokrasia yao. Kwa upande mmoja, wapo walioamini ushiriki katika uchaguzi ni njia bora ya kuleta mabadiliko ndani ya mfumo uliopo.
Kwa upande mwingine, wapo walioona mfumo huo huo umekuwa kikwazo cha mageuzi, hivyo kuamua kuutumia uchaguzi huo huo kama jukwaa la kutoa ujumbe wa kutoridhika kwao.
Jeshi la Polisi nalo lilisisitiza kuwa wito wa maandamano uliashiria kuleta vurugu na na kuwa yalikuwa ya kuvunja sheria. “Atakayevunja sheria Oktoba 29 asilaumu”, alisema Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime.
Maandamano ya 29 Oktoba
Chanzo cha picha, Getty Images
Oktoba 29, 2025, inatajwa kuwa siku yenye madhara makubwa ya kisiasa nchini Tanzania.
Tukio hilo lilileta uharibifu wa mali, vifo vya watu na majeraha ambayo bado yamesalia kuwa kumbukumbu ngumu vichwani mwa wengi.
Wengi wanakumbukumbu ya kuona na kusikia kuhusu vifo na majeruhi kadhaa. Kibinadamu inawapa kumbukumbu ya kutisha.
Ingawa kwenye mitandao, ukiwasikiliza vijana wa Gen z, hawaonyeshi sana kujali hili.
Pia watu walikosa huduma muhimu kwa karibu siku tano, wakiwa wameachwa na maumivu ya kihisia na kimaisha. Biashara zilifungwa, huduma zilikosekana na kwa ujumla yalikuwa maisha ya adhabu kwa wengi.
Katika mazingira haya, maandamano yoyote yanayokumbusha tukio hilo yaliweza kuwa na uzito wa kipekee.
Hamasa ya kujieleza kwa baadhi ya wananchi ilikosa kushinda hofu ya matukio yaliyopita, na hali ya kutokuwa na uhakika mara nyingi hushusha uwezekano wa umma kuchukua hatua za pamoja.
Tangu baada ya maandamano ya Oktoba 29, maelfu ya vijana walikamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya uhaini, ambayo ni kosa kubwa sana nchini Tanzania na lenye adhabu kubwa ikiwa mtu atathibitishwa, yaani adhabu ya kifo.
Ingawa wanasheria walikosoa mashtaka hayo wakisema hayana msingi wa kisheria, hali hii ilisababisha baadhi ya vijana kujitathmini.
Tangu Oktoba 29, kauli mbalimbali zilikuwa zikitolewa na viongozi wa serikali, dini, polisi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Wengine walihimiza kuandamana kama haki ya kiraia, wengine wakionya kuhusu uwezekano wa vurugu.
“Inakuonesha njia muhimu ni kusikiliza, kuruhusu watu waongee bila woga, watoe madukuduku yao, halafu serikali ifanyie kazi”, anasema Rehema Mema, mchambuzi
Rehema anatoa mfano wa Zanzibar, ilitumika njia hiyo ya mazungumzo kwa zaidi ya mwaka mzima mara baada ya ghasia za maandanao ya Januari 2001, na kuzaa maridhiano yanayoiweka Zanzibar Pamoja mpaka leo.
Rais Samia aliwahi kuonya kuelekea Desemba 9 kwamba Serikali imejipanga: “Likija wakati wowote, tumejipanga. Tutasimama na kuilinda nchi hii kwa nguvu zote.”
Kauli za viongozi na uwepo wa nguvu zilizotumika Oktoba 29 vimechochea tahadhari miongoni mwa vijana waliokuwa na nia ya kuandamana.
Polisi pia waliweka wazi kuwa maandamano hayo yamepigwa marufuku na ni haramu, hali iliyoonesha wazi kwamba hatua yoyote ya kinyume cha sheria inaweza kudhibitiwa kabla haijaanza.